Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Josephine Johnson Genzabuke

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JOSEPHINE J. GENZABUKE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nami niweze kuchangia hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwa dhati kabisa nimpongeze Mheshimiwa Rais, Mama yetu Mpenzi Mama Samia Suluhu kwa kazi kubwa anayoifanya kwa ajili ya watanzania. Lakini nimpongeze sana kwa kuweza kutuletea chanjo ya UVIKO-19 na kututoa woga tukaweza kuchanja. Mwenyewe tayari nimeshachanja mwanzo nilikuwa na wasiwasi, lakini sasa hivi nimechanja, lakini na wewe nakushukuru kwa kutuhamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niendelee kuwashukuru vilevile wasaidizi wake; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Mpango, Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya wanapita huku na kule kwenda kuwahamasisha watanzania na kuangalia shughuli zinazofanywa nchi nzima nawapongeza sana na Mawaziri pia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimpongeze sana Mheshimiwa Rais kwa fedha nyingi ambazo amepeleka Tanzania nzima fedha kwa ajili ya barabara kila Jimbo, fedha kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya na fedha nyingi kwa ajili ya ujenzi wa madarasa. Nampongeza sana Mheshimiwa Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba sasa madarasa yanajengwa na nyumba za walimu nazo ziweze kujengwa na niipongeze Serikali kwa kuwa tayari ilishaanza kuajiri walimu, iendelee kuajiri walimu ili madarasa yanapojengwa, nyumba za walimu zinapopatikana na walimu vilevile waweze kuwa wengi na waweze kufanyakazi ya kufundisha vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, natokea maeneo ya wakulima na wapiga kura wangu ni wakulima ukiangalia wakulima wengi wamejiajiri kwenye kilimo wakiwemo wanawake na vijana. Nilikuwa naomba Serikali iongeze bajeti kwa ajili ya kilimo, kwa mfano; ukiangalia mwaka tumekumbana na changamoto ya mbolea kupanda na kufikia mfuko mmoja shilingi 120,000. Ninaomba tuweze kuita wawekezaji waweze kujenga viwanda hatimaye mbolea iweze kushuka bei na wakulima wetu waweze kulima kilimo chenye tija. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie kuhusu umeme; ipo mikoa ambayo haijaunganishwa kwenye grid ya Taifa, Mkoa wa Kagera, Mkoa wa Kigoma, Mkoa wa Katavi na Mkoa wa Rukwa. Nilikuwa naomba mikoa hiyo iweze kupewa kipaumbele na yenyewe iweze kuunganishwa kwenye grid ya Taifa, kwa sababu ukiwaunganisha kwenye grid ya Taifa mikoa hiyo wawekezaji wataweza kwenda kuwekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mfano; Mheshimiwa Waziri Mkuu kila siku unakuja Kigoma kuja kuhamasisha kilimo cha mchikichi, lakini kama hakutakuwepo na umeme wa grid ya Taifa wananchi wakizalisha michikichi watakosa kiwanda. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo nilikuwa naomba kwa heshima na unyenyekevu mkubwa kabisa umeme wa grid ya Taifa uweze kufika kwenye mikoa hiyo minne niliyoitaja ikiwemo na Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tayari upo mradi ambao ulishaanza kuanzia Tabora, Uvinza mradi huo unaendelea naomba Serikali iongeze pesa ili mradi huo uweze kukamilika. Mheshimiwa Makamu wa Rais alipokuja mwezi wa nane alielekeza mradi huo uweze kukamilika Oktoba 2021. Kwa hiyo, naiomba Serikali katika Mpango tunao upanga sasa ipeleke pesa kusudi umeme wa grid ya Taifa uweze kufika Kigoma hatimaye wawekezaji waje kuwekeza Kigoma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini si hivyo tu hata hospitali zitaweze kunufaika kwa sababu kwa sasa hivi si wa uhakika hatuwezi kuwa na vifaa kama MRI, ST-Scan. X-Ray na Ultra Sound umeme wa uhakika ukiwepo vifaa hivyo vitakuja na wananchi wataweza kurahisishiwa maisha kwa sababu sasa hivi wanafuata matibabu wengine wanaenda Mwanza, wengine wanaenda Dar es Salaam na kutokana na kipato chao kidogo wengine wanapoteza maisha. Kwa hiyo naendelea kuomba umeme wa grid ya Taifa uletwe Kigoma na maeneo mengine mikoa ile ambayo sikuweza kuitaja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miundombinu, naendelea kuishukuru Serikali ya CCM katika Mkoa wetu wa Kigoma ujenzi wa barabara wa kilometa 260 wa kutoka Nyakanazi – Kibondo – Kasulu mpaka Buhigwe unaendelea. Tunaomba pesa zipelekwe ili barabara hiyo iweze kukamilika barabara ambayo inaunganisha mikoa, lakini vilevile inatuunganisha na nchi za jirani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho kabisa kwenye sura ya pili kuhusu hali ya uchumi; nikupongeze wewe mwenyewe kwa sababu kwanza umeendelea kuwaelimisha wananchi na kutuelimisha sisi Wabunge kwa kusema kwamba zipo sheria ambazo wakati mwingine zinahitajika kurudi Bungeni ili zifanyiwe marekebisho kusudi ziweze kuwasaidia watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bandari yetu ya Dar es Salaam inapitisha mizigo mingi sana, mizigo hiyo inapita inaenda nchi za jirani na mizigo hiyo inarudishwa tena kuja kuuzwa ndani ya nchi yetu. Nilikuwa ninaomba Mheshimiwa Waziri aangalie kipengele hicho ambacho kitawasaidia wazawa waweze kufanya biashara katika nchi yao. Tofauti na sasa hivi mizigo inapitishwa nchini mwetu inaenda nchi za jirani halafu inakuja kuuzwa nchini kwetu. Kwa hiyo, wazawa hawawezi kushindana na wale ambao wamepitisha mizigo nchini kwetu wanaenda kuuza kwa bei ya chini halafu sisi tunauza kwa bei ya juu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo ninakushukuru sana, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)