Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Venance Methusalah Mwamoto

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kilolo

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. VENANCE M. MWAMOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kukushukuru wewe na kukupongeza kwa kufika huu mwaka salama kwa sababu kuna wakati kidogo afya iliyumba, Mungu akubariki kwa sababu tunakuhitaji. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nianze kuwapongeza Mawaziri wote, Mheshimiwa dada yangu Kairuki pamoja na Mheshimiwa George Simbachawene na Mheshimiwa Waziri wa Sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia katika Utawala Bora. Kabla sijaanza kuchangia nitoe pole sana kwa wananchi wa Jimbo la Kilolo kwa accident ya bus ya Vitu Laini ambayo ilitokea hivi karibuni na kuua watu wengi na jana pia ndege moja ndogo ilianguka katika Jimbo la Kilolo, nawapa pole sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia; jana Mheshimiwa Rais alipokuwa kwenye shughuli ile ya haki kuna kitendo ambacho kilitokea pale, kitendo cha yule mama ambaye alipiga kelele alihakikisha kwamba anapata nafasi ya kuongea na Mheshimiwa Rais, lakini ukifuatilia malalamiko ambayo yule mama alikuwa anayalalamikia ni utawala bora. Kwamba ameingia kila mlango lakini alikosa kusikilizwa na kupewa haki zake. Ameingia Mahakama zote yule mama ameshindwa kusikilizwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichokuwa najiuliza hivi ni akinamama wangapi hasa wajane ambao wanakosa haki zao? Je, watakuwa na ujasiri kama ule? Hii ni changamoto kwetu viongozi kwamba kama hatuwasikilizi watasubiri mpaka Mheshimiwa Rais atakapokuja kwenye mikoa yetu na wilaya zetu ndipo wasimame haki zao zipatikane. Naomba Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia tunafanyaje jambo hili. Kuna watu wale wa Haki za Binadamu nafikiri wapo, kile kitengo nafikiri kikiimarishwa kikapewa nguvu kingeweza kusaidia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia ukienda Mahakamani kesi zinachukua muda mrefu, ukienda mahabusu na magereza zetu zimejaa, lakini ukienda pale kesi ambazo mimi nikiri nilishawahi kuwa Mkuu wa Wilaya, nilikuwa naingia mara kwa mara kwenye magereza, unaweza ukashangaa kesi nyingine siyo za mtu kukaa mahabusu, ukikaa pale utashangaa. Nafikiria sasa ni wakati muafaka Jeshi la Polisi na Mahakama wakashirikiana, sio lazima mtuhumiwa akituhumiwa leo lazima akamatwe leo, upelelezi unaweza ukafanyika akiwa hata bado hajakamatwa, wakati anakamatwa basi moja kwa moja upelelezi unakuwa umekamilika na haki inatendeka, aidha, kuachiwa au kufungwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi wamelalamika kuhusu utendaji wa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya. Kwanza nianze kwa kuwapongeza kwa sababu wenyewe wamekiri kwamba hawajapata semina. Mimi niwape tu semina kidogo ndugu zangu hasa Wakuu wa Wilaya kwa sababu na mimi nilikuwa Mkuu wa Wilaya, kwamba maamuzi yao yazingatie taratibu na haswa washirikishe Kamati zao za ulinzi na usalama, siyo kuanza tu kutoa maamuzi bila kushirikisha ile Kamati ya ulinzi na usalama. Naamini wakishirikisha Kamati ile basi busara zitatendeka.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia washirikishe vyombo na taasisi za dini, kuna wazee maarufu, linapotokea jambo haina haja ya kukurupuka, lazima usikilize pande zote mbili ndipo utoe maamuzi. Kwa sababu kuna baadhi ya watu ambao ni watendaji wazuri tunaweza tukawapoteza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia awamu hii imesaidia sana kutia nidhamu kwenye kazi. Leo hii ukienda Ofisi yoyote ukikaa pale kwenye benchi huwezi kukosa mtu wa kuja kukuuliza kwamba bwana una shida gani, umesikilizwa? Kwa hiyo, nikupongeze Mheshimiwa Kairuki kwamba sasa watumishi wanaanza kurudi kwenye line isipokuwa tu Wakuu wa Wilaya, Wakuu wa Mikoa na Watendaji wengine wapunguze, wawasiliane.
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili linasikika sana kwa sababu nao kwa kiherehere wanataka kila jambo litoke kwenye vyombo vya habari, mambo mengine yanakuwa kimya kimya, ukitaka kila kitu kitoke madhara yake ndiyo hayo. Hiyo nidhamu ni nidhamu ya uwoga, waache uwoga wafanye kazi wataonekana tu. Mheshimiwa ameshajua nani atabaki na nani ataondoka, wasiwe na wasiwasi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni suala la TASAF. Niseme wazi kwamba suala la TASAF ni kitu kizuri, niwapongeze sana TASAF kwa kazi nzuri ambayo wanafanya. Mimi ni Mjumbe wa TAMISEMI tumezunguka mikoa mingi, tumeangalia kazi ambazo zinafanyika na nyingine ukienda kama Pemba kule unaweza kushangaa mambo ambayo wanayafanya, wameenda mbali zaidi na sasa hivi wanafanya na mambo ya uchumi kwa kutumia fedha zile.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nafikiri kwa kuwa baadhi ya sehemu kumeonekana kuna matatizo turekebishe yale matatizo, tatizo kubwa lipo kwa Watendaji wa Halmashauri zetu, kwa sababu hawa Watendaji ndiyo wanapelekewa pesa, kwa hiyo, wao kwa sababu ya mazoea ya miaka ya nyuma walishindwa kubadilika. Sasa hivi nafikiri tukae tuone tunafanyaje ili TASAF iweze kusonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nikiri wazi hata Waheshimiwa Wabunge mmeona msongamano wa wale watu ambao walikuwa wanahitaji msaada kwetu umepungua, umepungua kwa sababu ya TASAF; wengi wanakuwa wamemaliziwa matatizo yao huko.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mwisho kabisa ni ajira. Tunashukuru sana kwa kazi ambayo mmeifanya, mmefanya uhakiki vizuri sana tena tunakuombea na Mungu akubariki. Sasa kazi iliyobaki ni ajira maana vijana ambao tumewasomesha sasa wasije wakaingia kwenye mambo mengine mabaya, juzi Dangote alitangaza kazi za udereva walioomba wengi ni kutoka Vyuo Vikuu kwa sababu hakuna kazi. Kwa hiyo, nafikiri wewe tangaza ajira na hivi umeshaanza basi wengi watapata na mimi niombe kwa kupitia nafasi hii vijana watulize munkari kwamba ajira sasa zitamwagwa na Serikali yetu hii itatujali. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwa sababu muda ninao nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu. Kwa kweli kazi aliyoifanya ni kubwa, mabadiliko tunayaona na mwenye macho haambiwi tazama anaona mwenyewe, kazi iliyobakia ni sisi kuwasaidia. Tuwasaidie tufanye kazi tuwe kitu kimoja ili tusonge mbele.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania kanyaga twende, ahsante kwa kunisikiliza.