Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Juliana Daniel Shonza

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. JULIANA D. SHONZA: Mheshimiwa Naibu Spika, awali ya yote na mimi nishukuru kwa kuweza kupata nafasi hii. Vilevile nichukue nafasi hii kuweza kuzungumzia hii hali ambayo inaendelea humu Bungeni.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda nianze kwanza kwa kukutoa hofu kwa sababu kwa sisi ambao tunasoma Biblia, ukifuatilia kitabu kile cha Mathayo utakuta kuna historia ya Mfalme Herode, tabia ya Mfalme Herode inafanana kabisa na tabia wanayoifanya viongozi wa CHADEMA ndani ya Bunge lako Tukufu. Mfalme Herode alikuwa na tabia ya wivu. Kilichomsababisha Mfalme Herode akatangaza kwamba watoto wote wa kiume wauwawe ni wivu aliokuwa nao kwa sababu alipoiona ile nyota ya mashariki akaona kabisa kwamba nyota hii ni ishara Mfalme anakwenda kuzaliwa kwa hiyo ataenda kuchukua nafasi yake. Naomba nikutoe hofu kwamba nyota yako ndani ya Bunge hili imeng‟ara sana na ndiyo inayowatisha Wapinzani kiasi kwamba wanabaki wanahangaikahangaika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini tukumbuke na nichukue nafasi hii kuweza kuwakumbusha Wapinzani kwamba pamoja na mbinu zote ambazo Herode alizifanya kumuangamiza Yesu mpaka leo hii Yesu ndiyo Mfalme wa dunia, ukitaja Wafalme wa Dunia wako wawili, ni Yesu pamoja na Mtume Muhammad, hakuna cha Herode wala cha nini. Kwa hiyo, watoke ndani ya Bunge au wasitoke bado Naibu Spika utabaki kuwa Naibu Spika na Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tunakutakia kila la kheri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa historia inaonesha kwamba Herode alianza kufa kabla ya Yesu pamoja na mbinu zake zote, kwa hiyo ni wazi kwamba sasa hivi CHADEMA kinaenda kufa na kinaenda kutoka miongoni mwa vyama Tanzania kwa sababu mambo wanayoyafanya katika Bunge hili siyo mambo waliyotumwa na wananchi wa Majimbo yao. Kwa hiyo, naomba nikutoe hofu, wewe ni kiongozi makini na sisi Wabunge wa Chama cha Mapinduzi tuko pamoja na wewe kama ambavyo jina lako ni Dkt. Tulia tunaokuomba utulie. (Makofi/Kicheko)
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naomba moja kwa moja nianze kwa kuunga mkono hoja ya bajeti ya Wizara ya Fedha. Nichukue nafasi hii kuipongeza Kamati ya Bunge ya Bajeti kwa sababu imefanya kazi kubwa sana. Niiombe Serikali iweze kuzingatia maoni ya Kamati ya Bajeti chini ya Mwenyekiti wake Mheshimiwa Hawa Ghasia kwa sababu maoni waliyoyatoa ni mazuri na yakifanyiwa kazi yataleta tija na kuongeza mwamko katika Serikali hii ya Hapa Kazi Tu.
Mheshimiwa Naibu Spika, nianze kuchangia moja kwa moja Wizara ya Afya ambayo imetengewa kiasi cha fedha cha shilingi trilioni 1.99, vipaumbele vyake vikiwa ni kununua dawa, vifaa tiba pamoja na kulipia deni la MSD. Tunatambua kwamba ni jambo zuri kulipa deni la MSD na najua zahanati zangu kule Mkoani Songwe sasa zitaenda kuwa na uhakika wa dawa.
