Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

Hon. Maulid Said Abdallah Mtulia

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kinondoni

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria Pamoja na Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa kwa Kipindi cha Januari, 2016 hadi Januari, 2017

MHE. MAULID S. A. MTULIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu muumba mbingu na ardhi kwa kunijalia uzima. Lakini pili nikushukuru sana Mwenyekiti kwa kuamua kuwa mimi niwe mchangiaji wa kwanza. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe pongezi zangu za dhati kwa Kamati hasa hii Kamati ya Serikali za Mitaa kwa kueleza na kwa kutimiza wajibu wao wa kuishauri Serikali; kueleza mambo kwa kina sana, nawashukuru sana muwasilishaji na wanakamati kwa ujumla.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze na Kamati ya Katiba na Sheria. Katika Wizara yetu ya dada yangu pale anayeshughulikia ajira na walemavu; dada Jenista. Ukiangalia Kamati imejikita sana kwenye mambo ya kisheria, lakini mahali pengine kwenye taarifa hawajagusa chochote kwenye suala la vijana na walemavu. Ukiambatanisha vijana, walemavu na ajira maana yake hili ni kundi muhimu sana; vijana ni kundi muhimu ambalo linahitaji ajira na walemavu ni kundi muhimu ambalo linahitaji uwezeshaji. Lakini sijui kutokana na Kamati kuwa na mambo mengi bahati mbaya sana sikuona kwamba suala la ajira limepewa uzito.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini niseme, tuna tatizo kubwa sana la ajira na hasa kwa vijana. Mimi kama mwakilishi wa Jimbo la Mjini, Jimbo la Kinondoni linapambana sana na tatizo la vijana na hasa vijana kukosa ajira. Nilitegemea ama wakati mwingine Kamati itueleze Wizara yetu imefanya jambo gani katika ajira; katika kupitia utekelezaji wa Mpango wa Utekelezaji ndani ya mwaka mzima wa Kamati, ningefurahi sana kama Kamati ingetuonesha. Tuna tatizo kubwa sana la ajira, vijana wetu hawana ajira, Serikali lazima ijitahidi ihakikishe inatoa ajira kwa vijana.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini nikiliunganisha hilo la ajira na mikopo ya vijana, kwamba watendaji wetu wa Halmashauri na Serikali za Mitaa hawatoi umuhimu unaostahiki katika ile asilimia kumi ya mapato ya ndani ambayo inatakiwa iende kwa wanawake na vijana. Wakati mwingine wawakilishi tunagombana na watendaji kuonesha kwamba lazima tutenge hizi pesa, lakini wakati mwingine watendaji wanaona kwamba pesa ikibaki ndipo ipelekwe kwenye kundi lile la asilimia 10 ya wanawake na vijana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, niiombe na niishauri Serikali na nikubaliane na Kamati utengenezwe utaratibu au waraka maalum wa kuwasisitiza watendaji wote wa Halmashauri kwamba suala la asilimia kumi si hisani ni suala la sheria; kwamba Halmashauri zote zitenge asilimia kumi; kiwe ni kipaumbele na isiwe mpaka matatizo au bajeti inapoonekana inaruhusu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la TAMISEMI napenda kutoa ushauri kwa Serikali. Suala la TAMISEMI kuwa chini ya Ofisi ya Rais sisi wananchi bado halijatunufaisha na nadhani ni busara sasa kama Mheshimiwa Rais ataiona ni vizuri hii TAMISEMI ikarudishwa tena kwa Waziri Mkuu, ili Waziri Mkuu aweze kulisimamia. Kwa sababu kwa mtazamo wangu naamini Mheshimiwa Rais ana majukumu mengi sana na hili jambo linahusu Halmashauri na Manispaa zetu, hivyo Mheshimiwa Rais abaki katika kujikita kwenye kusimamia Serikali Kuu na Serikali za Mitaa zisimamiwe na Waziri Mkuu. Huu ni ushauri ambao naamini mtani wangu ataupokea. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini lingine, leo Makao Makuu yamehamia Dodoma, Dar es Salaam tunabaki kama jiji. Serikali ifike mahali sasa itambue kwamba ina wajibu wa kuyajenga majiji. Tuna Jiji la Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, na Mbeya. Haya ni majiji, ukiachilia mbali Tanga na mengineyo, ni majiji ambayo Serikali lazima ije na mpango wa kuhakikisha majiji haya yanakuwa ni majiji kweli yanafanana na majiji mengine na hasa ukizingatia kwa sisi watu wa Dar es Salaam baada ya Serikali kuhama yote tutabaki sisi kama sisi watu wa Jiji la Dar es Salaam na tunatakiwa tujengewe uwezo wa kutosha ili kuhakikisha Jiji letu la Dar es Salaam ambalo ndilo jiji kubwa kuliko majiji yote liwe ni jiji la mfano katika East Africa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala la utawala bora. Tuna tatizo la utawala bora. Kamati imesema vizuri sana na mimi naipongeza.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukianza kwenye uzinduzi wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi, Mheshimiwa Rais alisema magari yote ambayo sio ya mwendo kasi yanayopita katika njia ya mwendokasi yakikamatwa yang‟olewe matairi. Mheshimiwa Rais mtani wangu, mimi najua Kiswahili yeye hajui na mara nyingi anapenda kutumia Kiswahili kwa lugha ya picha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitegemea kwamba kwa kusema magari yang‟olewe matairi nilivyomfahamu mimi, kwa kuwa hajui Kiswahili, nilitegemea kwamba anaonesha ni tatizo gari zisipite na gari itakayopita ikamatwe ipelekwe kwenye vyombo vya sheria, ipewe hukumu kali kwa mujibu wa sheria. Si kwamba wang‟oe matairi kama walivyong‟oa. Kwa sababu hata akisema mtu anatumbua naamini huwa anatumia lugha ya picha, hatumbui kwa maana ya kutumbua, anamwajibisha mtu aliyefanya makosa kwa kutokufuata taratibu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa inakuaje leo vyombo vya dola, polisi wanashindwa kumfahamu Mheshimiwa Rais kwamba ana matatizo ya kutofahamu vizuri Kiswahili badala yake wanawakamata mapikipiki wanayang‟oa matairi kisha wanawapeleka mahakamani, sasa huyu mtu umeshang‟oa matairi umemuadhibu, unampeleka mahakamani kwenda kufanya nini? Jeshi la Polisi lazima lielewe lugha ya Mheshimiwa Rais.
Mheshimiwa Mwenyekiti, alipoambiwa kule njaa, aliwaambia mimi niwapikie, alikuwa na maana kwamba hii njaa ya Tanzania kila mtu atimize wajibu wake kuhakikisha anaepukana na njaa. Niwaombe watu wa Jeshi la Polisi wamwelewe sana mtani wangu huyu kwamba hakukusudia wang‟oe matairi ya watu na wale vijana waliong‟olewa matairi yao warudishiwe. Mahakama ndiyo yenye uwezo wa kumtia mtu hatiani, si Jeshi la Polisi wala si tamko la Mheshimiwa Rais ambalo watu hawakulielewa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi watu wa Kinondoni tuna tatizo na wakati mwingine ndiyo maana hatupendi sana Mheshimiwa Rais kuwa…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.