Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Desderius John Mipata

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nkasi Kusini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. DESDERIUS J. MIPATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. Nishukuru pia Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Viongozi wa Kamati zote mbili kwa namna walivyotoa taarifa zao nzuri na inaonekana kwa kweli ni taarifa nzuri za kufanyia kazi. Katika kuunga mkono nina maeneo mawili ya kuchangia na nikipata nafasi naweza nikachangia eneo la tatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la kwanza ni suala la Utawala Bora. Suala la utawala bora kwa kadri wenzangu walivyokwisha kulisema kwa kweli ni kitu ambacho siyo cha ku-acquire mtu hivi, ni kitu ambacho lazima mtu aandaliwe. Ni vizuri Viongozi wakapata mafunzo, bila kuwapa mafunzo mambo yataenda mchakamchaka lakini athari zake mtaziona kubwa mno. Hii haitatusaidia katika nchi. Watu wapate mafunzo katika ngazi zote kuanzia Vijiji, Wilaya Mikoa na Taifa, ni muhimu sana. Natoa mfano mmoja wa jambo ambalo limeniathiri, katika eneo langu ambalo nadhani ni maagizo ya kupokea halafu watu hatuwezi kukaa tukaona athari ili tuone tunaweza tukashauri ngazi za juu namna gani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kwanza, nina shule yangu moja inaitwa Mirundikwa, shule ya Sekondari. Shule hii imejengwa kwenye majengo ambayo yaliachwa na Jeshi miaka ya 1998. Kwa kutoa barua kukabidhi vijiji kwamba eneo hilo linaachwa na Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi ligawiwe vijiji na mimi nilikuwa kwenye Kamati mojawapo ya kugawa vijiji vinavyozunguka eneo lile lililobaki. Eneo hilo lilikuwa ni shamba la Mirundikwa State Farm zamani, Wanajeshi walipoingia mwaka 1998. Walipoingia na kukomesha shughuli zao mwaka 1998 wakaliacha eneo na Halmashauri mwaka 2000 wakaanza kulitumia, tukagawana na kuanza kujenga miundombinu, tukajenga shule nzuri sana ya sekondari katika suala la kuondoa kero hizi za elimu kulingana na jinsi mnavyotuagiza. Tumejenga shule nzuri sana, imefikia kiwango cha form six.
Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi tumeambiwa kwamba tarehe 1 Januari shule hiyo inafutwa, itafutwe sehemu nyingine Wanajeshi wanaenda pale. Shule hii ilikuwa inafanya vizuri sana katika Wilaya ya Nkasi, ni moja kati ya High School iliyokuwa inafanya vizuri sana. Takwimu zinaonesha tu hapa mwaka jana kulikuwa na mchepuo wa HGK, HGL na HKL, wasichana peke yake walikuwa 32, division one tulipata wanne shule ya kwanza hiyo, division two tukapata 14 na wote waliobaki ni division three. Kwa hiyo ilikuwa ina-perform vizuri sana na wananchi wakaiunga mkono wakaendelea kujenga miundombinu mbalimbali.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wametuparaganyisha kwa maagizo ya haraka kwamba sasa shule itoke ili lianzishwe jeshi hapo. Sisi tunaomba mtuachie hii shule tumeijenga wenyewe, katika kutafuta wananchi wetu waweze kupata elimu, waweze kuishi maisha bora. Hata hao wanaotoa maamuzi kama wasingepitia shule, wasingekuwa na ubavu wa kutoa maamuzi haya. Jambo hili mimi limeniumiza sana katika eneo langu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nataka kusema kwamba, athari zimepatikana kubwa zaidi ya watoto mia tatu hamsini na kitu hawana pa kwenda, wamepata athari ya kisaikolojia, wanaanza kwenda shule moja, moja wamegawanywa kwenye shule mbalimbali za Wilaya yetu jambo ambalo litapunguza sana performance yao. Sasa jambo hili lazima kuliangalia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi inalazimika leo kutenga bajeti yake imetumia zaidi ya milioni 50 kutoka kwenye vyanzo vyao kwa hiyo haiwezi kuendesha shughuli zake zingine. Kwa mujibu wa Mthamini ni zaidi ya milioni 871 zinatakiwa, hii milioni 871 zinatakiwa ili kurejesha miundombinu kwenye shule ambayo tunaijenga upya ambayo tunajenga katika eneo la Kasu. Sasa wananchi waliokuwa wamemaliza shughuli zao, wamemaliza wakaanzisha mpaka shule ya high school leo wanaanza upya, Serikali haina mchango hata kidogo, kwa kuanza upya hii ni athari kubwa sana na watu wameathirika na kwa namna hiyo hawawezi kuipenda Serikali yao.
