Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia Wizara hii ya Ujenzi. Kwanza kabisa Waziri akija kutujibu hapa jioni, ningependa atufafanulie katika hizi fedha za maendeleo ni kiasi gani kinakwenda kulipia madeni ya Wakandarasi ambayo natambua yameanza kulipwa, ni kiasi gani kinakwenda kumalizia miradi tuliyopitisha bajeti ya mwaka jana na kiasi gani kinakwenda kwenye miradi mipya, isiwe kiujumla hivi. Tunaomba, mmesema hapo kazi na sisi tunataka tuwasimamie muifanye kazi kiufasaha, siyo jumla jumla hivi, aje atuambie, kwenye randama sijaona. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningetaka kulizungumzia na hili pia nitasema kama Waziri kivuli wa Sera, Uratibu, Bunge na mazagazaga mengine. Mwaka uliopita kwenye Mfuko Mkuu, Wizara hii ilipitishiwa bilioni 199, leo kwenye kitabu chake Mheshimiwa Waziri amekiri mpaka Aprili amepokea bilioni 600. Kwa utaratibu wa kuheshimu mihimili amepata zote na ziada, alimpitishia nani? Huku ni kuvunja Katiba na kudharau Bunge, alipata zote, kuna Wizara zingine hazijapata, kaka yangu Mheshimiwa Nape wamempa bilioni mbili, mwaka jana tulimpitishia bilioni tatu hizi bilioni 500 nani alimpitishia?
Mheshimiwa Naibu Spika, lazima Bunge liheshimiwe, lazima tufuate Kanuni, lazima tufuate Katiba, kuna Wizara nyingine hazipata hata asilimia 50, yeye amepata 200 tofauti na tuliyompitishia humu, hatusemi asipewe pesa, tunataka utaratibu ufuatwe ili kujenga nidhamu ya matumizi. Leo kuna akinamama kule wanaomba gloves tumepitisha bilioni mia na, amepata 600 nani kampitishia? Tunapoyasema haya tunataka tutengeneze nidhamu, hatuna hila, mimi mwenyewe nataka apate fedha, angekuja kuomba sasa hivi tupitishe leo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naendelea, Mheshimiwa Rais wetu mtukufu, mpenzi sana amesema tunataka tujifunge mkanda tubane matumizi fedha nyingi ziende kwa wanyonge. Kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri naona kuna residential house, Ikulu, JK ametoka miezi sita iliyopita imeharibika lini? Kila mwaka hapa tunapitisha fedha za ukarabati, je, amemtuma?
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwambalaswa amesema ukimtazama moyoni dhamira yake ni kwa wanyonge, hizi fedha mngepelekea TEA aende akatengeneze miundombinu ya elimu. Sasa hivi Wahisani wamegoma kuleta pesa, kipaumbele siyo kujenga residential house Ikulu, tupeleke kwenye miradi ya maendeleo wangempa Mheshimiwa Nape, wangepeleka TBC, wangepeleka na maeneo mengine. Kipaumbele residential house Ikulu, Dar es Salaam? (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri, jambo lingine nimesoma ripoti ya CAG, kuna halmashauri tano zimetoa mikataba ya utengenezaji wa barabara zaidi ya bilioni moja na milioni mia saba bila kujua dhamana ya hawa Wakandarasi, kweli! Ndiyo maana kule kwenye Halmashauri zetu mtu anaomba tenda hana hata greda, kwa nini wasilime barabara kama mashamba? Huu ni wizi, lazima usimamiwe, tukisema wizi usimamiwe tunataka biashara hii ikome ili Jimboni kwangu kule wananchi wangu watengenezewe barabara, mambo yaende hatuwezi tukasema funika kombe mwanaharamu apite, halafu hapiti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nakuja Jimboni. Mwaka jana walitupa bilioni moja utengenezaji wa barabara ya kuanzia kwa kaka yangu kule Mheshimiwa Kangi, Kisolya – Bulamba – Bunda – Nyamswa, na hili nilimwambia Mheshimiwa Waziri, mwaka jana ilipitishwa kwa kiwango cha lami leo naona imewekwa kwenye changarawe, tuchukue lipi? Wananchi wa Bunda kuanzia Mwibara kwa kaka yangu kule Mheshimiwa Boniphace Mwita, tueleweje, ni kiwango cha lami au cha changarawe? Hata hivyo, Mkoa wa Mara umekuwa ukipewa fedha ndogo kila mwaka, Mheshimiwa Rais alivyoomba kura alisema hizi ni kiwango cha lami hapa mmetuwekea changarawe, lipi ni lipi? Maneno yanakwenda huku, vitendo kule, tuamini kipi hapa?
Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kulikuwa kuna ukarabati, upanuzi wa barabara kubwa ya kutoka Dar es Salaam kwenda Musoma, Mheshimiwa Waziri wananchi wangu waliridhia kupisha upanuzi wa barabara wameshafanyiwa tathmini huu mwaka wa nne pamoja na baba yangu Mzee Wassira nyumba yake iko Manyamanyama, mnawalipa lini? Sasa mtuambie hapa lini mnawalipa hawa? Yuko na Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Gimano anadai humu, lini mnawalipa? Kuna wazee maskini mmoja babu yangu, mpaka amekufa jana hajalipwa, kwa nini mliwafanyia tathmini mpaka leo hamjawalipa, naomba majibu. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine, Mheshimiwa Waziri Halmashauri yangu mimi ni mpya barabara nyingi haziko sawa, kupitia TANROADS Mkoa wa Mara mmejipanga vipi kuhakikisha hizi Halmashauri changa mnazisaidia. Kwanza kama mnavyojua Wilaya ya Bunda ni miongoni mwa Wilaya maskini, Wizara kupitia TANROADS Mkoa wa Mara mnajipanga vipi kuhakikisha hizi Halmashauri mnazipa support kuhakikisha barabara zinapitika.
Mheshimiwa Naibu Spika, natambua kuna nyingine zimeshaanza kufanyiwa kazi kama Balili – Mgeta, namshukuru Mkurugenzi wa TANROADS Mkoa wa Mara na maeneo mengine ya Kangetutya, Manyamanyama, sasa hizi nyingine hizi mna mkakati gani wa kuhakikisha mnazisaidia ?Ahsante sana.