Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Eric James Shigongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Buchosa

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. ERIC J. SHIGONGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa nianze kwa kuunga mkono hoja na baada ya hapo nitoe shukrani nyingi sana kwa Serikali ya Awamu ya Sita, Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan kwa mambo ambayo ameyafanya kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa ajili ya miundombinu, niendelee tu kukumbusha kwamba, barabara ya kutoka Sengerema kuelekea Nyehunge - Buchosa bado inahitaji kutiwa angalao lami ili wananchi wa Buchosa nao waweze kuona lami kwa mara ya kwanza katika maisha yao. kwa hiyo, nilitaka tu kukumbusha hilo kabla sijaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya shukrani hizo nitazungumzia maeneo mawili. Eneo la kwanza kama walivyotangulia wenzangu nitazungumza juu ya kilimo cha nchi yetu na baada ya hapo nitazungumzia suala la uwezeshaji wa wazawa wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kilimo cha nchi yetu kama ambavyo tumetangulia kusikia kinaajiri watu asilimia 65. Mchango wa kilimo kwa Taifa letu kama ambavyo tumesikia wote ni asilimia 26.9 ya pato la Taifa. Hii ni dalili kabisa ya kwamba, kilimo chetu kinatoa mchango mkubwa sana kwa Taifa letu. Sasa nimeusoma mpango, nimepitia ndani, sijaona mahali popote ambapo wamezungumza juu ya taasisi zifuatazo: Sijasikia wamezungumza juu ya TANTRADE, sijasikia wamezungumza juu ya TIRDO, sijasikia wamezungumza juu ya TEMDO, CAMARTEC na SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini nazitaja hizi taasisi? Nazitaja kwa sababu ya mfano wa nchi kama Taiwan, ninapozungumzia suala la maendeleo ya kilimo huwa napenda sana kuchukua mfano wa nchi ya Taiwan. Watu wa Taiwan mwaka 1950 walifikia uamuzi ya kwamba baada ya vita ya pili ya dunia walime na wakaamua kulima sana na wakawa wana-export mazao kwa wingi sana kwenda nchi za nje, lakini baadae wakasema haifai kuendelea ku- export mazao ghafi, badala yake ni bora waanze kutengeneza bidhaa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, walichokifanya ndiyo hicho ambacho Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliki-copy na kukileta hapa nyumbani ya kwamba, tunalima halafu tunatengeneza bidhaa ndiyo tunazipeleka nje. Alipokuja hapa Mwalimu alikuja kuanza na taasisi ya kwanza ya Board of Internal Trade na baadaye akawa na Board of External Trade ambayo kwa sasa inaitwa TANTRADE ambayo kazi yake ni kutafuta masoko ya bidhaa mbalimbali. Kwa hiyo, tulikuwa tunaanzia sokoni kutafuta kwanza masoko halafu tukishapata masoko tunakuja hapa nyumbani tunawaambia sasa nyie watu wa Tanga mtalima katani, nyie watu wa Kilimanjaro mtalima kahawa, watu wa Mwanza mtalima pamba kwa sababu soko lipo, hilo ndilo lilikuwa likifanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo taasisi za utafiti kama TIRDO ilikuwa inafanya utafiti wa kutengeneza vifaa vya kiwandani, mashine za kiwandani kwa ajili ya kutengeneza bidhaa kutokana na kilimo tulichokuwa tunafanya. TEMDO walikuwa wanafanya pia na wenyewe utafiti na CAMARTEC wanatengeneza mashine za kutumia katika kilimo chetu huko vijijini. Sasa sijaona kiasi cha fedha ambacho kimetengwa kwa ajili ya taasisi hizi. Ndiyo ninataka kumkumbusha Mheshimiwa Waziri ni bora akalizingatia suala hili kwa sababu hatuwezi kunufaika na kilimo chetu kama tutaendelea tu ku-export raw mazao ambayo ni ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, jambo la muhimu sana ni kuhakikisha kwamba, tunatengeneza products na tunazi-export kwenda nje. Nilitaka kukumbusha kuhusiana na suala hilo ni la muhimu sana kwa ajili ya kilimo chetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kuzungumzia suala hilo nataka nizungumzie suala moja muhimu sana juu ya National Whisper, yaani mnong’ono wa Taifa. Sisi kama Taifa, kama Tanzania, tunanong’ona nini juu ya wafanyabiashara wetu? Tunanong’ona nini juu ya vijana wa Taifa hili? Tukiwa tumekaa peke yetu sisi wenyewe tunaongea nini juu ya maendeleo ya vijana wetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninasikitika tu ya kwamba, vijana wetu wa Tanzania walioko katika nchi hii hatuwapi kipaumbele kikubwa linapokuja suala la maendeleo ya Taifa lao. Nasema hivi kwa sababu, wote tunaona kwa macho na wote tunashuhudia kabisa kwamba, vijana wetu tunawapeleka shule, wanasoma, wanapata elimu, wakitoka shuleni wanakuwa hawana chakufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ombi