Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Deo Kasenyenda Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makambako

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. DEO K. SANGA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikushukuru kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia. Wanasema ukiona watu wanasema wewe una tatizo, wewe songa mbele, wewe ni jembe unafaa kutumikia wananchi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nampongeza sana Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutuletea bajeti nzuri yenye mwelekeo na kwa kumteua Waziri Mpango pamoja na Naibu Waziri. Naipongeza Wizara ya Fedha na Watendaji wote kwa kutupa bajeti yenye mwelekeo mzuri kwa maendeleo ya Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa mategemeo yetu Watanzania ni kwamba matatizo ya maji, elimu, afya, barabara, umeme yatapungua. Hii ikiwa ni pamoja na utekelezaji wa ahadi alizozitoa Mheshimiwa Rais kwa Watanzania ikiwemo Mji wa Makambako ambapo aliahidi maji, vifaa tiba, lami kilomita sita, umeme na kadhalika. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, imani yangu bajeti hii hata waliotoka humu ndani nao wanahitaji maendeleo kwenye Majimbo yao. Rais wetu alishasema maendeleo hayana chama, peleka maendeleo hata huko katika Majimbo waliyotoka utakuwa unawatendea haki Watanzania. Ingawa wenzangu watasema, aah, aah, ndugu zangu tunawapelekea maendeleo Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nizungumzie suala hili ambalo limeleta mkanganyiko mkubwa juu ya mageti ambayo yalishatangazwa kwamba yanaondolewa kwenye Halmashauri zetu yanayohusiana na ushuru. Waziri atakapokuwa anahitimisha hapa atuambie jambo hili limekaaje maana tayari linaleta mkanganyiko kuhusiana na kuondoa mageti haya ya ushuru wakati Halmashauri zilishaweka bajeti na wananchi wameshapata kauli ya kwamba ushuru sasa umeondolewa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nimpongeze Waziri kwa kuondoa tozo mbalimbali kwa wakulima. Jambo hili limeleta faraja kubwa sana kwa Watanzania na wakulima wetu. Nirudie tena kumpongeza Rais John Pombe Magufuli kwa kumteua Waziri huyu Mheshimiwa Dkt. Mpango sasa tunaona mipango itakwenda vizuri, nakupongeza sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, napingana na hawa watu ambao wametoka hapa na wamekuwa wakipinga kwamba hii bajeti haina mwelekeo na kadhalika, ndugu zangu uchaguzi ulishakwisha, Rais sasa ni Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Makamu wa Rais Mheshimiwa Samia Suluhu, Waziri Mkuu ni Mheshimiwa Majaliwa Majaliwa pamoja na Mawaziri wote walioteuliwa, naomba chapeni kazi ya maendeleo kwani watu wanasubiri maendeleo katika maeneo yao. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, wenzangu wengi wamezungumzia sana suala la kiinua mgongo. Mimi niseme tu kwamba suala la kiinua mgongo linagusa Watanzania wote hasa watumishi. Watumishi pamoja na Waheshimiwa Wabunge tumekuwa tukikatwa kodi mbalimbali lakini kodi hii ya kiinua mgongo kwa watumishi nadhani iangaliwe upya. Kwa sababu watumishi hawa wametumikia nchi na wamekatwa kodi mbalimbali. Kwa hiyo, naomba suala la kiinua mgongo kwa watumishi wote kwa ujumla liangaliwe vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niipongeze Serikali imesikia kilio cha Wabunge ambao wamezungumzia sana suala la manunuzi kwamba lilikuwa ni tatizo kubwa katika Halmashauri zetu na wenzangu wengi wamesema hapa. Suala hili la manunuzi ilikuwa hela zikipelekwa kwenye Halmashauri zinaliwa tu na baadhi ya watendaji ambao siyo waaminifu. Naishukuru sana Serikali, Waziri alisema hapa unaletwa Muswada wa kubadilisha Sheria ya Manunuzi na mimi naafiki kwamba utaratibu huu ukibadilishwa utaleta tija na maendeleo katika Halmashauri zetu na hizi fedha zote zinazojadiliwa hapa sasa zitakwenda kutumika ipasavyo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mji wetu wa Makambako sasa tunazungumzia suala la kujenga viwanda, watu wanahitaji kuwekeza viwanda katika mji wetu lakini tatizo kubwa ni upatikanaji wa maji. Niipongeze sana Wizara ya Maji ambayo tayari imetenga fedha kwa ajili ya kutatua tatizo la maji katika Mji wa Makambako. Kwa hiyo, tunaomba Wizara ya Fedha ipeleke haraka fedha hizi ili ziweze kuleta maji ili wawekezaji waweze kuanzisha viwanda katika Mji wetu wa Makambako. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo la mwisho, hili nimelisema mara nyingi sana, naomba nirudie, Serikali imewekeza fedha kwenye hospitali yetu pale kwa miaka zaidi ya minne sasa, tumejenga wodi mbili kubwa za akina mama na watoto imebaki tu kumalizia, miaka minne imebaki magofu. Mheshimiwa Waziri wa Fedha hebu liangalie suala hili zinahitajika hela kidogo sana ili wodi hizi ziweze kufanya kazi iliyokusudiwa kwani fedha ya Serikali imekaa pale kwa muda mrefu. Namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anahitimisha aone ni namna gani atatatua tatizo hili la kumalizia wodi hizi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ni kwamba hospitali ile ya Mji wa Makambako imeshapandishwa hadhi na kuwa hospitali kamili na kwa miaka mitatu tunakwenda vizuri. Tatizo ambalo lipo katika Mji wetu wa Makambako, nilimueleza hata Waziri wa Afya na Waziri wa TAMISEMI, tayari tuna jengo pale la upasuaji ambalo limeshakamilika lakini tunakosa tu vifaa tiba vya upasuaji. Tuna gari letu la ambulance kwa siku mara saba linapelekea wagonjwa Njombe kwa ajili ya upasuaji. Fedha inayohitajika ni kidogo sana hata shilingi milioni 30 hazifiki ili tuweze kununua vifaa vya upasuaji vilivyobakia ili shughuli za upasuaji ziweze kuendelea. Mmetuletea Madaktari wazuri wako pale wamekaa tu hawawezi kufanya kazi kwa sababu shughuli za upasuaji hakuna. Namuomba Waziri wa Fedha atakapokuwa anahitimisha aone namna ya kutatua tatizo la kununua vifaa vya upasuaji ili kuweza kutatua tatizo la Makambako. Vifaa vinavyohitajika ni kifaa cha kuchanganyia dawa ya usingizi na vitu vidogo vidogo tu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, mambo yote naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu, Waziri Dkt. Mpango chapa kazi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja hii kwa asilimia 100. Ahsante sana.