Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Richard Mganga Ndassa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Sumve

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa nafasi ya kwanza asubuhi hii, nijaribu kujadili hotuba ya Mheshimiwa Waziri wa Ujenzi. La kwanza, naomba tumwombee Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi nzuri sana anayoifanya, lakini naye pia amekuwa akituomba sisi Watanzania wote kwa dini zetu zote, tumwombee sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, pili, hili ni ombi, sisi kama Wabunge tumekuwa na maneno mengi sana humu ndani ambayo kwa kweli hayana tija sana kwa Watanzania. Nawaomba sana Waheshimiwa Wabunge wa pande zote mbili; upande wa CCM lakini na upande wa wenzetu; Watanzania wanaotusikiliza na kutuona, wanategemea tutoe michango ili kusudi wataalam walioko hapa waweze upata ushauri mzuri zaidi. Hili kwa kweli naomba sana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niongezee hapo kwamba, ni vizuri kwa sababu tunazo Kanuni zetu, zituongoze katika kuendesha Bunge letu. Endapo limetokea tatizo, Kiti chako kisisite kuita Kamati ya Uongozi, kwa sababu tukienda na utaratibu huu kama ilivyo sasa, juzi kuna wanafunzi kutoka Msalato walikuwa wamekaa pale, lakini baada ya kuanza kurushiana maneno na kutupa vitabu, wale wanafunzi ambao walikuwa wamekuja kwa ajili ya mafunzo, waliondoka humu ndani. Sasa kwa utaratibu huo, wanapotoka Walimu wao na wao wenyewe wanatuelewaje sisi kama Wabunge? Kwa hiyo, nashauri sana hili tulizingatie kwa sababu sisi ni jicho la Watanzania. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la pili, Mheshimiwa Waziri nataka aniambie, kupitia hotuba yake hasa ujenzi wa Mwanza Airport, imetengwa shilingi bilioni 30. Ni za nini? Ni za kujenga uwanja au ni za kukarabati? Kwa sababu tumekuwa tukisema mara kwa mara, jinsi mnavyotenga pesa kidogo kidogo hizi, hazitoshelezi hata kidogo. Ujenzi wa Mwanza Airport gharama yake ili ikamilike, siyo chini ya Dola bilioni 60 mpaka 90. Sasa leo mkitoa shilingi bilioni 30, pesa hizi hazitoshi. Nashauri Mheshimiwa Waziri, hebu suala hili alitazame upya.
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, nizungumzie reli ya kati. Namshauri Mheshimiwa Waziri, nimeongea na Naibu wake, mabehewa wanayopeleka kutoka Mwanza…
MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Naibu Spika, mabehewa wanayopeleka Mwanza kuja Dodoma au Tabora ni machache mno. Unapeleka mabehewa matatu ya abiria kutoka Tabora kwenda Mwanza; kuna msongamano wa abiria kule, lakini watu weo Mheshimiwa Waziri wanawadanganya eti kwamba abiria ni wachache, siyo kweli. Inawezekanaje eneo lingine wakapeleka mabehewa 15 lakini Tabora - Mwanza, mabehewa matatu; wanasababisha watu walanguliwe. Nashauri suala hili litazamwe kwa mara ya pili. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, zipo ahadi za Mheshimiwa Rais mbili; ya kwanza ni ujenzi wa barabara ya lami kutoka Magu mpaka Hungumalwa, sijaiona humu ndani. Ahadi ya pili, wataalam nafikiri walikuwepo siku ya uzinduzi wa Daraja la Mto Simiyu pale Marigisu. Mheshimiwa Rais aliahidi kuweka mita hamsini hamsini kwa kiwango cha lami, lakini sijaona humu. Nashauri hiyo ni ahadi ya Mheshimiwa Rais. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nishauri, barabara ya kutoka Nyanguge kwenda Musoma na barabara ya kutoka Mwanza - Shinyanga Border barabara hizi zimekuwa zikitengewa pesa mara kwa mara; hivi kwa nini tusiangalie namna nyingine nzuri zaidi ili kusudi barabara hizi zikwanguliwe zote kwa mara moja, halafu ijengwe upya kuliko hivi ilivyo sasa? Tutakuwa tunatenga pesa mara kwa mara lakini pesa hizo hazina maana. Kwa hiyo, nashauri wajaribu kubadilika kidogo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, lingine, siku ile niliuliza swali hapa na kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri amesifia hizi ndege zinazotoa huduma humu ndani kwa maana ya kwenda Mwanza na Mbeya. Pamoja na kusifia, lakini ndege hizi zinaumiza sana wasafiri wetu. Bei ni kubwa mno! Kutoka Dar es Salaam kwenda Mbeya, sh. 700,000/=, ukienda na kurudi sh. 1,400,000/=; kutoka Mwanza kwenda Dar es Salaam, sh. 800,000/=; kwenda na kurudi ni shilingi milioni moja na kitu.
