Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Mbaraka Kitwana Dau

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mafia

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. MBARAKA K. DAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa fursa hii ili na mimi niweze kuchangia hotuba ya Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.
Awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyetuwezesha kuwa hapa wote tukiwa salama na afya na kuweza kujadili mambo mbalimbali yanayohusu mustakabali wa nchi yetu.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa namna ya kipekee kabisa nimshukuru sana Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, ndugu yangu Mheshimiwa Makame Mbarawa na Naibu wake rafiki yangu Mheshimiwa Ngonyani kwa hotuba nzuri sana ambayo kwa kiasi kikubwa sana imejikita katika kuondoa matatizo na kero mbalimbali za wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, niende moja kwa moja kwenye uchangiaji. Kuna dhana hii ambayo ilikuwa ikizungumzwa sana ya maeneo ya pembezoni, maeneo yaliyosahaulika. Kwa bahati mbaya sana, kila inapojadiliwa maeneo ya pembezoni na yaliyosahaulika kisiwa cha Mafia kinasahaulika. Wananchi wa Kisiwa cha Mafia wana kila aina ya sababu na sifa zote za kuitwa watu ambao ni wa maeneo ya pembezoni na waliosahaulika.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi leo mtu akisafiri kutoka Dar es Salaam mpaka Mwanza kuanzia saa 12 asubuhi akifika saa 3 au 4 lakini mwingine akaondoka na boti Dar es Salaam pale akielekea Mafia basi yule wa Mwanza atafika wa Mafia hajafika. Nayasema haya kwa sababu adha ya kusafiri kwa boti kutoka Dar es Salaam mpaka unafika Mafia inaweza ikachukua siku moja mpaka mbili na ndiyo maana kwa makusudi kabisa tukaamua wananchi wa Mafia wanapotaka kusafiri wanakwenda Kusini kidogo kwa kutumia barabara ya Kilwa mpaka maeneo ya Mkuranga, wengine wanakata kushoto wanakwenda Kisiju. Sasa matatizo yanaanza pale, barabara ya Kisiju - Mkuranga kilometa kama 46 ni ya vumbi, ni mbaya sana na imekuwa ikipigiwa kelele sana lakini bado haijashughulikiwe.
Mheshimiwa Mwenyekiti, pia bandari ya Kisiju ni kama economic hub ya Kisiwa cha Mafia kwani mazao yote ya nazi na yanayotokana na bahari yanapitia bandari ya Kisiju lakini tatizo la uharibifu wa barabara ile ya Mkuranga – Kisiju ni kubwa. Nimeangalia kwenye Kitabu cha Mheshimiwa, nikakisoma mara mbili mpaka tatu sikuiona barabara ya Mkuranga - Kisiju ambayo ni kilometa 46. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati anahitimisha basi alitolee maelezo suala hili.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini namna ya pili ambayo abiria wengi wanaitumia kufika kisiwa cha Mafia ni kwenda mpaka Bungu, Rufiji wanakata kushoto wanakwenda mpaka kwenye bandari ya Nyamisati. Baina ya Bungu na Nyamisati ni kama kilometa 41, pale napo pia barabara ni kama hakuna. Ina mashimo na kipindi kama hiki cha mvua inakuwa kama imekatika. Wananchi wa Mafia wanaposafiri na boti kutoka Kilindoni wakafika Nyamisati wana kazi nyingine pale ya kudandia magari mbalimbali na wengine bodaboda ili wafike Bungu na hatimaye kuja Dar es Salaam. Naomba sana Mheshimiwa Waziri wakati unahitimisha ulielezee hilo pia.
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kwa upande wa Kisiwani Kwenyewe Mafia, kuna barabara kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi kilometa 55. Mkononi kwangu hapa nina Ilani ya Chama cha Mapinduzi ambayo ndiyo tuliyoinadi kwa wananchi, ndani ya Ilani hii inasema wazi kabisa, Chama cha Mapinduzi kwa miaka mitano ijayo tutajenga barabara kwa kiwango cha lami kutoka Kilindoni - Rasi Mkumbi (Bweni). Hata hivyo, nimeangalia kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri sikuiona barabara hiyo. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri nakuomba sana atakapokuja ku-wind up alitolee maelezo na hilo nalo.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Mafia kuna barabara inaitwa Airport Access Road kilometa 14 inatoka Kilindoni inakwenda mpaka Utende ambayo imetengenezwa kwa kiwango cha lami. Kwa masikitiko makubwa sana, barabara ile haijakabidhiwa huu unafika mwaka mmoja toka imekamilika. Naiomba sana Serikali na Mheshimiwa Waziri, itakapofika wakati mkandarasi anataka kuikabidhi barabara ile Serikali msikubali kuipokea kwani ina mashimo mwanzo mpaka mwisho na mpaka leo haijazinduliwa. Barabara ina matatizo, kuna jokes zinaendelea kule Mafia wanasema kama gari ikipata pancha ukipiga jeki badala ya ile gari kwenda juu basi jeki ndiyo inatitia chini kama vile umepiga jeki kwenye matope. Kubwa zaidi wenyewe wanaiita barabara ya Big G maana yake ina mashimo mashimo mengi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haraka haraka nizungumzie kuhusu Bandari ya Nyamisati ambayo na yenyewe pia imo katika kitabu hiki cha Ilani ya CCM. Jana kwa bahati nilipata fursa ya kuongea na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA) akanithibitishia kwamba bandari ile itajengwa lakini pesa zilizotengwa zilikuwa ni kidogo na walipoenda kufungua zabuni wakakuta ame-quote shilingi bilioni nane na wao Mamlaka ya Bandari hawana uwezo wa kulipia fedha hizo. Akanihakikishia Mkurugenzi Mkuu kwamba wamenunua dredger (mashine la kuchimbia na kuongeza kina kwenye bandari), kwa hiyo wamesema kazi hiyo wataifanya wao wenyewe.
Mheshimiwa Waziri naomba wakati utakapokuja ku-wind up uniambie na uwaambie wananchi wa Mafia ni kiasi gani kimetengwa kwa ajili ya Bandari ya Nyamisati kazi ambayo wataifanya wenyewe Mamlaka ya Bandari? Vinginevyo kwa mara ya kwanza mimi sijawahi kutoa shilingi hapa lakini leo kama nisiposikia habari ya Bandari ya Nyamisati kiasi gani kimetengwa na mimi nitaingia kwenye record hapa ya kuzuia shilingi au pengine hata noti. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nizungumzie upanuzi wa uwanja wa ndege wa Mafia. Sasa hivi tuna kilometa 1.5 ili ndege kubwa ziweze kutua tunahitaji runway yenye angalau kilometa 2.5 ili watalii waweze kuja moja kwa moja katika Kisiwa cha Mafia. Ndugu yangu Mheshimiwa Waziri iliyobaki pale ni kilometa moja tu, naomba sana mtupatie hiyo kilometa moja ili watalii waweze kuja Mafia na tuweze kunufaika na biashara ya utalii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, MV Dar es Salaam…
MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa Dau nakushukuru sana.