Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2015, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017 na Mapendekezo ya Serikali kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. Kwanza kabisa nianze kwa kukupa pongezi wewe mwenyewe kwa kazi nzuri unayoifanya. Tunamuomba Mwenyezi Mungu akujalie afya njema uendelee hivyo hivyo, kazi yako iko safi, tunaona juhudi zako, Mungu akubariki sana.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile nitoe pongezi kwa Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa hotuba yake nzuri aliyeitoa. Nimpongeze kwa bajeti nzuri ambayo kwa kweli ni ya kihistoria na utekelezaji wa bajeti hii kama kweli itatekelezeka kwa asilimia zaidi ya 80 Tanzania itakuwa imeweza kwenda mbele zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaipongeza bajeti hii kwa kuangalia umuhimu wa maendeleo. Kwa kweli katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi katika uchaguzi uliopita mwaka jana 2015 tuliahidi mambo mengi sana. Jambo kubwa tuliloahidi ilikuwa ni kuondoa umaskini na kuondoa umaskini ni lazima tujikite kwenye kilimo na kwenye shughuli mbalimbali ambazo zitaweza kuondoa umaskini wa wananchi wetu. Tukiangalia hata katika bajeti hii inaonesha asilimia 40 inakwenda kwenye matumizi ya maendeleo.
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile tunatoa pongezi kwa sababu maendeleo bila elimu na yenyewe ni tatizo. Tumeona katika bajeti hii asilimia 22.1 imekwenda kwenye maendeleo ya elimu, tunawapongeza kwa hilo.
Mheshimiwa Naibu Spika, tukumbuke kwamba katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliwaahidi akina mama kwamba watakapochagua Serikali ya Chama cha Mapinduzi basi mama hatapata mzigo wa kutafuta maji kwenye vyanzo mbalimbali vya mito na visima na kwamba tunakwenda kukomesha tatizo la akina mama kujihimu asubuhi kwenda kutafuta maji. Katika bajeti hii tunaona imetengwa asilimia 4.8 kwa ajili ya maendeleo ya maji. Tunaomba juhudi zifanyike, utekelezaji uwe wa asilimia 100. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tuliwaahidi akina mama na watoto kwamba kwa kuchagua CCM mwaka 2015 huduma za afya zitaboreshwa. Tukiangalia katika bajeti iliyopo asilimia 9.5 imetengwa kwa ajili ya maendeleo ya afya. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunawaombea na kwa kushirikiana na Watanzania wote tufanye kazi kwa juhudi ili yale malengo yaliyopangwa yaweze kutimia. Vilevile tuweze kuwaondolea kero wananchi na kutimiza ahadi ya Chama cha Mapinduzi ilizowaahidi wananchi katika Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2015. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika haya nina changamoto ninazoziona na naweza nikachangia zaidi. Tukienda kwenye suala la kodi ya majengo, Umoja wa Madiwani na Mameya wa Miji wamekaa na kutoa tamko kwamba hawakubaliani na maamuzi au mapendekezo aliyoyatoa Mheshimiwa Waziri katika bajeti hii. Wanayapinga kwa sababu wanasema kwamba Mkoa wa Dar es Salaam ulianza kama piloting katika ukusanyaji wa kodi ya majengo kwa maana ya Kinondoni,Temeke pamoja na Ilala, kwa Wilaya zote tatu za Mkoa wa Dar es Salaam lakini matokeo hayakuwa mazuri, ukusanyaji wa kodi za majengo haukuwa mzuri, wanakuja na maoni ya kusema kwamba mapendekezo haya yabadilishwe. Mimi nina maoni kwamba, kama tunaamua kwenda huko, nia ni njema tunataka tukusanye kodi za majengo lakini kama piloting results zake hazikuwa nzuri mmeona nini ambacho kitakwenda kurekebishwa ili TRA iweze kukusanya kodi za majengo? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kama kuna changamoto zilionekana Dar es Salaam, je, tutazi-tackle vipi kuanzia tarehe 1Julai, 2016? Nasema hivi kwa sababu tunaweza tukaamua TRA kukusanya kodi ya majengo na ukitazama Halmashauri nyingi zinategemea kodi ya majengo kuanzia asilimia 30 mpaka asilimia 60 leo tunawaondolea, je, sisi tumejidhatiti kwa namna gani? Je, tutapeleka pesa zinapohitajika?
Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile wanalalamika kwamba wana changamoto za mikopo katika Halmashauri zao na wamekwishaingia mikataba na mabenki. Je, TRA ikikusanya hizi Halmashauri zitalipiwa madeni katika mabenki kupitia huu mfumo wa kupitia Hazina? Nafikiri Waziri aje atueleze na awape amani Mameya ambao wamekusanyika na wengine wamekuja hapa jana toka Dar es Salaam, wamegawa tamko lao kwa Wabunge wanalalamika kwamba uamuzi huu unakwenda kuwaondolea uwezo na hivyo Halmashauri zitakufa na njaa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ni kuhusu kodi za mazao. Tunashukuru wameondoa kodi hasa kwenye mazao ya mbegu ambazo zinazalisha mafuta na kuweka kodi kwenye crude oil kwa maana ya mafuta yanayotoka nje kwa ajili ya mafuta ya kula. Tanzania tunatumia zaidi ya tani laki nne kwa mwaka na mafuta tunayo-import yanatokana na palm. Leo tumeyawekea kodi, nakubali nia ni nzuri lakini tumejipanga vipi kuzuia bei ya mafuta kupanda? Kwa sababu kama tumeweka kodi lazima bei ya mafuta itapanda na kama ikipanda hata chipsi mtaani itapanda bei kwa sababu mafuta ya alizeti kidogo gharama yake ni kubwa. Nafikiri kidogo tungeweza kwenda taratibu, tusiende pupa kwa sababu tutatengeneza bei kubwa ya mafuta ya kula na tutajikuta tunashindwa. Nia ni njema tunakubaliana na ninyi lakini tuangalie ni namna gani ya kuweka unafuu kusudi tupate mafuta kwa bei ya chini. Chakula kinacholika mtaani mama lishe wanapika kwa kutumia mafuta ya palm oil, japokuwa kweli yana matatizo kwa sababu yana cholesterol lakini tuangalie ni jinsi gani ya kuingia katika kuboresha uzalishaji wa mafuta ya ndani ambayo yatakidhi mahitaji ya mafuta tunayotoa nje. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nilishatoa ushauri kwamba kuna zao la pamba, watu wa Mkoa wa Simiyu wanalima pamba, bei ya pamba inakwenda kuporomoka. Inaporomoka kwa sababu hakuna mikakati ambayo inaonesha kwamba Serikali iko serious kumuokoa mkulima wa pamba. Bei ya pamba inaelekea kudorora na percent kubwa ya pamba tunayolima tunapeleka nje, je, tunajiandaa vipi kuwa na viwanda vyetu vya ndani ambavyo vitafanya mkulima wetu alime kwa uhakika wa soko, alime bila kuogopa bei? Sasa hivi kuna directive price inatolewa ambayo inamkandamiza mkulima. Sasa hivi mkulima anayelima pamba anabadili kilimo cha pamba anakwenda kwenye alizeti kwa sababu kilimo cha pamba hakilipi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba ianzishwe Wizara ya textile kama inawezekana tuamue ku-specialize ku-produce nguo tuuze katika soko la East Africa ambalo lina population ya watu zaidi ya milioni 100 sasa hivi kwa sababu nguo zina demand kubwa. Mtoto akizaliwa leo anatumia nguo, unapoishi unakuwa unatumia nguo, unapofariki unafunikwa na nguo, matumizi ya ngua yako juu, lakini tunalima pamba tuna export, kwa nini tusiwe na viwanda vilivyojitosheleza kwa maana ya kuzalisha nguo na tukauza katika soko letu la East Africa? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, tumeweka kodi kwenye mitumba kwa sababu tunadhani tunaweza tuka-produce nguo. Nachosema tuna-promote soko la China, watatuletea nguo hapa mpya, nguo za mitumba tutaziwekea kodi lakini sisi wenyewe hatuzalishi nguo. Tunaomba Mheshimiwa Waziri mlitazame suala hili kwa upana wake. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii, napenda kuunga mkono hoja. Ahsante sana.