Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Deodatus Philip Mwanyika

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Njombe Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. DEO P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia katika Mpango na Mapendekezo ya Mpango ulio mbele yetu wa mwaka 2022/2023.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa nijikite kwenye maeneo mawili; eneo moja ni eneo la uwekezaji kwa maana ya Mradi wa Liganga na Mchuchuma na muda ukiruhusu niweze kuangalia Sekta ya Kilimo kama wenzangu ambavyo wameangalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango huu unajaribu kujikita kutoa msingi wa maandalizi ya Mpango wa Maendeleo wa 2022/2023 na umeainisha maeneo muhimu ya vipaumbele. Katika maeneo haya kuna maeneo ya miradi ya kielelezo. Kwenye maeneo haya kuna eneo la Liganga na Mchuchuma; nipende kusema na mwenzangu Mbunge wa Ludewa ameliongelea, lakini mimi nitaliongelea kwenye angle tofauti kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashindwa kuelewa kinachoelezwa katika Mpango, kuhusiana na mradi huu ni kwamba, majadiliano yanaendelea na tunakubali, lakini tuishauri Serikali kwamba mradi huu ni mradi mkubwa, ni mradi ambao unaweza ukawa game changer. Leo nataka nitoe takwimu kidogo tu hapo baadaye za kwa nini Mpango unaokuja ni lazima uzingatie kuona matayarisho ya Mradi huu wa Liganga na Mchuchuma kwa maana ya makaa pamoja na chuma uweze kuanza kuonyeshwa na kuandaliwa wakati majadiliano yanaendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, majadiliano hayo ambayo hayaishi hatuelewi ni majadiliano gani. Tunaelewa kwamba pengine kuna ugumu kwenye kujadiliana, lakini tufike mahali maamuzi yafanyike na option za uwekezaji katika sekta hizi za madini kama chuma ni muhimu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wachumi wanasema kuna gharama au kuna hasara ya kutofanya jambo fulani kwa wakati fulani, wao kitaalamu wanaita opportunity cost. Sasa tukiangalia sasa hivi bei ya chuma ndani ya miezi 24 imefika dola za Kimarekani kwa tani 400 ni ongezeko kubwa la asilimia 200. Wachina peke yao ndiyo wanao-dominate soko hili la chuma kwa sasa. Wanazalisha karibu asilimia 56.5 ya chuma chote duniani. Afrika peke yetu tunazalisha kama asilimia 17, Tanzania ni sifuri, lakini tuna chuma hapa na tuna resource hapa kubwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nipende kusema kuna research imefanyika na Institute ya Global for Development Studies ya Boston University ambayo inaonesha katika kipindi cha 2008 mpaka 2019 Wachina peke yao wametoa mikopo ya financing ya maendeleo duniani ya karibu dola za Kimarekani bilioni 462. Ndani ya hizo dola bilioni 462 asilimia 80 imeenda kwenye miradi ya infrastructure, maana yake unaongelea bandari, reli, madaraja na kadhalika. Afrika peke yetu tumepata dola bilioni 106 katika hizo dola bilioni 462.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa ninachotaka kusema ni nini? Hizo dola bilioni 106 ni karibu trilioni 230 za Kitanzania. Hoja hapa ambayo Mpango lazima uangalie ni kwamba tuna kila sababu ya ku-take advantage ya uchumi wa makaa ya mawe na chuma sasa hivi ili tuweze ku-benefit huko tunakokwenda. Kama Tanzania peke yetu tungeweza kupata, maana yake katika hii 80 percent infrastructure na Afrika ni dola bilioni 106, sisi tuna chuma, kama tungekuwa tumeanza uzalishaji hata tukapata asilimia 50 tu ya hiyo biashara ya ujenzi wa infrastructure katika maeneo ambayo yanahitaji chuma sana madaraja, SGR, barabara, ports, zote zinataka chuma, tungepata asilimia 20 tu ya hiyo biashara ya kuzalisha hiyo chuma, bajeti yetu nzima yote trilioni 39 ingeweza kutoka katika biashara ya chuma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ipo haja tuone kwamba tuna haja na tuna kila sababu ya kuhakikisha haya majadiliano yanafika mwisho ili tufanye huu uwekezaji katika hili eneo la chuma pamoja na makaa ya mawe. Tuliangalie vile vile pengine nje ya box, kama tunaona maana yake hapa hatuhitaji pesa ya Serikali, pesa ya uwekezaji kwenye maeneo haya ipo duniani na wawekezaji wapo duniani. Kama tuna mwekezaji ambaye hatuwezi kwenda naye anatuchelewesha, tujue kwamba hiyo opportunity cost inakula kwetu.

