Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

Hon. Constantine John Kanyasu

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Geita Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hotuba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakati wa Kufungua Bunge la Kumi na Moja

MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Kwanza naomba kumshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa kunifikisha hapa lakini niwashukuru sana wapiga kura wangu kwa kunipa ridhaa hii ya kuwawakilisha. Niseme kwamba nitajitahidi kutimiza wajibu wangu kadri Mungu atakavyoniwezesha. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, siyo vibaya nikasema kidogo kuhusu tukio lililotokea hapa kwamba limenisikitisha. Kwanza kwa namna ambavyo niliamini baada ya wewe kutoa amri kwamba sasa watu hawa washughulikiwe na baadaye nikaona watu hawashughulikiwi wanabembelezwa, haikunifurahisha sana. Mimi nilitarajia askari wakiwa nje wangepanga mkakati wao wa namna ya kuwashughulikia na wanapokuja ndani wanakuja straight wamekwishajua wanawashughulikia namna gani. Matokeo yake wameanza kutukanwa hapo, vyombo vya dola vinatukanwa na vyombo vya habari vinachukua. Nataka niseme, matukio haya hayawezi kukoma katika mfumo wa Jeshi legelege namna hii. Mwenyekiti anapotoa amri wanaoingia ndani kutimiza amri wanapaswa waache mjadala na wahalifu. Ipo siku watu watakuja hapa wamekamia kufanya maovu na watakuja kuchukua hatua tayari wamekwishaua mtu hapa ndani. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, jana wakati mchangiaji mmoja anachangia aliwashambulia sana Wakuu wa Wilaya akasema yeye angetamani kuona Wakuu wa Wilaya wanafutwa. Pengine inawezekana yeye katika Jimbo lake haoni umuhimu wao kwa sababu anatazama zaidi vyeo vyao vile vya kisiasa na namna wanavyoshughulikia wahalifu lakini wananchi wa kawaida nafasi ya Mkuu wa Wilaya ni ya muhimu sana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nimekuwa Mkuu wa Wilaya, kwa siku nilikuwa naweza kumaliza migogoro mingi ambayo ingeenda yote Mahakamani, Mahakama ile isingeweza kufanya kazi. Tuna migogoro mingi ya ardhi, kuna watu wanaonewa huko hawawezi hata kufika polisi wakajieleza, hawawezi kwenda mahakamani wakajieleza hata kama haki ni ya kwake akifika mahakamani hawezi kujieleza, kwa Mkuu wa Wilaya wanaongea kwa uhuru na matatizo yao yanasikilizwa.
Kwa hiyo, mimi nasema wananchi waache kupokea hizi propaganda ambazo zinaweza zikawafanya wakashawishika kufikiri kwamba Mkuu wa Wilaya siyo mtu muhimu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tumefika hapa watu wanaongea hovyo kwa sababu mwanzo watu wametumia sana vyombo vya habari kupata publicity. Mimi naunga mkono TBC isirushe live na sababu za msingi ziko kwamba watu wametumia vibaya sana nafasi hii na matokeo yake badala ya kuzungumzia vitu vyenye manufaa kwa wananchi, wamekuwa wakiitukana Serikali na wananchi. Kwa hiyo, naomba kusema kwamba msimamo huo ulikuwa sahihi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba nizungumzie sasa kuhusu hotuba ya Mheshimiwa Rais. Mheshimiwa Rais ana vision ya kuona Tanzania inaelekea kwenye viwanda, mimi pia naunga mkono na nafikiri vision yake iko sahihi. Hata hivyo, yapi ni mahitaji muhimu ya kuwa na viwanda na viwe wapi. Tunachokitazama sasa hivi, ikitokea bahati mbaya likatokea tatizo, karibu 75% ya nchi itakuwa giza kwa sababu source ya umeme iko sehemu moja. Katika nchi hizi ambazo tunafikiri tunataka kuanzisha viwanda, kama viwanda vyote vitawekwa sehemu moja basi siyo ajabu siku moja Tanzania tukajikuta zaidi ya 30% ya watu walioko kwenye viwanda wamekosa kazi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu ni kwamba tuanze kwanza kwa kutambua maeneo yapi tunataka kuweka viwanda. Ningetamani kuona tunaanzisha miji ya viwanda. Kwa mfano, kama tutasema tunafanya Singida kuwa mji wa viwanda na likatambuliwa eneo kubwa kuwa la viwanda, basi eneo hilo lipelekewe kila aina ya miundombinu ambayo itasababisha wawekezaji waweze kufika. Hatuwezi kuweka viwanda Singida tukategemea umeme unaotoka Dar es Salaam, ipo siku njia hii ya umeme wa kutoka Dar es Salaam itapata matatizo na viwanda vyote vitasimama. Lazima tuwe na alternative route ya umeme kutoka sehemu nyingine.