Mheshimiwa Naibu Spika, sote tunatambua kwamba zahanati zetu nchini zina hali mbaya hususani zahanati ambazo zipo katika Mkoa wangu wa Songwe. Zahanati zangu zina hali mbaya sana na Sera ya Wizara ya Afya inasema kwamba kutakuwa na zahanati kwa kila kijiji na kutakuwa na kituo cha afya kwa kila kata lakini mpaka leo hii ambapo tumesimama kujadili bajeti hii ni wazi kwamba hatujafikia hata nusu ya malengo ambayo tulikuwa tumejiwekea. Mfano, nikienda katika Mkoa wangu wa Songwe katika Wilaya ya Ileje ina zahanati 23 tu zote zinakabiliwa na tatizo la uhaba wa maji, wanatumia maji ambayo siyo safi na salama, matatizo ya umeme pamoja na ukosefu wa watumishi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika Tarafa ya Bulambya katika Zahanati ya Chabu pamoja na Izuba, zinatumia maji machafu yanayotoka katika Mto Songwe na ukiangalia maji yale yalishapimwa yakaonekana kwamba yana vijidudu asilimia 18, kwa hiyo hayafai kwa matumzi ya binadamu. Kama hiyo haitoshi, nikienda katika Wilaya yangu ya Mbozi ina zahanati 99, zahanati ambazo zinafanya kazi mpaka sasa hivi ni 62 tu na zote matatizo yake yanafanana. Hakuna umeme, maji, wahudumu na waganga wa kutosha.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, katika zahanati ambayo ipo katika kijiji cha Wasa mpaka leo hii ina Mganga mmoja tu. Ukienda katika Zahanati ya Ipunga ina Mganga mmoja tu kiasi kwamba siku Mganga akipata shida zahanati zile zinafungwa. Unaweza kuona kwamba tunaweka rehani maisha ya mama mjamzito na watoto. Kwa hali hii, inaashiria kwamba bado afya ya mama mjamzito na mtoto iko hatarini.
Mheshimiwa Naibu Spika, kama hiyo haitoshi, katika Wilaya ya Mbozi kuna Kata ya Itaka, kuna mfadhili alishatoa vifaa vya maabara vikiwepo vifaa vya kupimia CD4 lakini kwa sababu mpaka leo hii hakuna umeme, vile vifaa vimebaki kama mapambo. Ndiyo maana sisi kama Wabunge wanawake tunahitaji commitment ya moja kwa moja ya Serikali yetu katika kuzihudumia zahanati zetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile ukienda Wilaya ya Momba mpaka sasa hivi ina zahanati 27 tu na vituo vya afya vitatu. Hili jambo nimekuwa nikilipigia kelele katika Bunge hili kwamba Wilaya ya Momba hata Hospitali ya Wilaya hakuna, hivyo vituo ambavyo viko 27 bado havitoshi na ukizingatia havina mahitaji muhimu.
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba commitment ya Serikali katika kuhakikisha kwamba inaweka mkono wake na siyo kuziachia tu Halmashauri zetu. Tunataka commitment ya moja kwa moja ya Serikali katika kuzihudumia zahanati zetu. Sote tunatambua vifo vya akina mama na watoto vinatokea kule chini katika zahanati lakini siyo katika Hospitali za Mikoa au Wilaya. Hivyo, kama tumejipanga kuhakikisha kwamba tunakomesha vifo vya watoto na akina mama, niishauri Serikali isiziangalie tu Hospitali za Wilaya na Mikoa, tutupie jicho chini katika zahanati zetu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimesoma kwa umakini sana bajeti ya Serikali Kuu. Bajeti hiyo haijatenga bajeti ya moja kwa moja kuzihudumia zahanati zetu. Ndiyo maana ukisoma kuna kiwango cha fedha ambacho kimetengwa katika bajeti ya TAMISEMI shilingi bilioni 32, hizo ni fedha ambazo zinatoka katika own source kwa maana ni fedha ambazo zimetengwa na Halmashauri zetu na fedha hizi siyo za uhakika, kwa sababu ni fedha ambazo inategemeana na makusanyo ambayo Halmashauri zetu zitakuwa zimekusanya. Nimesoma hiyo bajeti ya TAMISEMI kuna Kituo cha Afya cha Tunduma ambapo kuna ukarabati ya wodi ya wazazi, kujenga sehemu ya kujisubirishia akina mama wajawazito pamoja na jengo la upasuaji na chumba cha kujifungulia katika Zahanati ya Katete na Chiwezi, zote zimetengewa kiasi cha shilingi milioni 128 lakini ukiangalia source ni kwenye local governments, UNICEF na vyanzo vya ndani.
Mheshimiwa Naibu Spika, vyanzo hivi siyo vyanzo vya kuaminika. Ndiyo maana sisi kama Wabunge wanawake tunaotoka katika mikoa ambayo ina shida ya huduma za kiafya, tunaomba commitment ya Serikali kwamba sasa iweze kuzingatia ushauri ambao umetolewa na Kamati ya Bajeti. Ushauri ule ni mzuri kwamba iongezwe Sh.50 kwenye kila lita ya mafuta ya petrol na diesel ili kwa mwaka tuweze kukusanya shilingi bilioni 250 ambapo shilingi bilioni 220 zikatumike katika kuhakikisha kwamba tunasambaza maji katika mikoa yetu na shilingi bilioni 30 zipelekwe kumalizia zahanati zetu na kuzifanyia ukarabati.
Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hayo, naunga mkono hoja.