Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, asante sana. Nianze moja kwa moja, sitaki nipongeze, niende Ukurasa wa 78 wa Kitabu cha Mheshimiwa Waziri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru sana kwa sababu, ametenga asilimia 94 kwa ajili ya maendeleo, lakini hasa kwenye Sekta ya Nishati. Namshukuru sana Mheshimiwa Waziri, lakini ili tuipate hiyo trilioni moja nashukuru kwa sababu, bahati nzuri nyuma yangu hapa kuna Waziri Mkuu na ningemwomba Mheshimiwa Waziri Mkuu anisikilize vizuri, naomba mumshtue hapo! Hili Jimbo la Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, Mheshimiwa Shabiby, hili Jimbo la Ruangwa kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, eneo lote lile lipate umeme, lakini na maeneo mengine ya Watanzania.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge tuliomo humu ndani tunaiomba sana Serikali hii, asilimia 94 ambayo ni sawa sawa na trilioni moja; Mheshimiwa Waziri wa Fedha tumekuwa tukisema mara nyingi sana humu ndani kwamba, pesa hizi zitoke, lakini bahati nzuri au mbaya pesa hizi hazitoki! Hata zile fedha ambazo tumeziwekea uzio na zenyewe mnazipeleka sehemu nyingine, lakini ili nchi hii iendelee na ili iwe ya viwanda lazima tuwe na umeme wa kutosha. Tutaimba nyimbo hapa, lakini kama hatuna umeme wa kutosha, umeme wenye uhakika, hatuwezi tukafikia yale malengo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana hapa, Serikali kupitia Waziri Mkuu, mtakapokaa kwenye vikao vyenu huko hii trilioni moja iliyoombwa na Wizara ya Nishati na Madini itoke ili kusudi huyu Waziri wa Viwanda anapozungumzia viwanda, lazima apate umeme. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini tukipata umeme wenye uhakika REA wakasambaza umeme vijijini wale vijana wanaokuja mjini hawatakuja mjini tena kwa sababu kuna umeme vijijini. Naomba sana Serikali zile pesa ambazo tulikuwa tumetenga kwa ajili ya umeme Tanzania, tozo, pamoja na zile ambazo zilibaki mwaka jana, lazima wapelekewe wenzetu wa TANESCO ili kusudi waweze kufanya kazi yao vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la pili na hili nimekuwa nikilisema mara kwa mara, Serikali imeshindwa kulipa TANESCO madeni yake, sijui tatizo ni nini! Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri wa Nishati, hii si Serikali kwa Serikali, hivi hawawezi kukaa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha wakaondoa hili deni ili kusudi vitabu vya TANESCO viwe visafi! Maana kila siku tunakuta madeni, madeni, madeni! Hebu wakae chini hili tatizo walimalize.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie bomba la gesi; huu ni ushauri kwa Mheshimiwa Waziri wa Nishati. Bomba hili lina gharama kubwa, linatakiwa liwe na ulinzi wa kutosha na wasiweke pale Waswahili, waweke Jeshi la Ulinzi liende lisimamie ulinzi wa bomba lile kwa sababu, gharama yake ni kubwa.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la tatu, mitambo ya kusindika gesi, LNG; bado hatujachelewa, tuongeze speed kwa sababu, huwezi ukazungumzia trillion cubic meters za gesi tuliyonayo, wamesema 57 trillion, halafu huna mtambo wa kusindika hiyo gesi! Lazima tuwe na mtambo wa kusindika hiyo gesi, vinginevyo tutabaki hapa, hata manufaa yatakuwa hayapo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Bomba la mafuta la kutoka Uganda kuja Tanzania, Tanga. Nimshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kuchangamkia, sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, hii ndiyo fursa yenyewe, tusiiachie hata kidogo, lakini lazima kuwe na ulinzi wa kutosha katika usimamizi wa ujenzi wa bomba hili la mafuta kutoka Uganda kuja Tanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, REA. Niwapongeze sana REA kwa kazi nzuri sana wanayofanya na niwaombe Waheshimiwa Wabunge, kwa umoja wetu, kwa kazi nzuri sana aliyofanya REA, hata kama huwapendi kwa sura zao, basi wapende kwa matendo yao, wamefanya kazi nzuri mno. Cha msingi hapa, sisi kama Wabunge, ni kuibana Serikali, ili itoe pesa za kutosha ili miradi iliyobaki ya REA II na REA III tunayokwenda kuanza, iweze kukamilika ndani ya muda unaotakiwa. Lazima tuibane Serikali humu ndani na tuishauri Serikali kwamba, kwa sababu, tunakwenda kwenye REA III tuibane Serikali ili kusudi iweze kutoa pesa za kutosha.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo dogo upande wa REA, lakini ni vizuri wakarudi nyuma ili wajifunze kwamba, tulifanikiwa REA I, kulikuwa na matatizo gani? Changamoto zilizopo, tumekwenda kwenye REA II changamoto ni zipi tulizoziona? Sasa tunakwenda kwenye REA III zipo changamoto nyingi, hasa urukaji wa vijiji na vitongoji; wanaweka umeme hapa, wanaruka, wanakwenda wanaruka, wanaruka, wanaruka!
Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vizuri kwa sababu, wanapita kuangalia ni wapi wameweka umeme, ni vizuri kama ni kijiji kimoja basi kijiji chote kiweze kupata umeme. Si vizuri sana wanaweka umeme kwenye nyumba, wanaruka wanakwenda kuweka kwenye nyumba hii, wanaruka! Si vizuri sana, tungependa sana umeme kwenye kijiji X umeme uwepo. Kwenye maeneo ya Jimbo langu, nilishawasilisha kwa Ndugu Msofe maombi, sitaki niseme hapa, lakini nimwombe sana, maeneo ambayo yamerukwa, vijiji ambavyo vimerukwa, naomba katika awamu ya III umeme uweze kupatikana. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho. Naomba kusisitiza tena, najua Waziri wa Fedha hayupo, lakini najua Waziri wa Nishati yupo na Waziri Mkuu ananisikiliza. Pesa tunazokubaliana humu kwamba, pesa hizi zinatakiwa zitumike kwa kazi fulani, naomba zitumike kwa kazi hiyo hiyo, zisitumike kwa kazi nyingine na haya ni makubaliano ya Bunge. Nasisitiza tena, tukikubaliana kwamba, pesa hizi zinakwenda kwa ajili ya umeme, kama ni tozo za mafuta ziende zikasaidie kule, kusaidia wananchi wetu ili waweze kupata umeme wenye uhakika, basi ziende.
Mheshimiwa Mwenyekiti, bila umeme wenye uhakika hakuna maendeleo, bila umeme wa uhakika hakuna viwanda. Mheshimiwa Mwijage, ni vizuri wakakaa kwa sababu huko mbele bila umeme wa uhakika, viwanda tunavyozungumza Dar-es-Salaam au maeneo mengine vijijini, havitapatikana! Ni lazima tupate umeme wa uhakika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.