Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

Hon. Angelina Adam Malembeka

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mpango na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa mwaka wa fedha 2016/2017.

MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.
Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza naomba wenzangu wa upande wa pili wawe watulivu na hizo microphone wasiwe wanawasha kwa sababu sisi huwa hatuwashi. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa na timu yake yote. Pia nichukue nafasi hii kipekee kumpongeza Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Dkt. Magufuli kwa kazi nzuri anayoifanya. Kiaina nimpongeze aliyetengeneza kitabu hiki kwa kumwonesha komandoo akiwa kwenye mavazi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu kwenye Wizara hii kwanza naunga mkono kwa asilimia mia moja. Nichangie kwenye nyumba za askari. Nimeona juhudi za Wizara katika kujenga nyumba za askari. Naomba Serikali yangu tulivu iendelee kuwajengea nyumba askari hawa ili waweze kuishi vizuri na kufanya kazi zao kwa umakini zaidi. Nimeona maeneo mbalimbali ambapo nyumba zimejengwa.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia niombe Serikali yangu tulivu iendelee kuboresha maslahi ya askari wetu ikiwepo mishahara na vyombo ya usafiri. Niombe pia Wizara hii kwa nguvu za dhati ihakikishe mafunzo kwa askari wapya yanafanyika yakiwa yamelenga kada tofauti. Nimesikitishwa hapa na mwasilishaji wa Kambi ya Upinzani akishangaa Askari mstaafu kuwa mganga wa kienyeji. Mimi naamini kabisa kule kwenye uaskari siyo kwamba wana fani moja tu ya kushika bunduki na kucheza gwaride. Najua kabisa kule tunao Askari ambao ni wajasiriamali, wana ujuzi wa teknolojia mpya, wanahabari, wanamichezo, madaktari, madereva, marubani, walimu, mafundi umeme na waokoaji. Kwa hiyo, huyo Askari aliyeenda kuwa mganga wa kienyeji ndiyo fani yake usimlaumu.
Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kuchangia zaidi katika ajira. Naomba jeshi hili hasa Jeshi la Wananchi liangalie uwiano wa mikoa yote. Kuna baadhi ya maeneo imeonekana kama vile kuna kabila moja tu ndiyo jeshi hilo kazi yake mpaka inafika kipindi mitaani huko ukiwauliza JWTZ ni nini, wanakwambia ni Jeshi la Wakurya Toka Zamani.
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba ajira zile ziangalie mikoa mbalimbali angalau ukikuta Wachaga kumi basi na Wamasai, Waluguru na Wapare wapo isiwe kabila moja ndio linafanya kazi ya jeshi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niombe pia Wizara hii iangalie ubunifu wa vijana wetu. Tunao vijana wengi ambao katika utundu wao wameweza kubuni redio, TV, simu mpaka helikopta. Ni vizuri jeshi hili likawachukua vijana wale na kuwapa mafunzo halafu baadaye wapate ajira. Nategemea kwa kufanya hivyo tutaendelea kuwa na vijana ambao watakuwa askari bora zaidi. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nichangie pia katika kambi za jeshi. Najua wakati zinaanza zilikuwa nje ya mji lakini baadaye mji jinsi ulivyokua imeonekana kama vile vimeingiliana. Katika kuepuka madhara zaidi ya mabomu kama yale ya Gongo la Mboto na Mbagala au kuepuka migogoro ya ardhi kati Wanajeshi na raia lakini pia kuepuka migororo ambayo mingine inaingilia mipaka ya kimapenzi kati ya Askari na raia, ni vizuri basi tuangalie uwezekano wa kubadilisha makazi hayo. Mapori bado tunayo mengi, wahame kidogo waende kule ili wananchi waweze kukaa katika maeneo hayo kwa utulivu. Yapo maeneo ambayo hayawezekani kuhamishwa kutokana na hali halisi ilivyo basi wale ambao wanazunguka eneo lile wahamishwe kwa utaratibu unaofaa ili waweze kupisha jeshi.
