Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Andrew John Chenge

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Bariadi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. ANDREW J. CHENGE – MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA SHERIA NDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipatia fursa hii niweze kuhitimisha hoja yangu, hoja ya Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo. Niwashukuru sana Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Niwashukuru sana waliochangia kwa kuongea humu Bungeni, Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, Mheshimiwa Mlinga na Mheshimiwa Aida Khenani. Pia kuna Waheshimiwa Wabunge wamechangia hoja hii kwa maandishi ambao ni Mheshimiwa Lucia Mlowe, Mheshimiwa Zuberi Kuchauka na Mheshimiwa Juma Othman Hija. Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaongea kwa kifupi sana. Ukimuona nyani mzee porini ufahamu kwamba amekwepa mishale mingi sana. Kwa hiyo, ndugu zangu hii ndiyo hali ya maisha. (Makofi/Kicheko) Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewasilisha hoja hii, Waheshimiwa Wabunge mtakapopata fursa isomeni, hoja ya msingi hapa ni kwamba Sheria Ndogo ni sheria halali za nchi hii na zinawagusa wananchi wetu katika maisha yao ya siku hadi siku. Mimi nashukuru sana uamuzi wa Mheshimiwa Spika kwamba Kamati hii iwe inapewa fursa ya kuwasilisha taarifa yake mapema kabla ya taarifa zote. Kwa sababu tusipofanya hivyo kama mnavyoona sasa hivi wananchi wataendelea kuumizwa tu kwa sheria ambazo zina dosari na ambazo zingeweza kurekebishwa. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Rais wetu amesema ziko kodi, ada na tozo nyingi sana kwenye mazao hasa ya biashara, hilo ni agizo, tunategemea kwamba Wizara zenye sekta hizo watafanya haraka ndani ya uwezo wao kuzipitia zile sheria na kanuni, kama msingi wake uko kwenye sheria mama basi wafanye marekebisho kupitia sheria mama kuleta Muswada wa Marekebisho hapa Bungeni. Kama ni kwenye Sheria Ndogo ndiyo unachukua nafasi ya Kamati hii kuyaleta mapema ili tuweze kuyapitia tuyanyooshe twende mbele. Hivyohivyo kwa maelekezo ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, maelekezo mazuri sana ameyatoa alipokuwa katika ziara Mikoa ya Kusini. Maana tukiacha hizi zitaendelea kutumika, ni sheria. Kwa hiyo, nimeona hilo niliseme kwa sababu linatuhusu sote. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Hija ameshauri tu kwamba labda Kamati ya Sheria Ndogo itusaidie hii migogoro ya wafugaji na wakulima, mtoe mchango wenu kwa hilo. Napenda sana hiyo lakini hali halisi sio hivyo. Kamati hii inafanya uchambuzi wa Sheria Ndogo ambazo zimewasilishwa hapa Bungeni na Serikali. Ombi langu kwenu kama viongozi, kwa sababu tatizo hili ni kubwa, tukianzia chini kwenye maeneo yetu katika kutunga au kupendekeza maoni yetu ya kutunga Sheria Ndogo ambazo zitasimamia matumizi bora ya ardhi, Sheria Ndogo hizo ndiyo zitaweza sasa kufanikisha hilo ambalo Mheshimiwa Juma Othman Hija anapendekeza lakini sisi hatuwezi kwenda tukafanya kazi ambayo siyo sehemu ya majukumu ya Kamati hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, la elimu, kuwawezesha wanasheria, kwanza wanasheria kwenye Serikali za Mitaa au Halmashauri zetu tumelisema kwenye taarifa, hiyo ndiyo inachangia dosari nyingi ambazo zinaonekana katika Sheria Ndogo hizi. Hata hivyo, mimi najua uandishi wa sheria ni taaluma ya kipekee na ndiyo maana hata kwenye Ofisi ya Mwanasheria Mkuu ni wachache na wale wazuri, hii siyo feature ya Tanzania tu, nenda kokote ndani ya Nchi za Jumuiya ya Madola tatizo hili lipo, kwa sababu hawa is a special breed, wanafunzwa namna ya kuandika. Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ili uweze kufika ile grade tunayoitaka lazima uwe una uzoefu mpana sana wa sheria lakini pia na masuala ya kijamii sasa kuwapata hao itatuchukua muda. Hata hivyo, tukasema tunapendekeza angalau kwa wanasheria waliopo katika Halmashauri zetu wakinolewa kila baada ya muda kama walivyofanya juzi hapa Dodoma, wamefanya semina ya wanasheria wote hawa waliletwa hapa, ya siku tatu, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu imetoa inputs zake, wanasheria wa TAMISEMI wametoa inputs, ndivyo inavyotakiwa, labda itatusaidia sana katika kuimarisha uandishi wa sheria. Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesema vizuri, jamani Ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali, ofisi kwanza yenyewe ni hatari. Serikali imetoa ahadi na sisi tunaamini kabisa kwamba ahadi ni deni tunategemea tuone ndani ya muda mfupi ofisi hiyo inaboreshwa kiutendaji lakini kwa vifaa vya kisasa. Maana haya tunayoyasema ya kuwasilisha Sheria Ndogo kwa mujibu wa Kanuni ya 37(2) na kwa mujibu wa kifungu cha 38 cha Sheria ya Tafsiri yanategemea ofisi ya Mpigachapa Mkuu wa Serikali. Kama hajafanya utakuwa unaonea Serikali kwamba kwa nini hamjaleta mawasilisho yenu Bungeni, lakini acha tuone. Kuna mchango mzuri tu wa Mheshimiwa Kuchauka, yeye anasema hawa wananchi wanaokaa karibu na hifadhi ndiyo wanasaidia kutunza hifadhi hizi lakini tunapata mapato kiduchu asilimia 25. Sasa yeye anapendekeza waongezewe, hayo ni ya kwenu huko, sisi tunasimamia Sheria Ndogo kama itakuja na mapendekezo hayo na yamekubalika kule itakuwa ni uamuzi wenu. Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme moja, Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa, Sura ya 290, kupitia Bunge la bajeti mwaka wa fedha 2011/2012 wote mliokuwa Bungeni mnakumbuka, yaliletwa marekebisho ya kuongeza cess ya mazao ili watoze kwa kuangalia hali halisi ya Halmashauri yako, kati ya asilimia tatu mpaka asilimia tano. Hata hivyo, ukweli wa mambo, hakuna Halmashauri nchini ambayo imetoza chini ya asilimia tano, zote zimepiga ile ceiling. Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa Kamati, ingawa siyo la kwetu lakini tunayaona, tumemwambia na Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI kwamba kama malalamiko ni haya hebu tujitahidi basi tukaweka ifahamike. Maana sasa hivi mmewapa ile leeway wanapiga mpaka kwenye ceiling, ni afadhali ikafahamika kama ni asilimia tano iwe asilimia tano, kama ni mbili au tatu iwe tatu, tutakuwa tumeiweka sheria katika msingi mzuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, nisingependa nipigiwe kengele ya pili, kazi hii tumeianza, tunaomba Kamati hii iendelee kuungwa mkono kwa kuwezeshwa. Hawa wajumbe wa Kamati hii kazi yao ni kusoma documents. Wenyewe pia ili waweze kuifanya kazi hii vizuri lazima wawezeshwe vizuri. Tofauti na baadhi ya wajumbe ambao ni wanasheria kama akina Mheshimiwa Ridhiwani, Mheshimiwa Ngeleja na wanasheria wengine lakini wengine hawa siyo wanasheria na siyo lazima uwe mwanasheria kuweza kuzifanya kazi hizi lakini ukisaidiwa ukawasikia wale ambao wamebobea katika masuala haya mtakuwa mmeisaidia sana Kamati hii. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, nisichukue muda wako mwingi, tuna mambo mengi sana leo, lakini niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliotuunga mkono. Nami nimalizie kwa kusema maoni na mapendekezo yote ambayo yamo kwenye taarifa ya Kamati sasa Bunge lako iyakubali kama Maazimio yaliyopitishwa na Bunge. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.