Mheshmiwa Mwenyekiti, kwa hiyo ningependa niombe sana sana Mpango huu, ukiangalia kwa mfano katika Mpango, matumizi ya mwaka jana katika robo ya kwanza hata wachukue robo mbili, matumizi ya Serikali kwenye maandalizi ya mradi huu huwezi kuamini wametumia shilingi za Kitanzania milioni 3.7, nadhani ni kuwalipa walinzi wanaolinda yale maeneo. Kwa hiyo ni kwamba hakuna uwekezaji wa aina yoyote kwenye eneo hilo na kwamba ni kama hatuoni umuhimu kwenye hii mradi huu wa kielelezo, ambao ni muhimu. Nchi yoyote ambayo ina chuma leo na ikaanza kuchimba itakuwa na bajeti nzuri, itakuwa na chanzo kikubwa sana cha mapato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuliongolea hilo, kwa hiyo nisema maandalizi ni pamoja na kuhakikisha kwamba hizo fidia zinalipwa kutengeneza hilo eneo ili mambo yakikamilika haya ya majadiliano, uwekezaji uanze, siyo tena tuanze kuhangaika kwamba kwenye bajeti hakuna compensation, hakuna hela za kulipa. Kwa hiyo Mpango ujaribu kuliangalia hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna masuala pia ya miundombinu, project hii ita entail vilevile kuendeleza SGR kutoka Mtwara mpaka Mbamba Bay mpaka kwenye Mchuchuma. Kwa kweli kwenye Mpango inaonyesha kwamba bado wanaendelea kufanya tathmini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba haya mambo yaharakishwe kwa sababu si lazima Serikali itumie pesa kujenga SGR, tufanye hii kitu tofauti na tulivyofanya kwenye central line, kuna watu wanaweza wakajenga kwa pesa zao tu-negotiate nao ili tuweze kunufaika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niongelee haraka haraka kilimo, wengi wameongelea, suala zima la tija katika kilimo tuliliongelea hapa na tumeliongelea muda mwingi kwamba tunahitaji kupata mbolea kwa wakati na mbolea ambayo ni affordable. Hali si nzuri wote tunaelewa, tunajua kwamba Serikali itakuja na maelezo hapa kabla Bunge halijaisha kutuambia kuhusu suala la mbolea. Hata hivyo, nipende kusema, tunashukuru Serikali imefanya jitihada za kuona namna gani itashusha bei ya mbolea au itawapa nafuu wakulima. Ukweli wa mambo ni kwamba bado hakuna nafuu, tuiombe Serikali na Kamati imejaribu kuongea na imesema ni vizuri Serikali ikaangalia uwezekano wa kutoa ruzuku katika suala hili la mbolea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kuongelea zao la parachichi, kwa sababu nalo ni chanzo kingine kizuri sana cha mapato. Zao la parachichi ukiangalia kidunia Watanzania tumezalisha kama asilimia 0.2 ya mazao yote ya parachichi duniani. Ukweli ni kwamba, Tanzania ndiyo nchi pekee yenye potential kubwa sana ya kuendelea kukamata soko la parachichi katika dunia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaweza tu kufanya hiyo iwapo tutahakikisha kwamba sasa hivi Serikali ina-invest katika kilimo kwa maana ya kuhakikisha kwamba wakulima wote kwenye masuala ya mbegu, ubora wa mbegu, yanaangaliwa kwa umakini sana, kwa nini? Kwa sababu unalima parachichi leo, unaanza kuzalisha baada ya miaka mitatu, lakini full production inaanza baada ya miaka saba. Kama mbegu tunazotumia hazina uhakika, hazina ubora tutafika kule mwisho hatuta-realize hayo tunayotaka kuyafanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niombe sana tulikuwa na promise ya Serikali ya kuweka mamlaka ya kusaidia…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Kengele ya pili.

MHE. DEODATUS P. MWANYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru na naomba niunge mkono hoja. (Makofi)