Mheshimiwa Naibu Spika, pia hii itasaidia katika kujenga heshima ya jeshi. Imefika sehemu heshima ya jeshi inaanza kupungua kwa sababu wanajichanganya sana na raia. Katika kujichanganya na raia unakuta kuna mambo mengine ambayo Wanajeshi wanafanya unashangaa. Hata katika foleni za magari unakuta kwenye mchepuko na yeye anaingia, unatazama unaona ni Askari na ana kofia. Napenda zaidi Askari waoneshe wao wako makini na ni watii wa sheria, siyo wote wanaofanya hivyo ni baadhi. Wapo ambao pia wanakuwa wasumbufu katika maeneo ya watu yaani hata jirani yake anaogopa kukaa jirani na mjeshi. Naomba wale wachache wenye tabia kama hizo wabadilike. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, nielezee kuhusu baadhi ya shule ambazo zinasimamiwa na jeshi zikiwepo shule binafsi nikitolea mfano Mgulani na Lugalo.
Kuna shule ambazo zimeendeshwa vizuri wanafunzi wa pale wanakuwa na maadili mazuri. Ni vizuri shule kama zile ziendelezwe na kupewa ushirikiano ili tuendelee kupata wanafunzi wenye nidhamu na wenye uchungu na nchi yao ambao hata kesho wakija huku Bungeni wataongea kwa kuitetea nchi yao siyo kuzomeazomea.
Mheshimiwa Naibu Spika, zamani tulikuwa na vyuo vya ualimu ambavyo vilikuwa vinasimamiwa na jeshi nikitolea mfano ya Monduli, Morogoro TC na Tabora Boys. Vyuo vile vilikuwa vinatoa walimu wenye nidhamu nzuri na wenye uchungu na nchi yao. Kama kuna uwezekano utaratibu ule urudishwe ili tuendelee kupata Wanajeshi ambao wanakuwa na fani tofauti. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, siwezi kunyamaza kimya bila kusemea suala la uchaguzi wa Zanzibar. Tunakubali wote kwamba Amiri Jeshi Mkuu alisema, tena matangazo yalitoka kwenye televisheni, redio na magazeti kwamba yeye kama Amiri Jeshi Mkuu ana wajibu wa kulinda usalama Tanzania hii katika mkoa wowote siyo Dar es Salaam, Pemba au Mwanza na alimalizia kwa kusema atakayefanya fyokofyoko nitamshughulikia. Ukiona mtu analalamika kama alifanya fyokofyoko anashughulikiwa. Kwa hiyo, nampongeza sana Mheshimiwa Rais kwa kuonesha, kama angesema halafu wakanyamaza wangedharau wakasema amesema mbona hajafanya lolote, amesema na hawajathubutu kufanya fyokofyoko ndiyo maana wamenyamaza na kama watafanya fyokofyoko, Amiri Jeshi Mkuu aendelee kufanya kazi yake, ndiyo tutaendelea kuheshimiana. (Makofi)
Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee zaidi katika suala zima la mafunzo ya kijeshi kwa vyama vya kisiasa. Kumekuwa na utaratibu wa baadhi ya vyama vya kisiasa kutengeneza makundi ya kijeshi kwa kujifanya kwamba wanalinda wakati wa kampeni au kulinda kura zao. Naomba jeshi lifanye kazi ya ziada, Mheshimiwa Waziri alisimamie, yapo makundi yanayojiita mazombe, wenyewe wanayajua huko ndiyo maana kila saa wanayataja, kuna makundi yanajiita blue guard yapo huko, yanafanya vituko kusingizia vyama vya siasa. Naomba Mheshimiwa Waziri yale…
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Green guard umetaja wewe sijataja mimi. Kwa hiyo, ninachoomba yale makundi yote yanayoendesha mafunzo ya kijeshi kwa kusingizia vyama wayadhibiti kwa sababu hayo ndiyo yanayotuletea fujo katika nchi yetu na kusababisha makundi ya wahalifu katika mitaa yetu.
Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na kusema hayo, naunga mkono hoja kwa asilimia 100 na wale waliobana sasa wameachia. Ahsante.
NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Malembeka wakati ukichangia, kuna tuhuma hapa umezitoa kuhusu ukabila jeshini. Kwa mujibu wa Kanuni ya 72(1) na Kanuni ya 64(1)(a), naomba ufute hayo maneno halafu tuendelee. (Makofi)
MHE. ANGELINA A. MALEMBEKA: Mheshimiwa Naibu Spika, nilitolea mfano na nafuta kauli hizo.