Mheshimiwa Naibu Spika, mfano ukichukua ndege kutoka Dodoma kwenda Dar es Salaam, siyo chini ya sh. 800,000/=. Hebu tuangalie, ndiyo tunataka huu usafiri, lakini basi usafiri huu usije ukawa kama ni adhabu kwa Watanzania. Nashauri chombo ambacho kipo chini ya Mheshimiwa Waziri kisimamie vizuri ili kusudi wananchi wetu wengi wapande usafiri huo. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu, nawapongeza sana Mamlaka ya Hali ya Hewa kwa taarifa nzuri ambazo wanatupa sisi Watanzania. Ombi langu kwa upande huu, kama vifaa vyao ni vichache kwa sasa na wanafanya kazi katika mazingira magumu, hebu waongezewe vifaa ili kusudi mamlaka hii iweze kufanya kazi yake vizuri zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, la mwisho, tunazo taasisi zetu mbili; TPA kuna Kaimu, hakuna Bodi. Kuna maamuzi mazito yapo pale yanatakiwa yatolewe na Bodi. Nataka uniambie, Bodi ile itaundwa lini? ATCL kuna Kaimu, hakuna Bodi na bahati nzuri unasema unataka kupeleka ndege pale. Hivi utaamua mwenyewe pale au itaamua Bodi? Vyombo vile Mheshimiwa Waziri, ni lazima kuwe na Bodi ili iweze kusimamia majukumu yote yaliyopo pale kwa sababu yapo kwa mujibu wa sheria. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, namshauri Mheshimiwa Waziri, najua mengine hayapo chini yake, lakini bado ana uwezo wa kumwomba Mheshimiwa Rais ili kusudi taasisi hizi hasa TPA kwa sababu kuna mambo mengi mazuri pale, sasa nani anayasimamia? Nani anaamua? Namwomba sana, Mheshimiwa Waziri, hayo nayo ayachukue.
Mheshimiwa Naibu Spika, kubwa zaidi naomba Mwanza Airport Mheshimiwa Waziri asipoleta majibu ya kutosha humu ndani nitakamata shilingi. Namwambia mapema kabisa! Shilingi nitaondoka nayo mpaka nipate majibu kwa sababu kila mwaka wanasema watatenga fedha. Mwaka 2015 ilikuwa ni hivyo hivyo, tukatenga fedha nyingi chini ya Mheshimiwa Mtemi Chenge, tukaahidiwa, lakini hakuna fedha iliyotoka. Safari hii namwambia Mheshimiwa Waziri tutaungana watu wote wa Kanda ya Ziwa ili tupate majibu ya kutosha kuhusu Mwanza Airport. Wamesema wengi sana humu ndani na jana Mheshimiwa Maige alisema. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, hivi Mheshimiwa Waziri akilinganisha viwanja vya ndege, sikatai maeneo mengine, kwa ajili ya uchumi wa nchi yetu. Mwanza Airport, hivi hawaijui kwamba ina faida gani kwa nchi hii? Nashauri sana. Mheshimiwa Waziri atakapokuja kujibu alete majibu ya kutosha. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, reli ya kati na yenyewe ina maneno. Standard gauge wanayosema sijui, lakini bado nasema viwanja vya ndege Mwanza Airport na reli ya kati. Vitu hivi viwili wakisimamia vizuri, nina uhakika tutasonga mbele. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana na naunga mkono hoja.