Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Issa Ally Mchungahela

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Lulindi

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana awali ya yote nimshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehma kwa kuniweka hai mpaka hivi leo na watu wa Lulindi wako wakinisikiliza kutaka kuwaongelea jambo lao.

Mheshimiwa Mwenyekiti,kama muongeaji aliyepita natamani kuishauri Serikali kama itawapendeza basi waweze kuchukua na hiki ninachokusudia kuwashauri kukiweka katika mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimejielekeza sana kwenye kilimo kama vile ambavyo wenzangu waliotangulia lakini nimejielekeza katika muonekano mmoja kwamba kama tutahangaika vizuri tu na kilimo biashara bila shaka matatizo makubwa ya kiuchumi lakini pia ya ajira yanaweza yakawa yamepungua kwa kiasi kikubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niongelee eneo moja eneo ambalo linahusu maeneo ninayoishi kule kwetu Mtwara kwa maana ya Lulindi korosho. Korosho ni kitu ambacho inailetea pato nchi hii pesa nyingi sana nashindwa kuelewa kigugumizi kiko wapi kwamba Serikali bado haiweki juhudi ya kutosha kuhakikisha kwamba korosho zinapatikana kama vile ambavyo wao wanavyotarajia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, makusudio kwa mfano ya bajeti hii inayokaribia kuja Serikali ilijaribu kuelekeza kwamba korosho zipatikane takriban tani laki saba. Sasa tani laki saba ndugu zangu haziwezi kuja hivi hivi kwa maneno lazima tuwe tumejipanga vizuri na kwenye Mpango humu sioni wapi kwamba kuna kitu cha namna hii kitakachotuwezesha zao la korosho zipatikane tani laki saba, na kwa nini tani laki saba kwa sababu mpaka sasa hivi ambapo ni kiasi cha korosho kinapungua hakifiki hata tani laki tatu Serikali inapata pato la dollar takriban milioni 500 ambayo ni trilioni 1.3 kwa maana kama kweli lengo la tani 700,000 litafikiwa ina maana hapa ni zaidi ya dollar milioni moja ni kiasi cha trilioni tatu na zaidi mnaweza mkaona kwa jinsi gani hapa suala la kupata pesa ya kuingiza kwenye uchumi ilivyokuwa nyingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama sisi hii dollar milioni 500 plus ambayo ni trilioni 1.3 mmeona athari yake kwenye uchumi nchi nzima kila mahali sasa hivi watu wanahangaika tunajenga kule tunajenga kule uchumi unaingia pale uchumi unaingia pale. Mnaweza mkaona hii dollar milioni moja ambayo Serikali ina i-target kupitia korosho tani laki saba inaweza ikawa ina athari kiasi gani? Sasa kwa hali hiyo hapa panahitajika kuwekeza kitu kidogo tu na chenyewe ni kitu kama hivi kwangu panahitajika kuingiza pembejeo za kutosha lakini mapema kabisa tena ambazo haziwezi zikazidi hata bilioni 100. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini halikadhalika kuwezesha jambo hilo pia liende vizuri tunahitaji pia ile barabara ya kutoka Mtwara kupitia Nanyamba kwenda Newala, kwenda Lulindi kwenda Masasi kwenda Nachingwea ambayo ni takriban kama bilioni 300 hivi. Hivi jamani hapa ukichukua hapo makadirio inaweza ikawa kama bilioni 400, bilioni 400 ukiwekeza ukapata takribani trilioni tatu hivyo jamani tunahitaji kitu gani? Shida ninayoona ninaona kwamba sisi tunafikiria sana vitu vikubwa mno baada ya kufikiria vitu vidogo vidogo ambavyo viko pale wala havihitaji kazi kubwa kuvitekeleza vikatupatia pesa. Kama tungekwenda kwa mtindo huu tukaenda kwenye eneo jingine la kilimo tukafikiria katika mtizamo huu bila shaka suala la kilimo kuwa uti wa mgongo lingekuwa lina maana sana na lenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini baada ya kutoa ushauri huo nataka niipongeze Serikali kwa kazi yake kubwa ambayo imejaribu