Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2017/2018.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kabla sijachangia ninaunga mkono hoja ya Kambi ya Upinzani, nafikiri ripoti yetu iko sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapoendelea nataka nimpongeze Waziri, Mheshimiwa Ummy Mwalimu, nafahamu amefanya kazi kwenye NGO’S, hiyo peke yake inamsaidia kum-shape na kumfanya akafanya kazi vizuri ikaweza kumsaidia kidogo.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumzia na Wabunge wenzangu wengi wamezungumzia matatizo ya mimba za utotoni. Tumepiga kelele tukijua kwamba mimba za utotoni janga la Taifa hili, kila Bunge linalopita tunazungumzia habari hii. Ndugu yetu amepeleka kesi Mahakamani ameshinda lakini Serikali imekata rufaa. Mheshimiwa Ummy Mwalimu, kuweka alama katika Wizara yako tusikubali sisi kama wanawake, kwa namna yoyote, iwe ya dini, iwe ya mila, itakayopelekea watoto wakapata shida katika umri mdogo na kupewa mimba. Ninaomba tupambane na tukubaliane kabisa, hatutakubali watoto wetu wakiolewa, sasa hivi inafika mpaka miaka tisa watoto wameingizwa kwenye ndoa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninakupongeza pia kwa kuanzisha kanzidata katika Wizara yako kwa upande wa mambo ya kijinsia, nafikiri hilo ni suala la kukupongeza. Bado kuna shida, tunapofanya udahili, kwenye hotuba yako ukurasa wa 81 umeelezea jinsi tutakavyofanya udahili wa wanafunzi katika Vyuo vya Udaktari, watoto wa kike ambao tumewashawishi wasome sayansi wanapokuwa vyuoni hawana pesa za kulipia mikopo japokuwa wanafanya vizuri darasani na tunajua kabisa tuna uhitaji mkubwa sana wa madaktari katika Taifa letu. Ukienda Chuo cha Kairuki kuna wasichana wameacha shule mwaka wa pili kwa kushindwa kulipa ada za masomo yao. Tunawezaje kusaidia wanawake hawa na Wizara hii kama ni Wizara husika ikawasaidia wasichana wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kukumbusha, Wizara ikahamasisha uanzishwaji wa nyumba salama (safe home), hizi nyumba salama zitasaidia wasichana wadogo, wanawake ambao wamefanyiwa ukatili wa kijinsia wakati wakishughulikiwa masuala yao, wapate sehemu sahihi ya kusubiri, wakati mambo yao yakishughulikiwa. Ninafikiri Wizara hii ni wakati muafaka sasa wa kuhamasisha. Kuna wadau binafsi wamejitokeza na wameanza, nachukua nafasi hii kumpongeza huyu Dada Janeth Mawinza wa Mwananyamala, yeye amejaribu kuwa na safe home kwa ajili ya wale akina mama wanaopigwa au wale wasichana ambao wanafanyiwa ukatili na baadaye wakaenda wakawahifadhi. Wizara lazima mtambue watu kama hawa, lakini ni wajibu wenu wa kuanzisha vituo kama hivi.(Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie suala la wanawake na uchumi. Hii Wizara inazungumza mambo ya wanawake na kuwatetea. Leo hii tunazungumzia Benki ya Wanawake binafsi nimefanya kazi na Benki ya Wanawake. Mwaka jana Mheshimiwa Ummy ulimwambia Meneja atoe maelezo jinsi gani anafanya kazi, sasa sikujua kama ni siasa au alikupa maelezo na wananchi haujatupa mrejesho ulifikia wapi. Benki hii ina-charge kama benki za kawaida. Inatoa riba kubwa kama benki za kawaida, jina lake ni tofauti na matumizi ya wanawake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule kwetu Mbeya benki hii ina mawakala, lakini Mikoa kama Mbeya, Mwanza, Mikoa mikubwa lazima ingekuwa na matawi makubwa na kuweza kusaidia wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wengi wamezungumza vijijini ambako kuna asilimia kubwa ya wanawake benki hii haijafika, tutaendelea kufanya siasa au tutaendelea kusaidia wanawake.

Ninaomba Mheshimiwa Ummy pamoja na Mkurugenzi wa Benki ya Wanawake fanyeni hima…

(Hapa kengele ililia kuashiria kuisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.