Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Bonnah Ladislaus Kamoli

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Segerea

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. BONNAH M. KALUWA: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipa nafasi ya kuongea. Pia nimpongeze Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo ameitoa.
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri sijaona bajeti ya wakazi wa Kipunguni ambao wapo Kata ya Kipawa. Wakazi hawa wa Kipunguni kama Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 inavyosema watu wanaweza wakaiachia sehemu kama Serikali inaiihitaji lakini kwa kupata fidia. Wananchi wa Kipunguni wa Kata ya Kipawa, mtaa wa Kipunguni na wa Mashariki, wamefanyiwa tathmini mwaka 1995 lakini mpaka leo hawajawahi kupewa hiyo fidia. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, wananchi hawa wengine sasa hivi wamekuwa ni wazee na wengine ni wastaafu wana maisha magumu sana. Kwanza, zile nyumba zao hawawezi kuendeleza kitu chochote kwa sababu hizo leseni zao za makazi hawawezi hata wakawapa benki au mtu yeyote ili waweze kupata kitu chochote ambacho kinaweza kikawasaidia kwa miradi yao maendeleo. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa anafanya majumuisho ya hotuba yake atueleze ni lini sasa Serikali itawalipa fidia hawa wananchi wa Kipunguni pamoja na Mashariki. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia nataka Waziri aje kutueleza kwamba hawa wakazi waliofanyiwa tathmini mwaka 1995 watakapowapa sasa hivi hiyo fidia watawapa fidia ya aina gani. Kwa sababu mwaka 1995 hata mfuko wa simenti ulikuwa unauzwa bei ndogo, lakini kwa sasa hivi bei zimeshapanda na hawa wakazi ndio kama hivyo bado wanasubiri wapewe fedha zao au hiyo fidia ambayo walifanyiwa tathmini 1995. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri akija anipe hayo majibu mawili, kwanza aniambie atawalipa lini na pili aniambie atatumia sheria gani ya kuwalipa hawa watu waliofanyiwa tathmini mwaka1995. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine nataka niongelee Bodi ya Wakandarasi kwa sababu Dar es Salaam, Manispaa ya Ilala barabara zetu zimekuwa zikitengenezwa kwa kiwango duni sana. Mfano kama barabara ya St. Mary’s, Vingunguti ambayo inatokea Barakuda na Kimanga zimetengenezwa lakini sasa hivi haziwezi kupitika kwa sababu waliotengeneza wametengeneza kwa kiwango duni na magari yanayopita hapo ni makubwa sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba Mheshimiwa Waziri atuambie Bodi ya Wakandarasi wanashughulikia kitu gani kwa sababu tumekuwa kila mwaka tunarudia kutengeneza barabara na hii inatufanya wakazi wa Manispaa ya Ilala hasa Jimbo la Segerea wasiweze kwenda mbele kwa sababu ya barabara. Hizi barabara nazoziongelea ni barabara ambazo kama zingetengenezwa vizuri na kama zingeweza kupitia vizuri basi kungekuwa hakuna foleni pale TAZARA au Ubungo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri naomba kwenye hii Bodi ya Wakandarasi pamoja na kwamba unasema sasa hivi tunasaidia wakandarasi wazawa, lakini tuwasaidie wakandarasi wazawa wenye uwezo. Tumeangalia wakandarasi wengi ambao wanasema kwamba wanasaidiwa na sisi tunashukuru kwa sababu wakandarasi wazawa watakaposaidiwa ndiyo na nchi yetu inapiga hatua lakini sasa hawa wakandarasi hawana vifaa vya kufanyia kazi. Mfano mimi nilimtembelea mkandarasi ambaye anajenga daraja Boyonkwa, nimekuta mchanga anabebea kwenye matoroli, hana vifaa vya kufanyia kazi na nilivyouliza sana wanasema mkandarasi huyo hana vifaa vya kufanyia kazi lakini bado wanaendelea kupewa tender na Manispaa ya Ilala. Hiyo inatukwaza sisi watu wa Manispaa ya Ilala lakini pia inatukwaza watu wa Dar es Salaam kwa sababu hawa ndiyo ambao wanaendeleza foleni inakuwa kubwa. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kitu kingine ambacho nataka niongelee ni kuhusu daraja ambalo linaunganisha Kipawa na Kata ya Segerea na kuja daraja lingine ambalo linaunganisha Kipawa na Kata ya Kinyerezi. Najua kwamba TANROADS wamejenga daraja ambalo linaunganisha Kata ya Kipawa na Segerea lakini hili daraja lingine ambalo ni la Kata ya Kipawa linalounganisha Segerea na lenyewe ni kubwa kama linalounganisha Kipawa na Kinyerezi. Nimesikia daraja lile linajengwa na Manispaa ya Ilala kwa maana kwamba linajengwa na TAMISEMI.
Mheshimiwa Naibu Spika, tangu mwaka 2011 hili daraja lilipochukuliwa na mafuriko halijawahi kujengwa mpaka leo 2016 kila mwaka wanalipangia bajeti lakini hakuna kitu chochote kinachoendelea. Kwa hiyo, namuomba Mheshimiwa Waziri aangalie ni jinsi gani anaweza akafanya hili daraja walichukue wenyewe la si hivyo wananchi wanaendelea kupata matatizo, mvua ikinyesha wananchi wa Segera wanabaki Segerea, wananchi wa Kipawa wanabaki Kipawa. Cha ajabu daraja ambalo lina vigezo kama hivyo ambalo linaunganisha Kinyerezi na Kipawa limejengwa. Nimuombe sana Mheshimiwa Waziri atakapokuja aweze kutuambia atafanya kitu gani katika mambo hayo.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nalotaka kuongelea ni bandari kavu. Mji wetu wa Dar es Salaam sasa hivi una foleni kubwa kutokana na kwamba hakuna bandari kavu, magari yote yanarundikana sehemu moja. Kwa hiyo, tunaomba Mheshimiwa Waziri asimamie tupate bandari kavu pale Kibaha ili magari yaweze kuwa yanakusanyikia hapo, lakini pia tuondoe hizo conjunction za Dar es Salaam, kwa sababu sasa hivi Dar es Salaam magari ni mengi.
Mheshimiwa Naibu Spika, naunga mkono hoja.