Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Kwagilwa Reuben Nhamanilo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Handeni Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nichukue nafasi hii nikushukuru sana kwa kunipa fursa ya kuchangia Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo mchango wangu ni mfupi sana. Ukurasa wa 116 wa Mapendekezo yaliyosomwa, yaliyoletwa hapa na Serikali, kipengele cha 3.3.7.3 - Ubia kati ya Sekta Binafsi na Sekta ya Umma; pana miradi pale imeorodheshwa kama 11. Sisi kwenye Taarifa ya Kamati tumeeleza jinsi ambavyo miradi hii ya PPP imeorodheshwa kwa miaka na miaka bila kutekelezwa na matokeo yake kwenye Mpango huu tunaotarajia kwenda kuwa nao, Serikali imeongeza mradi mwingine mmoja mpya. Mradi huu ndiyo umenisukuma nizungumzie eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu, kipengele K, unasema: “kuendeleza upembuzi yakinifu wa mradi wa kusimika boya la kuegesha meli za mafuta katika Bandari za Dar es Salaam na Bandari za Tanga.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu una conflict of interest na maslahi ya nchi, kuuweka kwenye utekelezaji wa kutumia sekta binafsi na kwa maneno rahisi, kuandaa huu mradi kwa kumpa mtu binafsi aufanye, kwa maneno rahisi kabisa naweza kusema hii ni hujuma kwa nchi yetu na ni jambo halikubaliki. Tusipoangalia, tunakwenda kutengeneza TICTS nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, iko hivi, mradi huu wa kutengeneza boya la kuegesha meli za mafuta, unagusa bandari, tena bandari mbili. Bandari ni uchumi… (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kwagilwa tuwekee vizuri ili uende tu vizuri, yaani kwamba Serikali hapa imeweka katika orodha ya PPP. Kwa hiyo, ni orodha ya watu binafsi na Serikali yenyewe. Nawe unasema kwamba ni binafsi peke yake, labda tuwekee vizuri tu.

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nasema hivyo kwa sababu mradi upo kwenye upembuzi yakinifu, inamaanisha mradi haujaanza kujengwa, ina maana unaikaribisha Sekta Binafsi au mtu binafsi ashiriki kuanzia kwenye kujenga hilo boya na kwa lugha nyingine kujenga kipande cha bandari; umkabidhi kipande cha bandari ili ajenge gati kwa ajili ya meli kubwa za mafuta na gesi kuja kushusha pale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii inagusa habari ya usalama wa nchi, lakini inagusa habari ya uchumi wa nchi, vile vile bandari ni lango la nchi yetu. Kumpa mtu binafsi au kumshirikisha kwenye hizi hatua za awali za kujenga, kumpa miundombinu ile ya bandari, siyo jambo sahihi sana kwa mustakabali wa Taifa letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaelezea jambo hili kwa sababu ukiongelea meli kubwa za mafuta unaongelea pia na meli kubwa za gesi. Sisi tunazalisha gesi. Tumetoa gesi, tumeshaichimba, tumewekeza billions of money kwenye gesi na kila mwaka shirika letu linaloshughulika na habari za gesi na mafuta linatumia bilioni 50 kila mwaka kwa ajili ya utafiti kwenye mafuta na gesi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kana kwamba hiyo haitoshi, tayari tumeshakopa Benki ya Exim, Dola za Kimarekani bilioni 1.2 kuitoa gesi kutoka Madimba pale Mtwara, kuitoa Songosongo Lindi, kupitia Somanga Fungu, tumeifikisha Pwani na iko Dar es Salaam. Sasa gesi yetu ile ni natural gas. Tumeshaifikisha Dar es Salaam, Serikali haina juhudi yoyote inayofanya ya kuisambaza gesi kwa wateja. Imeshafika Dar es Salaam, lakini badala yake imerukia inataka impe mtu binafsi aingize gesi nchini. Hiki kitu hakiko sawa. Hakiko sawa kwa sababu huyu mtu au hii sekta binafsi ikipewa kuwaruhusu…

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa.

T A A R I F A

MHE. OMARI M. KIGUA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimpe taarifa mzungumzaji, Mheshimiwa Reuben, Mbunge wa Handeni Mjini, kwamba anapoendelea kushangaa hilo ashangae pia kwamba gesi hiyo ambayo inatoka Mtwara kuja mpaka Dar es Salaam inatumika kwa asilimia 20 tu. Maana yake bado gesi yetu ya ndani haijapata soko. Ahsante.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Kwagilwa, unaipokea taarifa hiyo?

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipokea taarifa hii, tena naipokea kwa uzito sana, hasa ukizingatia kwamba taarifa hii imetolewa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuwe wazalendo kwenye mambo haya. Mambo haya kwa sababu yanashirikisha mikataba na experience inaonesha kwamba tumekuwa tukifanya vibaya sana kwenye mambo ya mikataba, hasa inayogusa rasilimali kubwa kama hii. Nashauri hapa tusiingie kwenye huu mtego. Tulishaingia huko tukafanya mambo ya hovyo na ya ajabu ambayo hayawezi kuzungumzika, tusirudi huko. Tusirudi huko. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi huu, upembuzi yakinifu uendelee na ukikamilika ufanywe na Serikali. Kwa hiyo naishauri Serikali iondoe huu mradi kwenye hii orodha ya miradi inayopanga kuitekeleza kama PPP. Ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumewashauri hili kwenye Kamati, tulifikiri wameelewa lakini wamekuja nalo kwenye floor huku na ndiyo maana na sisi tumeona tusione haya tuje tuseme hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka niliseme ni kwamba katika Mpango huu uliopita kwa maana…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. KWAGILWA R. NHAMANILO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana, mchango huu unatosha. Ahsante. (Makofi)