Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Amb. Adadi Mohamed Rajabu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. BALOZI ADADI M. RAJAB - MWENYEKITI KAMATI YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nashukuru sana kwa kupata nafasi hii kumalizia hii hoja. Hoja hii imechangiwa na Waheshimiwa Wabunge 29. Waheshimiwa Wabunge 23 wamepata nafasi ya kuzungumza na sita wameweza kuleta kwa maandishi. Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge michango yao yote tutaichukua na kuboresha kwenye maazimio yetu. Nawashukuru pia Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Waziri kwa michango yao ambayo ni muhimu sana kwenye Kamati hii ambayo inajumuisha karibu Wizara tatu na nne. Mheshimiwa Mwenyekiti, nawashukuru pia wana Kamati wenzangu, wamefanyakazi nzuri sana na wengine kwa kweli wamekuwa na roho ngumu; hata tulipoingia kwenye Magereza na kuwaona wafungwa na mahabusu jinsi walivyo, wengine machozi yaliwatoka. Nawashukuru sana kwa kuwa wavumilivu. Mheshmiwa Mwenyekiti, amani na utulivu katika nchi yoyote ile ni jambo la msingi sana. Tukichezea amani na utulivu, naamini hatuwezi kukaa. Kuna mifano mingi sana ambayo ipo kwenye ulimwengu huu. Nchi ambazo zimechezea amani na matokeo yake wanayaona na wasingeweza kukaa hata kwenye ukumbi wa Bunge kama hivi. Sisi kama Kamati yetu tutajaribu kwa kadri tunavyoweza kushauri Serikali namna ya amani na utulivu umuhimu wake unavyotakiwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, majukumu haya ambayo yote yapo kwenye Wizara hizi; za Mambo ya Ndani na Mambo ya Ulinzi na Usalama yanahitaji fedha; lakini kwenye Wizara zote hizi tatu ambazo tumezizungumza zote zimeonekana kuna upungufu wa fedha. Fedha ambazo zimepitishwa na Bunge lako Tukufu hili, zimeshindwa kuwafikia wahusika ili waweze kufanya shughuli za maendeleo. Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati imetembea kwenye baadhi ya Magereza na baadhi ya Magereza mengine tumekuta wafungwa wanadai vyombo, zana za kufanyia kazi ya kilimo. Wanasema tunaomba matrekta, tuna ardhi iko hapo imejaa na tuna hela zetu. Ni Gereza la Songwe wanasema tuna hela zetu shilingi milioni 40 ziko kule kwenye akaunti, tupeni tununue matrekta. Sijui kwa nini, nafikiri Waziri wa Fedha na Waziri wa Mambo ya Ndani, atakuwa analisikia. Toeni hizo hela na kuacha huo urasimu, wapeni wafungwa walime.
Mheshimiwa Mwenyekiti, msongamano wa mahabusu kwa kweli ni tatizo kubwa sana. Kama nilivyosema kwenye taarifa yetu, kuna watu wamekaa Magerezani kwa miaka mine mpaka mitano kwa makosa ya mauaji na madawa ya kulevya; kitu ninachongojewa ni kitu kinaitwa High Court Session. Polisi na Mahakama zimefanya kazi nyingi sana za kesi ndogo ndogo, bado hizi kesi kubwa. Mahakama Kuu kuna nini? Kwa nini hambadilishi taratibu za kuangalia kubadilisha huu mfumo wa High Court Session ambao unawaweka mahabusu muda mrefu ndani ya Magereza? Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, kuhusu, msongamano wa mahabusu ambao unaambatana na hiyo kwa kweli ni suala ambalo linatakiwa lishughulikiwe. Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, Waheshimiwa Wabunge wamezungumza na tumetoa mapendekezo na maoni ambayo tunaona ni muhimu yaweze kuchukuliwa, isipokuwa cha msingi ni fedha ziende kwenye Balozi nje ya nchi. Mabalozi kule hawana hela. Hela tumepitisha lakini haziendi. Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa mabalozi watatumika sana kwenye diplomasia ya uchumi. Wao wana uwezo mkubwa sana wa kuleta Wawekezaji hapa na watalii. Tuwapelekee fedha, tuwawezeshe waweze kufanya hayo mambo. Hii ni pamoja na Mabalozi ambao wako hapa nje; nyumba nyingi tu; mfano huo wa Sweden ni mmoja, lakini nyumba nyingi za Mabalozi ziko kwenye hali mbaya na zinahitaji kuboreshwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimepata mchango wa Mheshimiwa Bilago. Warundi wamejaa kwenye Gereza la Kibondo, kwa sababu pale ni mpakani, huwa kuna utaratibu wa mikutano ya ujirani mwema. Waburundi wanakuja na sisi tunakwenda, tunanunua vitu na wao wananunua vitu. Sasa wanapokuja wale, unawakamata kwamba wameingia nchini isivyo halali, unawajaza kwenye Magereza, kwa kweli siyo haki. Waziri wa Mambo ya Ndani na Serikali iliangalie hilo ikafanye mikutano ya ujirani mwema kuondoa hilo tatizo. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Polisi wanafanya kazi nzuri sana na mpaka sasa hivi wamepunguza uhalifu kwa kiwango kikubwa sana, tukichukulia uhalifu in totality; lakini hawana nyenzo. Bajeti ambayo tumeipitisha hapa kuwapa fedha, hawajapata hizo hela, au kama wamepata, zote zimekwisha. Sasa tusiwafanye Polisi wawe ombaomba, isipokuwa naitaka Serikali iangalie hilo suala na kuhakikisha fedha ambazo tumepitisha hapa, basi Polisi wale wanapewa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Madawa ya kulevya ni tatizo kubwa, watoto wetu wameharibika, Watanzania wanakamatwa sana huko nje. Sisi tunaweza kuwafuatia Nigeria sasa hivi. Kwa hiyo, wamejaa kwenye Magereza ya nje, ni vita. Nami naomba tutakaporudi kwenye Majimbo yetu tuwasaidie kutoa taarifa ya wote wanaohusika na madawa ya kulevya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, Makamanda wa Mikoani wa Polisi na Makamanda wa Wilaya, wana jukumu kubwa sana la kuwasaidia Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Ni lazima wafuate taratibu za upelelezi. Taratibu za upelelezi zipo wazi. Upelelezi ni profession jamani. Kuna doctorate ya investigation inachukuliwa. Upelelezi hauendi hivi hivi. Huwezi ukatoa upelelezi kwa kutaja watu majina, hakuna! Mimi sijawahi kuona kitu kama hicho. Kwa hiyo, ninachotaka kusema ni kwamba Makamanda wa Polisi na wa Wilaya, waangalie. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, zipo Police General Orders, Police Force Ordinance na Criminal Procedure Act ambazo zinaeleza kabisa namna ya Polisi kutekeleza majukumu yake. Kwa hiyo, kinachotakiwa ni kukaa pamoja na hao Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kuwasaidia. (Makofi) Waheshimiwa Wabunge, mtakumbuka wakati Mheshimiwa Lyatonga Mrema alipokuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, mimi nilikuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam na alifanya kazi kubwa sana, lakini kulikuwa na kazi nyingine anakwenda nje, kinyume. Nikasema tukimwacha Mheshimiwa Lyatonga aende hivi, ataharibu kesi Mahakamani. Ikabidi Wakuu wakae na Mheshimiwa Mrema, wakaelekezana taratibu za kufanya na Polisi walimpa support na mambo yakawa yanakwenda vizuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nashauri kwamba Makamanda wa Polisi wa Mikoa na Wilaya wakae na Wakuu wa Mikoa wao na Wakuu wa Wilaya zao, waangalie na kuwashauri namna ya kugawanya hizi kazi. Hawa Makamanda wamesomea, wanaelewa. Wamekwenda kwenye vyuo mbalimbali, wanaelewa taratibu. Hatutaki waharibu hizi kesi nzuri au hii operation nzuri ambayo imeanza ili kesi hizi ziende kufa kule Mahakamani. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge kwamba yote ambayo mmeyaongea na kushauri tutayachukua na tutaweka kwenye maazimio yetu na ninawahakikishia kwamba tutaunda Kamati Maalum ya kufuatilia yote ambayo tumeyasema ili kuhakikisha kwamba kabla hatujatoa report nyingine mwaka kesho, basi tutatoa utekelezaji wa maazimio haya. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, kwa niaba ya Kamati ya Mambo ya Nchi za Nje, Ulinzi na Usalama, napenda kuwasilisha taarifa yangu na naomba kutoa hoja.