Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Rashid Ali Abdallah

Sex

Male

Party

CUF

Constituent

Tumbe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwanza sina budi kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha leo hii kusimama hapa, lakini pia nikushukuru wewe kwa kunipa nafasi hii.
Mheshimiwa Spika, Wabunge wengi ambao wamechangia katika Wizara hii walionesha umuhimu wa Wizara hii ya Afya na umuhimu wenyewe ni kuhakikisha kwamba Wizara hii ndiyo yenye jukumu la kuokoa maisha ya Watanzania. Sielewi kwamba Wizara hii inaona umuhimu hasa wa kuokoa maisha ya Watanzania na nasema hivi kutokana na kuangalia kwa mfano Hospitali yetu ya Taifa ya Muhimbili jinsi gani inavyopangiwa bajeti zake.
Mheshimiwa Spika, nitataja miaka mitatu ya nyuma; kuanzia mwaka 2013/2014 hospitali hii ya Taifa ya Muhimbili iliomba shilingi 84,991,000,000 na Bunge likapitisha shilingi 5,074,000,000, lakini Serikali ilitoa shilingi 2,184,000,000. Mwaka ulioendelea 2014/2015, wenyewe Muhimbili waliomba shilingi 113,025,000,000 Bunge likapitisha shilingi bilioni 3.8 na Serikali ikapitisha shilingi bilioni 1.29. Mwaka 215/2016, Muhimbili iliomba shilingi bilioni 118,993,000,000, Bunge lilipitisha shilingi 1,694,000,000 na hatimaye Serikali ikatoa nusu bilioni yaani shilingi milioni 553.
Mheshimiwa Spika, katika hali hii hospitali ambayo ni tegemeo kubwa la Taifa kila mwaka kushuka kwa bajeti yenyewe inadhoofisha huduma za matibabu kwa Wizara hii. Ukiangalia hospitali hii inakusanya maduhuli yake, mapato yake ya ndani, lakini mapato haya ya ndani wanayatumia kwa kuwatibu wale wananchi ambao wana msamaha, kwa mfano wazee, watoto ambao wapo chini ya miaka mitano na walemavu.
Mheshimiwa Spika, kwa kuthibitisha hii ni kwamba, mnamo mwaka 2015 Hospitali ya Muhimbili imetumia bilioni 7.2 kwa wagonjwa 89,644 jambo ambalo limedhoofisha hospitali hii kuweza kufanya shughuli zao za muhimu ambazo walijipangia, wakati huo Serikali imechangia kiasi kidogo sana. Hii itaifanya Hospitali ya Muhimbili kushindwa tena kutoa huduma kwa watu wa aina hii. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, niende katika jengo la wagonjwa wa akili. Mheshimiwa jengo hili ni hatari sana, limefanywa kama vile gereza, kama vile halina maana. Jengo hili toka mwaka 1965 halijawahi kukarabatiwa, ni jengo ambalo halifai kukaa binadamu. Watu hawa ni wagonjwa, wametupwa kabisa na Wizara wamewasahau. Nataka Mheshimiwa Waziri ahakikishe jengo hili analifanyia ukarabati ili hawa wagonjwa ambao wapo katika jengo hili na wale watumishi wawe kama binadamu na wafanye kazi vizuri. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, tukija katika Taasisi ya Upasuaji wa Moyo. Taasisi hii ni muhimu sana inaokoa fedha za kigeni. Ina vyumba viwili tu ambavyo vimejaa kabisa wapasuaji. Mheshimiwa katika hotuba yake, ukurasa wa 43, amesema kwamba: “Wizara itajengea uwezo Taasisi kwa kuweka vifaa ili chumba cha tatu kianze kufanya kazi.”