kuionyesha katika maeneo yale muhimu ambayo yanaweza pia kusaidia kwa namna moja au nyingine kuleta matokeo ya uchumi ya haraka. Maeneo mengi ambayo watu wengi wameshaanza kuyasema huko mwanzo kama vile uwekezaji wa reli ya Standard Gauge ninaiomba Serikali kusisitiza kwamba hili suala la Standard Gauge katika eneo letu la Mtwara kutoka bandarini kwenda Mbamba Bay nakupitia katika maeneo yale mawili ya Mchuchuma na Liganga yaani tunasema kwenye matawi itawezesha sana bandari ya Mtwara kutumika na kuingiza uchumi mkubwa katika nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu gani sasa hivi tumetumia pale takriban bilioni 157 lakini ni kama zimelala tu bado hakujawa na kitu chochote cha maana cha kuifanya bandari ile ichangie kikamilifu kama vile tunavyotarajia na tunaweza tukaitumia bandari ile katika maeneo yote yale kule ya nchi za kusini kama vile Mozambique ambavyo kwa sasa hivi wanashida kwa sababu hawatumii bandari yao kutokana na hali yao ya matatizo ya migogoro yao lakini halikadhalika Malawi na Zambia wanaweza wakaitumia vizuri sana bandari ile.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali itumie nguvu nyingi sana kuhakikisha bandari ile inatumika kikamilifu, mambo haya yasiishie kwenye karatasi tu tumekuwa wepesi sana wa kuongea lakini kuthubutu kufanya maamuzi ya kutekeleza ni wagumu sana nashindwa kuelewa sababu za msingi sijui ni kwanini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti hizi tunazokaa hapa mara nyingi sana wengi wanaona kama ni sehemu tu ya kuja kuigiza tunakaa tunachangia na kutoka tukishatoka hapa utekelezaji unakuwa mgumu sana unakuta kiongozi ambaye muhusika msimamizi wa Wizara fulani unavyojaribu kumfuata kutaka kufuata utekelezaji wa jambo fulani ambalo mmelizungumza pale halitekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Mfano nataka nizungumzie suala la mawasiliano kule kwangu. Bajeti hii iliyoko sasa hivi nilihakikishiwa kwamba takriban kata nane katika kata 16 maana yake kata 16 katika jimbo langu hazina mawasiliano kabisa ya simu wala redio. Kwa hiyo nilihakikishiwa takriban kata nane kwamba nitapewa mawasiliano na sababu kubwa ni nini? Kwamba lile Jimbo liko mpakani kabisa wa Mozambique mpaka ambao una shida ndugu zangu na tujue kabisa mawasiliano ni njia pia mojawapo ya ulinzi ni ulinzi namba moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa lakini mpaka sasa hivi hakuna chochote kinachofanyika kila ukiuliza wahusika hawana hata majibu yaani hata hawaelewi kitu gani wanaweza wakakwambia bwana kweli Mheshimiwa tulipanga hivyo lakini hili jambo halijatekelezwa kwa sababu gani sababu hazieleweki nashindwa kuelewa sasa hapa Bungeni tumekuja kuigiza au kweli tumekuja kufanya mambo kwa maana ya manufaa ya wananchi wetu?

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mchungahela mwaka haujaisha.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Sawa lakini angalau hata dalili zionekane.

MWENYEKITI: Najua hasira yako lakini mwaka wa fedha bado haujaisha

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli naelewa lakini angalau dalili zionekane jambo tendering ifanyike uone kwamba kuna tender imefanyika hapa kwa ajili ya huu mradi hakuna, ushaona kuna sehemu nyingine kwa mfano kule kumejengwa mnara ule mnara ni mfupi yaani unakaribia yaani kama ufupi wangu ulivyo. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa unashindwa kuelewa hivi mnara…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mchungahela muda hauko upande wako.

MHE. ISSA A. MCHUNGAHELA: Mheshimiwa Mwenyekiti, haya ahsante naomba kuunga mkono hoja lakini nawaomba wahusika watekeleze haya yote ninayojaribu kuwakumbusha; ahsante. (Makofi)