Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Dr. Hussein Ali Mwinyi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kwahani

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji na Taarifa ya Mwaka ya Shughuli za Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

WAZIRI WA ULINZI NA JESHI LA KUJENGA TAIFA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nami naomba nianze kuchangia hoja hii kwa kuishukuru Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kwa ushirikiano mkubwa wanaonipa mimi pamoja na watendaji wangu. Nataka niwahakikishie kwamba tutaendelea kushirikiana nao. Aidha, nawapongeza kwa kazi nzuri wanayoifanya. Tumekuwa tukifanya kazi pamoja nao tukitembelea maeneo mbalimbali na tunawashukuru sana kwa usimamizi wao na ushauri wao kwa Wizara yangu. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja kadhaa ambazo zimetolewa na napenda nianze na zile za Kamati kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la beacons kutokuwepo katika mipaka yetu. Ni kweli hili ni tatizo la muda mrefu lakini napenda niseme kwamba hatua zimeanza kuchukuliwa. Tumechukua hatua za aina mbili. Kwanza ni mazungumzo kati ya Wizara zinazohusika kwa upande wetu wa Tanzania pamoja na ule upande wa majirani zetu. Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi hii imekamilika kwa mpaka wa Tanzania na Kenya na beacons zimeanza kurudishiwa na mazungumzo yapo katika hatua nzuri kwa upande wa Tanzania na Uganda. Ni mategemeo yetu kwamba baada ya kukamilika kwa mazungumzo hayo, basi tutarusha zile beacons na kuweka buffer zone ili wananchi wasiingilie ile mipaka kisheria.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati pia imeeleza juu ya suala la marekebisho ya Sheria ya JKT ili iweze kutoa fidia kwa vijana wanaoumia wakiwa kwenye mafunzo. Hili tunalikubali, ni ushauri mzuri sana na ni kweli kwamba wapo vijana wanaopata matatizo ya kiafya na wengine wanaoumia kupitia yale mazoezi yanayofanyika kule. Kwa hiyo, ni jambo ambalo na sisi tunalipokea na tutafanya utaratibu wa kufanya marekebisho ili waweze kupata fidia iwapo watakuwa wameumia wakiwa katika mafunzo. Mheshimiwa Mwenyekiti, kulikuwa na hoja ya idadi ya vijana wa JKT waliochukuliwa mwaka huu. Napenda nitoe taarifa kwamba vijana waliochukuliwa kwenda JKT ni wa aina mbili; wale wa mujibu wa sheria ambao mwaka huu idadi yao ni 14,748 na wale wanaojitolea wamechukuliwa 9,848. Kwa hivyo, hao ndiyo ambao wamepata nafasi safari hii. Tunatambua kwamba idadi hii ni ndogo na inabidi tuwachukue wengi zaidi hususani wale wa mujibu wa sheria na tutaendelea kujenga miundombinu katika makambi yetu ili tuweze kuwa na uwezo mkubwa zaidi wa kuweza kuwachukua walio wengi zaidi. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hoja hizo za Kamati sasa niingie kwenye hoja za Waheshimiwa Wabunge mmoja mmoja na nianze na ile ya Mheshimiwa Rweikiza ambaye ametaka kujua ni kwa nini hatujasaini na ku-ratify ule Mkataba wa Biological Weapon Convention. Nataka nimpe taarifa Mheshimiwa Rweikiza kwamba kuna mikataba ya aina hii miwili; wa kwanza ni ule Chemical Weapons Convention na wa pili ni Biological Weapons Convention. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Chemical Weapons Convention tulishasaini na tumeshauridhia, kwa hiyo, pale tumemaliza. Kwa upande wa Biological Weapons Convention kusaini tulishasaini kilichobaki ni kuridhia na ku-domesticate kwa maana ya kwamba kuingiza katika sheria za nchi ili uweze kutumika katika sheria za nchi. Kazi hiyo inaendelea na iko katika hatua ya Cabinet Secretariat ili hatimaye iweze kufika Bungeni. Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mattar alitoa mapendekezo kwamba asilimia ya vijana wanaochukuliwa kuingia JKT kutoka Zanzibar basi angalau ipatikane asilimia kumi ya wale wa jumla wanaochukuliwa. Tunaweza kusema kwamba kwa sasa hivi au kwa mwaka huu Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ilipewa nafasi 300 na tunaona umuhimu wa kuongeza nafasi hizo. Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nimuahidi kwamba mwaka hadi mwaka tutaendelea kuwa tunaongeza idadi hii japo siyo kwa kufikia asilimia kumi ili tuweze kupata vijana wengi zaidi kutoka upande wa pili wa Jamhuri yetu, lakini wakati huo huo lazima tujenge miundombinu zaidi ili tuweze kupata idadi kubwa zaidi ya vijana wanaoingia katika Jeshi la Kujenga Taifa. Mheshimiwa Mwenyekiti, naye vilevile alishauri kwamba badala ya utaratibu unaotumika sasa ule wa kupitia Wilayani na Mikoani alishauri kwamba pengine vijana wachukuliwe kutoka JKU. Ambacho naweza kumwambia Mheshimiwa Mbunge kuhusu hili ni kwamba uamuzi wa jambo hili upo juu ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yetu sisi au mimi kama Waziri wa Ulinzi huwa napeleka nafasi zile kwa Makamu wa Pili wa Rais na tunawaachia jukumu la kuamua wao wanataka kutumia utaratibu gani. Mpaka sasa wamekuwa wakizigawa Wilayani na Mikoani. Kwa hivyo, naweza kumshauri Mheshimiwa Mbunge kwamba ni vyema akazungumza na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kuangalia utaratibu kama huo wa JKU utakuwa ni bora zaidi. (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna hoja ya Mheshimiwa Zitto Kabwe ya kuhusu Kanali Kashmir kwamba hajastaafishwa rasmi. Kwanza nataka nimpe taarifa ya kwamba Kanali Kashmir ni kweli alikuwa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania na cheo chake kilikuwa ni Chief of Logistics and Engineering (CLE) na sio Chief of Staff. Chief of Staff wakati wake yeye cheo hicho hakikuwepo ni baada ya yeye kutoka mwaka 1974 ndipo kilipoanzishwa cheo cha Chief of Staff. Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachosema ni kwamba kuhusu maslahi ya kustaafu ni suala la kisheria. Kama ni kweli kuna uthibitisho kwamba Kanali Kashmir hajalipwa jambo hili litaangaliwa kisheria aweze kupata mafao yake. Hata hivyo, taarifa nilizokuwa nazo ni kwamba wakati anatoka Jeshini kwenda SUDECO fedha za Jeshi alikuwa ameshapata na baada ya kustaafu kule SUDECO alitakiwa alipwe upande ule ule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo mengine nitayaleta kwa maandishi. Naunga mkono hoja na ahsante sana.