Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

Hon. Savelina Slivanus Mwijage

Sex

Female

Party

CUF

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa Mwaka wa Fedha wa 2016/2017.

MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. Nami kwanza namshukuru Mwenyezi Mungu niweze kuchangia hotuba hii. Kwanza nichangie suala moja linaloniudhi na kuniletea kichefuchefu, barabara ya kutoka Mlandizi kuja Chalinze; barabara ambayo ina matuta utafikiri wanapanda viazi, inanikera. Ni barabara ambayo tunaitegemea wote, Maraisi wanapita pale, Mawaziri wanapita pale, ile barabara ni mbaya sijui kama Mheshimiwa Waziri ameweza kuitengea fedha kwa sababu wote tunapita pale, tunaiona hiyo barabara ilivyo. Ukipita pale kwa speed lazima upate mweleka.
Mheshimiwa Spika, Wakandarasi wanaopewa shughuli zote za barabara, sijui wanakuwa wametoa rushwa mimi sielewi, kwa sababu barabara inatengenezwa siku mbili, tatu imeshaharibika, unakuta mashimo. Ni kwa nini wasitafutwe Wakandarasi ambao ni wasomi, wana uelewa wanajua kutengeneza? Kwa sababu ukiangalia barabara zote zinazotengenezwa Tanzania nzima, ni miezi miwili, mitatu tayari ina mashimo. Naona Wakandarasi hawa huwa wanatoa rushwa ndiyo maana wanapata hizo kazi. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye usafiri wa Ziwa Victoria. Nina majonzi makubwa sana kwa Wanakagera. Tumeanza kupata meli ya kwanza mwaka 1961 kwenye uhuru; Victoria, tukapata meli ya Usoga, tukapata Butiama, tukapata MV. Bukoba, lakini meli zote hizo unazozisikia zimeshakuwa chakavu na Victoria kila mwaka mnatenga bajeti ya kukarabati. Ni lini mtatuletea meli mpya? Kwa sababu tunapata ahadi kutoka kwa Marais na Rais kila anapoingia kwenye mchakato wa kampeni, anaahidi meli moja au meli mbili mpya; mpaka leo hii sasa naona mnaweka fedha za kukarabati. Hatutaki tena kukarabatiwa meli zikaja kuwaua watu, hatukubali tena kwa sababu kile kitendo cha MV - Bukoba kuendelea kuiweka ndani ya Ziwa Victoria imeua watu; mpaka mmekuja kusema kwamba irudi hiyo meli ya MV Victoria. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naiomba sana Serikali, watu wa Mkoa wa Kagera pamoja na wa Kanda ya Ziwa siyo watu wa kuwategeshea ili wakarabati siku mbili, tatu unakuta imezama, inakwenda Kemondo imezama, inakwenda kwenye Bandari ya Bukoba. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, naomba kuuliza, Bandari ya Kemondo na Bandari ya Bukoba Mjini hazijawahi kufanyiwa ukarabati toka kwa mkoloni mpaka sasa hivi. Ukiangalia hizo bandari, zilikuwa zinatumika kupeleka mizigo Uganda, inatumia meli ya Umoja, inatoa mizigo pale Bukoba Mjini inapeleka Uganda, inatoa Uganda inapeleka Kemondo, inatoka Kemondo inapeleka Musoma. Mpaka leo hii wananchi wa Bukoba pamoja na wa Kanda ya Ziwa wamekuwa maskini kwa sababu hawana sehemu ya kusafirishia, kupata uchumi katika mkoa wetu. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye barabara. Sisi tuna barabara ambazo zinaunganisha nchi zetu jirani. Tuna barabara ya kutoka Mushaka kwenda mpaka Kyerwa mpaka Uganda. Hiyo barabara nafikiri miaka nenda rudi haijawahi kutengewa fedha au kuisema katika orodha kwamba inatengenezwa au imewekewa fedha, sijawahi kusikia. Ni mashimo, kutoka Mushaka kwenda mpaka Kyerwa mpaka Mlongo. Ni barabara ambayo tunaweza kufanya biashara na watu wa Uganda kwa sababu ni njia ya karibu ya kuunganisha na Karagwe. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, barabara ya kutoka Mushaka kwenda mpaka Benako - Ngara ni barabara ambayo inatuunganisha kwenda Rwanda na Burundi, lakini ni mbaya na majambazi wanatuteka mle mara kwa mara, kwa sababu barabara ni mbaya. Sijawahi kusikia Serikali inaiongelea au kusema kwamba kuna kipindi ambacho itatengenezwa au wameitengea fedha kadhaa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende kwenye barabara tena. Kuna barabara ya kutoka Kanazi inakwenda Kafunjo, kuna daraja Kafunjo pale linaitwa Kalebe kabla hujafika Ibwela. Hilo daraja ni bovu sana. Kinachonishangaza ni kimoja na kila Mbunge wa Mkoa wa Kagera akisimama hapa anaeleza hiyo barabara, ni mbaya sana na tunaitegemea, mtu akitoka Kanazi anakwenda Ibwela akitoka Ibwela anaenda Kafunjo, akitoka anaunganisha, yuko Kyaka, tayari ameshaingia Uganda.
Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, ninachoomba, Mkoa wa Kagera ukiangalia hata kwenye bajeti za Mawaziri wote sijaona bajeti ambayo inatugusa Wanakagera, naomba sana kwa Mheshimiwa Waziri, wawe wanatukumbuka, nasi ni wananchi wao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, nakwenda kwenye viwanja vya ndege. Kiwanja cha Ndege cha Bukoba Mjini kimefanyiwa ukarabati, lakini tuna ahadi ya miaka nenda rudi Kajunguti. Kajunguti ina ahadi ya miaka mingi. Sisi tuna zao la ndizi Bukoba tuna mazao ya matunda; tungekuwa na uwanja ambao ni mkubwa na sisi tungekuwa tunasafirisha hata matunda yetu kupeleka nje, kwa sababu unakuta ndizi zinasafirishwa kupelekwa Uganda, Uganda wanasafirisha kupeleka nje, lakini sisi wenyewe hatuna. Ni kitu cha kukuza uchumi katika Mkoa wetu wa Kagera. Naomba sana na sisi wawe wanatukumba ni Watanzania wenzao. (Kicheko/Makofi)
Mheshimiwa Spika, narudi tena hapo hapo kwenye uwanja wa Bukoba. Uwanja wa Bukoba ni mfinyu sana. Kila wanapopanga fedha, wanapanga fedha ambazo ni kidogo kwa sababu unakuta huku kuna wananchi na huku kuna wananchi. Wanapanga fedha kidogo! Kwa nini isitengwe fedha ambayo ni kubwa angalau watu wote wa upande mmoja wakaondolewa, wakabaki wa upande mmoja, ukapanuliwa, tukawa tunasubiri hizo fedha za Kajunguti zitengwe. Hata juzi ndege imeleta matatizo ni kwa sababu ya hali ya hewa ya pale Bukoba.
Mheshimiwa Spika, naomba sana hali hiyo hiyo, michango hiyo inayochangia kuhusu barabara kuhusu na uwanja wa ndege tuna masikitiko makubwa, ni kwa sababu na sisi tuna uchumi ambao tunaweza kufanya. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukipata uwanja wa ndege mkubwa, tukipata barabara za kuunganisha na sisi tungekuwa tunajivunia Mkoa wetu wa Kagera, urudi kama Kagera ilivyokuwa zamani.
Mheshimiwa Spika, tunazalisha kahawa; utapeleka wapi kahawa? Naomba sana Mheshimiwa Waziri akija hapa aweze kutueleza sisi Wanakagera wanatuweka upande gani? Upande wa kukosa kabisa bajeti ya Serikali au upande wa kuwekewa kiporo au upande wa kutokukumbukwa kabisa? Tuelewe, hata sisi tujue kwenye bajeti ya Serikali, hatukumbukwi kabisa. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa kusema, barabara za Bukoba Mjini. Nasikitika, barabara za Bukoba Mjini ukiangalia na kipato cha Halmashauri yetu ni kidogo sana kwa sababu hatuna kipato chochote pale Bukoba na ni kwa sababu ya maunganisho ya hizo barabara nilizozisema. Ni mbovu ni mbaya, hatuna Stendi, hatuna Soko, hatuna nini; ni watu ambao tunakaa kwa kukaa kufikiria tufanye nini.
Mheshimiwa Spika, naomba kwa mchango wangu huo, nina majonzi makubwa, naomba Serikali itoe macho iangalie Mkoa wa Kagera na sisi tuweze kupata kipato, tupate hata kale kasungura tulikonako kadogo, kaende Mkoa wa Kagera. Naomba kuishia hapo.