Mheshimiwa Mwenyekiti, maamuzi ni mazuri lakini utaratibu huu unaweza kuwa na lengo zuri la kiusalama lakini athari zinazopatikana kwa wananchi mziangalie nazo. Halafu shule hii ni ya wananchi, tumejenga wenyewe na hawajatushirikisha kutoa mawazo ili shule hii iendelee. Naomba Waziri anayehusika hili jambo aliangalie kwa makini sana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo tuna athari kubwa, Halmashauri na wananchi wana kipato kidogo, walijikusanyia wakajenga miundombinu mingi mpaka ikawa shule nzuri yenye Kidato cha Sita sasa hakuna shule tena. Maeneo ya Jeshi yapo, ungesema acheni sekondari tafuteni maeneo mengine sisi tungewapa eneo lingine, kwa nini msifanye hivyo mchukue shule yetu? Haiwezekani.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale Luwa Sumbawanga kuna eneo ambalo lililkuwa la Jeshi zamani na halijaathirika chochote na lipo mpaka sasa, waliliacha kama la kwao na wala hawakulikabidhi kwa wananchi. Kwa nini wasichukue hata eneo hilo lingeweza kufanya hiyo kazi? Kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Rais aisikie habari hii na Viongozi wote ambao mnahusika mtuchangie, kama mnataka lazima iwepo shule Wizara ya Elimu leteni hela. Wizara ya Ulinzi ambayo mnataka tujenge sekondari pale leteni hela! Waziri Mkuu uliyeamua katika utekelezaji wa shughuli za Serikali shule yetu ifutwe tuliyojenga wenyewe tuletee pesa tujenge kwenye Sekondari yetu ya Kasu. Wananchi wanafanya kazi za kilimo na kadhalika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni suala hili la Utawala Bora. Kuna kijiji changu kinaitwa kijiji cha Kasapa, ni kijiji cha asili kilianzishwa miaka ya 1960. Mwaka 2010 kwa Tangazo la Serikali Na. 301 kimekuwa kijiji kamili na sisi tunategemea kilimo. Juzi tarehe Mosi mwezi Januari watu wa TFS wameenda kusema kijiji hiki kiko kwenye msitu wao, maeneo yote ya watu wanayolima ambayo ni mashamba wamesema ni maeneo yao, kwa hiyo, mazao yamefyekwa katika maeneo yale! Katika kipindi hiki ambacho hali ya chakula ni tete!
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejaribu kuongea nao na wakati huo nikaenda hata kwa Mkuu wa Mkoa kuona uwezekano wa maeneo hayo ambayo zaidi ya hekta 2000 zimelimwa mahindi wayaachie angalau miezi minne ili waweze kuvuna na kuondoka kama ni lazima wakati taratibu nyingine zinafanyika. Wamenikatalia, sikusikilizwa hata na Mkuu wa Mkoa kwa kweli!
Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo hili limenifadhaisha na limefadhaisha wananchi. Kijiji kile kilitupa kura sisi, mimi na Mheshimiwa Magufuli kiwango cha juu, tuseme watu wote walitupatia kura. Leo hii wanashangaa kuona Mbunge wao hana uwezo wa kutetea jambo hilo angalau kwa miezi michache! Hatujasema tumekataa, tumesema angalau miezi ambayo watu wamelima mazao tayari! Kwa nini wafyeke mazao yote! Nimeenda kushuhudia wamefyeka ekari 15 zaidi ya hekta 2000 kwa mujibu wa Mhifadhi mwenyewe na yenyewe wamesema hakuna mtu wa kuingia na hakuna mtu anayeingia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo Kaya 395 zimeathirika na wala hawaendi shamba wamekaa tu. Watu zaidi ya 2000 ambao wanategemea kilimo katika kijiji kile hawatakuwa na chakula, mjiandae kutuletea chakula.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejitahidi kwa kadri nilivyofanya, nimeshirikiana na DC, nimeshirikiana na Mkuu wa Mkoa, lakini haikuzaa matunda! Nikaenda kumwona Mtendaji Mkuu wa TFS nikamwelezea hoja anaielewa, lakini anakuwa mwoga nadhani bila shaka, baadaye alisema hapana, imeshindikana! Hii ni kuogopa! Mazingira yanayofanywa na Watendaji mimi nafikiri ni ya uwoga bila sababu kwa sababu, Mheshimiwa Rais ni Kiongozi ambaye anataka utawala wa uwajibikaji…
MWENYEKITI: Ahsante.