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu, pamoja na wingi wa gesi, tunavyo vyanzo vingine vya umeme. Pale Singida tuna upepo, hadithi hii imeongelewa kwa muda mrefu sana lakini kule Ngara tuna mto Ruvuvu, haukauki, una maji mengi sana. Tuna mradi wa umeme pale ambao Tanzania, Rwanda na Burundi wameamua kufanya kwa ubia, wamekadiria kutengeneza megawatts 70 peke yake lakini wataalamu walisema wangeweza kupata megawatts 300 kama wangewekeza vizuri. Mimi nafikiri ule mto kwa sababu ni source ya Mto Kagera na una maji mengi, badala ya Tanzania kulazimisha kutegemea mpaka kuingia ubia na nchi nyingine tungefikiria namna ya kupata umeme mwingi. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la viwanda inawezekana wawekezaji wakawa wanakuja lakini wanatukimbia kwa sababu hata waliopo wanalalamika uzalishaji gharama zake ni kubwa sana, tuna kodi nyingi na urasimu mwingi. Kama haya yote tutayarekebisha na tukapata maeneo ambayo ni industrial na yakawekewa kipaumbele cha kuwekewa kila aina ya miundombinu, vision ya Mheshimiwa Rais ya kuweka viwanda inaweza ikatimia. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika eneo langu ninalotoka tunachimba madini. Limekuwepo tatizo kubwa sana la wawekezaji wakubwa kuchukua maeneo yote mpaka ambayo walikuwa wanachimba wachimbaji wadogo wadogo. Ni kweli, tunaunga mkono wawekezaji wakubwa wapewe maeneo lakini kama Serikali itaendelea kupata pesa wananchi wanaendelea kuwa maskini tutaendelea kuona uchumi unakuwa kwenye Serikali lakini wananchi wanaendelea kuwa maskini kwa sababu hawana sehemu ya kuchimba. Kila wanapogundua madini anakuja mjanja anawahi Dar es Salaam analipia PL watu wanafukuzwa. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, pale kwangu Geita Mjini, Mgodi wa Geita umepewa kilometa za mraba 192 lakini hata katika maeneo ambayo walikuwa wanachimba wananchi kabla hawajapewa walifukuzwa wakapewa wao. Matokeo yake mji ule umedumaa na hauwezi kukua tena kwa sababu kazi ya asili ya watu wa pale ni kuchimba dhahabu. Naomba Serikali, wakati tunafikiria namna ya kuyafanya madini haya yawe na maana zaidi katika uchumi wa kwetu lazima tufikirie namna ya kuwafanya Watanzania waweze kupata maeneo ya kuchimba.
Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Rais alizungumzia suala la namna ambavyo Tanzania haifaidiki na mifugo na madini. Wakati miji hii ikiwa midogo wananchi wenye mifugo walikuwa wanaishi karibu na miji hii. Kadri miji inavyopanuka maeneo ya kuchungia mifugo yanazidi kupimwa na kujengwa nyumba, Serikali haijawahi kutenga eneo kwa ajili ya wafugaji ambao inawaondoa. Matokeo yake maeneo yote haya ambayo tunapima watu wanahamia ambayo zamani yalikuwa machungio ya mifugo sasa hivi kuna nyumba, sehemu zenye majosho kuna nyumba, hivi tunatarajia mifugo hii iende wapi? Hata kama tunasema mifugo hii ipunguzwe, huyo anayekuja kuweka kiwanda hapa Tanzania atapata wapi mifugo ya kulisha kiwanda chake? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nafikiri Serikali haijatimiza wajibu wake hapa. Tunayo mapori mengi ambayo hayana faida kwa nchi hii. Tukimuomba hapa Waziri wa Maliasili atuletee taarifa ya Pori la Biharamulo limeingiza shilingi ngapi, inawezekana tukachukua wazo la Mheshimiwa Waziri wa Mifugo la wafugaji kulipia wakawa na faida kuliko…
(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)
MWENYEKITI: Ahsante.
MHE. CONSTANTINE J. KANYASU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. (Makofi)