Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Suleiman Ahmed Saddiq

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mvomero

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi. Awali ya yote naomba kutoa pongezi zangu za dhati kabisa kwa Mheshimiwa Rais kwa kumteua Profesa Muhongo kuwa Waziri wa Nishati na Madini; naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri maneno ambayo yanazungumzwa aachane nayo, akaze buti tusonge mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, kazi yake ambayo amefanya tumeiona, tuna matumaini makubwa na yeye. Labda niseme neno dogo katika eneo hili, niwaombe watendaji wanaomsaidia Mheshimiwa Waziri waoneshe mshikamano na upendo mkubwa kwa Waziri, wafanye kazi kama Waziri anavyofanya ili eneo hili sasa lisonge mbele. Wapo watendaji katika eneo hili inaonekana hawana speed ya Waziri mwenyewe. Niwaombe watendaji wa Wizara husika msaidieni Waziri, sisi Wabunge tuna imani naye, tusonge mbele, tulete maendeleo katika nchi yetu. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na suala la umeme hususani umeme wa REA, vijijini. Naomba nimshukuru sana Mheshimiwa Waziri anaendelea kunipa ushirikiano wa kutosha katika yale maeneo ambayo huwa naonana naye na kuwasiliana naye.
Mheshimiwa Mwenyekiti, upungufu ambao unajitokeza katika mpango wa REA wa Awamu ya Pili. REA Wilaya ya Mvomero ipo kwenye tarafa zote nne. Na katika tarafa zote nne hizi kuna baadhi ya vijiji mradi ule unaendelea na baadhi ya vijiji mradi bado. Tumewasiliana mara nyingi na Msaidizi wa Waziri, tumewasiliana na Msofe wa REA, lakini bado yapo matatizo ya hapa na pale. Naomba Mheshimiwa Waziri aelewe kwamba, lile eneo la Kata ya Mtibwa, Wilaya ya Mvomero, katika Vijiji vya Kiduduwe, Kisara na Kunke, yule mkandarasi ambaye yuko pale leo ni miezi mitatu hajawalipa mafundi ambao wanafanya kazi ya kusambaza umeme.
Mheshimiwa Mwenyekiti, mafundi wale wapo zaidi ya 20 wanahangaika hawajalipwa na baadhi ya maeneo nguzo wameanza kuziondoa ambazo mwanzo walisambaza. Suala hili nilishamweleza Mheshimiwa Waziri , naomba hatua sasa zichukuliwe, lakini kuna maeneo ambayo umeme huu unasambazwa, ni maeneo ya barabarani peke yake, hakuna umeme unaokwenda vijiji vya ndani, umeme unalenga barabara kuu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, Kata ya Langali kuna vijiji vitatu, umeme ubaki kijiji kimoja kitongoji kimoja; tunaomba Mheshimiwa Waziri atoe tamko, gharama ya kupeleka umeme Mgeta ni kubwa. Inakuwaje leo umeme unakwenda kijiji kimoja wakati mamilioni ya fedha yametumika? Mheshimiwa Waziri tunaomba atusaidie hilo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini katika eneo la Kibati, Kijiji cha Ng‟ai waliweka nguzo, wameziondoa, wanasema nguzo ni chache, sasa hivi wanaendelea kutafuta nguzo. Naomba Mheshimiwa Waziri atusaidie, ili ile azma yake na azma ya Serikali itimie.
Mheshimiwa Mwenyekiti, shida moja mbayo ipo, Mheshimiwa Waziri, wale ambao walipewa mkataba na REA na wao wame-subcontract kwa mafundi wengine na kampuni nyingine na wale ma-subcontractor na wao inaonekana uwezo ni mdogo. Tunaomba Serikali iliangalie hili, uwezo wa ma-contractor wanaopeleka umeme vijijini, hasa wale wanaopewa subcontract, uwezo wao ni mdogo.