Mheshimiwa Spika, chumba hiki kinahitaji dola milioni mbili ambayo ni sawasawa na bilioni 4.28. Wizara hii imepangiwa bajeti kiasi ambacho kinasikitisha, ni kiasi gani Waziri atatuhakikishia kwamba chumba hiki cha tatu kinafanya kazi ili kuweza kuokoa fedha za kigeni na kuingiza fedha za kigeni. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije katika hospitali ya Ocean Road. Hospitali hii ni hatari sana, ni hospitali ambayo imepewa fedha shilingi milioni 399 kuweza kutoa huduma kwa wagonjwa, lakini wastani wa matibabu kwa mgonjwa mmoja kwa chemotherapy ni shilingi milioni moja hadi milioni mbili. Wagonjwa ambao wanaweza kutibiwa kwa fedha hizi ambazo zimetolewa ni wagonjwa takribani 200 mpaka 400, lakini angalia wagonjwa waliopokelewa kipindi hiki ni wagonjwa 3,512, hapa kuna ongezeko la wagonjwa 3100…
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Kuna ongezeko la wagonjwa 3,100, hawana dawa, wagonjwa wa saratani, gonjwa la hatari, hawana dawa, waende wapi au wakatibiwe na nani? Serikali iangalie suala hili vizuri otherwise inasababisha kifo, pale kila saa moja anapita maiti. Nataka mtu aende pale, achukue muda wake, kila saa moja maiti inapita. Hospitali ya Ocean Road lazima iangaliwe vizuri.
Mheshimiwa Spika, pale kuna mkataba wa kujenga lile jengo la Shirika la Atomiki Duniani, lipo pale, wameshamaliza, bado kukamilisha matengenezo, Serikali imeshindwa kabisa kutoa fedha asilimia 74. Mashine moja ambayo inahitajika pale ni shilingi bilioni nane, wanataka shilingi bilioni 48 ili ziweze kuondolewa zile mashine mbovu na kuwekwa mashine nyingine mpya, Serikali imeshindwa na hawa watu wamevunjika moyo kabisa. Hii inaleta picha gani kwa Serikali?
Mheshimiwa Spika, naomba Waziri anijibu, jengo lile na mashine zile zitapatikana lini kwa sababu hawa tayari wameshavunja mkataba na fedha inayohitajika ni shilingi bilioni 48 kuweza kununua mashine hizi. Ni lini mtaweza kununua mashine hizi ili kuondosha vifo pale vinavyotokea bila sababu yoyote. (Makofi)
Mheshimiwa Spika, nije kwenye vifo. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumza vifo, vinasikitisha sana, tunapoteza nguvu kazi nyingi, akinamama na watoto, sitaki nielezee idadi, nataka nijue mwaka 2010 Serikali ya Tanzania iliingia katika mkataba katika nchi 260 za kuweza kutoa huduma bora kuanzia asilimia 28 mpaka asilimia 60 ifikapo mwaka 2015. Katika huduma hizo ni kuhakikisha vituo vyote vya afya vinapata mashine ya upasuaji na kupata damu bora ambayo ni salama. Pia kuhakikisha kwamba inaokoa akinamama milioni 16 ifikapo mwaka 2015, kama hiyo haitoshi ni kuokoa watoto ambao wanakufa milioni 120, ifikapo mwaka 2015.
Mheshimiwa Spika, mwaka 2015 umepita, tunataka tupate maelezo, wamewaokoa akinamama wangapi kwa mujibu wa mkataba ule uliowekwa mwaka 2010, ni watoto wangapi wamewaokoa na ni vituo vingapi wamesambaza mashine za upasuaji pamoja na damu salama ili kuokoa maisha haya?
Mheshimiwa Spika, nirudi kwenye kero za madaktari wetu. Madaktari walifanya mgomo mkubwa na wakawa na changamoto nyingi, wanatakiwa stahili zao na mishahara yao, lakini hadi sasa tunaona kimya. Hawa hawajakaa kimya, wanaangalia utendaji wa Serikali, nadhani kuna siku watafumuka. Nataka Serikali kupitia Waziri itueleze stahili gani za madaktari wetu ambazo mpaka sasa wamezitekeleza katika maombi yao yaliyopita. Inasemekana kwamba madaktari wanaondoka wanakwenda nchi kama sikosei Berlin na kule wanapata mshahara kuanzia shilingi milioni tatu hadi milioni tisa za Tanzania…
SPIKA: Ya pili hiyo, Mheshimiwa Rashid.
MHE. RASHID ALI ABDALLAH: Ahsante sana Mheshimiwa.