Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Venant Daud Protas

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Igalula

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia angalau dakika tano nami nitoe mchango wangu katika Mpango huu wa Serikali. Awali ya yote nianze kumshukuru Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kupambana kuhakikisha wananchi wetu wanapata huduma nzuri. Fedha hizi zilizoletwa katika historia nilikuwa naona mikopo mingi inakwenda kwenye miradi ya Kitaifa, lakini mkopo huu umekwenda kuwagusa wananchi wa chini zaidi hasa wa vijijini. Tunamshukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na pongezi nyingi, tunakwenda kujenga madarasa, shule na mbiundombinu mbalimbali ya afya; lakini tujiandae na mambo mengine ambayo yatajitokeza hususan kwa watumishi wetu. Kwa hiyo, naiomba Serikali katika mpango wao ambao utakuja kwenye bajeti ijayo, iangalie namna gani ya kutusaidia kuongeza watumishi hasa katika Sekta ya Elimu. Madarasa ni mengi, idadi ya wanafunzi ni kubwa lakini idadi ya walimu ni ndogo. Kwa hiyo, naiomba Serikali ije na mpango huo wa kuweza kuongeza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, niende kwenye kuchangia Mpango. Serikali yetu katika Mpango wake ambao ulikuja mwaka 2020, wa miaka mitano, ilituelekeza itakwenda kujikita kwenye Sekta ya Kilimo, nami wananchi wangu wengi ni wakulima. Mpaka sasa hivi, Serikali imekaa kimya, haijatoa mwongozo wa nini kinakwenda kutokea juu ya ongezeko la bei ya mbolea. Tumekuwa na kigugumizi, hatujapata bei elekezi mbolea ni shilingi ngapi? Tunakwenda kwenye msimu ambapo mvua kwenye baadhi ya mikoa imeshaanza. Leo hii tunapokea simu kutoka kwa wananchi, wanauliza nini kilichotokea? Nasi hatuna majibu.

Naiomba Serikali isimame mbele, itoe mwelekeo na dira kwa wakulima kwa sababu msimu umeshaanza. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mambo mbalimbali ya kuisaidia Sekta ya Kilimo, naishukuru Wizara ya Kilimo inaendelea kupambana, lakini kuna mpango walikujanao wa kuwakopesha wakulima matrekta. Katika mkoa wangu na Jimbo langu wapo wananchi ambao walikopa. Ile mikopo ilikuwa ni kichefuchefu. Yamekwenda matrekta hayalimi hata nusu eka kwa siku, lakini wamekwenda kukopeshwa, na wale waliowakopesha kupitia Wizara ya Kilimo hawafuatilii changamoto gani wanazozipata kwenye kukusanya madeni. Wamekwenda TAKUKURU, eti TAKUKURU wakakusanye madeni. Sijawaji kuona aliyekopesha ni mwingine, anayekwenda kukusanya ni chombo kingine cha Serikali tena kikubwa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba Serikali, yale matrekta ambayo yalikuja kule, wananchi wameyapaki. Agizeni vyombo vyenu mkachunguze.

MWENYEKITI: Aina gani Mheshimiwa, hayo yanayolipa nusu eka kwa wiki.

MHE. VENANT D. PROTAS: Mheshimiwa Mwenyekiti, yanaitwa Ursus yametoka NDC. Yale matrekta nusu eka hayalimi. Kwa hiyo, naiomba Serikali, wananchi wangu wameyapaki, hawayatumii tena, wanahitaji wavunje mkataba. Wale jamaa wanapigiwa simu hawapokei. Nendeni mkachukue trekta zenu, mkataba uishe. TAKUKURU hawataki kuwaona huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ili tusaidie wakulima wetu katika maeneo yetu, lazima kama Serikali tuone namna gani ya kuweza kuwasaidia hususan kuwaletea zana bora za kilimo. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)