Mheshimiwa Waziri, tunaomba eneo la Kibati, Mgeta, Turiani na sehemu za Mtibwa, watusaidie umeme ufike maeneo ambayo bado. Naomba ku-declare interest mimi ni mfanyabiashara wa mafuta naomba na mimi niseme mawili, matatu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hapa leo tunaongelea mafuta ya petrol, mafuta ya kula wakati wake umeshapita. Naomba ku-declare interest na mimi ni mfanyabiashara wa mafuta ya petrol, ziko changamoto nyingi ambazo tunaona ni vyema tukazisema, ili Serikali izifanyie kazi. Changamoto ya kwanza, ni katika utaratibu mzima wa mafuta yanavyoagizwa, kwa maana ya bulk wale wanaoleta, sisi tunaunga mkono azma ya Serikali kuleta mafuta kwa utaratibu wa bulk, hilo mimi sina tatizo nalo na naliunga mkono.
Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo ambalo lipo ni eneo ambalo mafuta yale yanaingia kwenye depot, kwa maana ya ghala. Sasa kwenye ghala unayatoa mafuta unayapeleka kwenye petrol station, hapo sasa ndipo ambapo tatizo linaanzia na EWURA lazima wajue changamoto hiyo. Sisi wengine hatuendi kule tunafanya utaratibu wa malipo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, wenzangu wameongea na mimi naomba niseme. Tatizo lililopo ni kwamba, EWURA wao wanakwenda kumkaba moja kwa moja mlaji hawahangaiki na mpishi wa jikoni! Mpishi wa jikoni ni nani?
Mheshimiwa Mwenyekiti, mpishi ni yule depot ambaye yeye ndiye amepata mafuta yale. Sasa yule mpishi, ambaye kapika chakula kile, wao hawahangaiki naye wanakwenda kuhangaika na mlaji na wanamsulubu sana mlaji! Naomba EWURA waliangalie hilo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka ya nyuma wakati wa Serikali ya Awamu ya Tatu utaratibu huu ulikuwa unasimamiwa na SGS, SGS walisumbua sana sekta hii. Mheshimiwa Rais Mkapa aliwatimua SGS na waliondoka kwa sababu walikuwa wanafanya mambo ambayo leo yanafanywa tena na EWURA; naomba Mheshimiwa Waziri aangalie matatizo ambayo yalikuwepo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nikukabidhi gazeti hili uweze kulipeleka kunakohusika. Taarifa iliyotolewa humu ni taarifa ya TRA, afisa ambaye ametoa takwimu hizi anasema, leo kwenye Taifa letu fedha hizi zinapotea kwa sababu ya urasimu wa EWURA. Naomba sasa tubadilike, tubadilike katika eneo hili na wenzetu wa EWURA nao wabadilike, wabadilike ili tulete tija katika Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba niseme suala moja, TRA sasa hivi wao wanajua sehemu mbili ambazo zinapoteza mapato ya mafuta; sehemu ya kwanza ni transit, sehemu ya pili mafuta yanayokwenda ndani ya nchi, hususani kwenye migodi. Upande wa mafuta yanayokwenda kwenye migodi TRA wameweka monitored by track system.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maana mafuta yanayokwenda migodini sasa hivi yako monitored tayari na yale ya transit yanalipiwa ushuru sasa hivi na wahusika wenyewe, sasa tunahangaika nini kama hayo mambo sasa hivi TRA wenyewe wanayashughulikia na wao wana-monitor mambo haya? Naomba EWURA wakae chini, waangalie upufungu wao, lakini wafike mahali waangalie na ubinadamu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, unapokifungia kituo cha mafuta unapoteza ajira za watu. Kituo kinafungwa mwaka mzima, yule mwenye kituo unampotezea mwelekeo wake, Serikali inakosa mapato, lakini yule uliyemfungia kituo ni mlalahoi au ni mjasiriamali anayehangaika kuuza mafuta rejareja, kwa nini usihangaike na wale wanaoshughulika na vinasaba? Usihangaike na wale wenye maghala ya mafuta? Kwa hiyo, wenzetu wa EWURA hebu liangalieni hili, mimi sina ugomvi na EWURA! Sina ugomvi kabisa na EWURA, lakini nawaomba changamoto zilizopo tuzifanyie kazi. Naomba sana changamoto zilizopo tuzifanyie kazi ili twende sambamba, wote nia yetu ni moja, tuhangaikie Taifa letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimwambie Mheshimiwa Waziri, kuna suala la oil refinery ya Uganda kusafisha mafuta ghafi…
MHE. SULEIMAN A. SADDIQ: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.