langu kwa Mheshimiwa Waziri ni kuanza kufikiria namna ya kuanzisha mfuko wa ubunifu wa Taifa ambao utakuwa na kiasi cha fedha cha kuwasaidia vijana wetu ili waweze kuwa na ubunifu na mfuko huo uwasaidie kuweza kutengeneza bidhaa mbalimbali ambazo zitaweza kuingia sokoni. Hilo ni jambo muhimu sana kwa ajili ya nchi yetu, hatuwezi kuwa na vijana ambao wamesoma, wana elimu, lakini elimu yao haitumiki kwa ajili ya maendeleo ya Taifa. Kwa hiyo, ninaomba sana na ninaomba nisisitize kwa mara nyingine kwamba ni jambo muhimu sana kuhakikisha ya kwamba, kunakuwa na mnong’ono wa Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mnong’ono wa Taifa namaanisha nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha zote za nchi hii, utajiri wote wa nchi hii uko hapo chini kwenye hivyo viti vya hapo mbele vilivyokaa hapo. Utajiri wote wa Taifa hili uko hapo mbele, nikianzia huko kwa Mheshimiwa Mashimba nikaja mpaka huku kwa Mheshimiwa Kipanga, trilioni 33 za nchi hii ziko hapo chini, nani anazipata, ndiyo swali la kujiuliza, nani anazipata? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kunong’ona kama Taifa kwamba, tumeamua kama nchi tenda zote za kuanzia kiasi hiki cha fedha ziende kwa vijana wa Kitanzania? Hatuwezi kuongea kama Taifa ya kwamba, fedha hizi akija mwekezaji yeyote katika nchi hii lazima ashirikiane na Mheshimiwa Tale? Maana yake nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maana yake ni kwamba, kwa kufanya hivyo fedha hizi zitabaki kwa Watanzania wenyewe zinazunguka hapahapa nyumbani na tutatengeneza mabilionea wengi ambao unawaongelea hapa ndani. Tusipofanya hivyo watakuwa wanakuja hapa watu na begi baada ya miaka mitano ameshakuwa bilionea anaondoka zake sisi tunabaki tunashangaa. Matokeo yake vijana wetu wanajaa chuki ndani ya mioyo yao wanaanza kuchukia Serikali yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu ni lazima itengeneze mazingira ya kuwawezesha vijana wa nchi hii kutajirika. The Government must create environment ambayo ina-foster development ya vijana wetu. Kama hatutengenezi mazingira ya vijana wetu kutajirika hakuna kijana wa nchi hii atakuwa bilionea na mabilionea wataendelea walewale kila mwaka, mwaka huu na mwaka ujao. Kama tuna nia ya kutengeneza mabilionea wengi ni lazima tuseme kwa nia moja kwamba, tumenong’ona kama Taifa ndani ya chumba ambacho hatuzungumzi wala hatuandiki gazetini wala mahali popote ya kwamba, tumeamua kama Taifa vijana wetu ni lazima watajirike. Kwa hiyo, ukiwa kama ni mradi, Rais wetu alizungumza juzi akasema nimeleta fedha hizi zisaidie wawekezaji wa ndani. Ile kauli tafsiri yake ni nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara ya kutoka Buchosa kwenda Sengerema itengenezwe na mzawa. Tukifanya hivyo utajiri huu utazunguka kwa vijana wetu hawahawa ambao tunawatazama leo, mwisho wa siku nakuhakikishia mabilionea wataongezeka. Tusipofanya hivyo tutaendelea kushuhudia watu wanakuja hapa Tanzania baada ya muda mfupi ni mabilionea wanaondoka wanatuacha hapa tunalalamika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati umefika wa kuhakikisha kwamba, vijana wa nchi hii, vijana wa Taifa hili wananufaika na utajiri wa Taifa lao ili mwisho wa siku waweze kuanzisha viwanda wao wenyewe waajiri wenzao hapahapa nyumbani. Jambo hili linawezekana, South Africa walifanya, South Africa walikuja na utaratibu wa Black Empowerment. Black Empowerment ikawawezesha akina Motsepe na Rais wa South Africa wa sasa kuwa mabilionea mpaka leo. Sisi kama Taifa tunashindwa wapi? Tunashindwa nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatuwezi kama Taifa kuamua kwa nia moja kwamba, tumeamua kutengeneza mabilonea 20 katika nchi hii, tukaenda TIRDO, TIRDO wanayo incubation center ambapo vijana wetu wana products nyingi wamebuni lakini hawana mitaji ya kufanyia biashara. Wakienda kwenye benki za biashara kukopa wanaombwa nyumba na kama kijana hana nyumba hawezi kutengeneza product yoyote ile. Hatuwezi kama Taifa kusema, Mheshimiwa Waziri unanisikia, sehemu ya tozo hii tuchukue pesa kidogo tuanzishe National Innovation Fund ambayo kijana akiwa na idea yake yuko COSTECH au yuko TIRDO awe supported atengeneze bidhaa hatimaye aje aajiri wenzake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, haya mambo yanawezekana. Nia ya wazee wetu wa mwanzo ilikuwa ni kuona Watanzania wanatajirika. Hatuwezi kuendelea kukaa hapa tunashuhudia wanatajirika watu, wanakuja wanatajirika wanaondoka, hatutakubali. Tukiendelea hivi baada ya muda utaanza kuona kutakuwa na chuki dhidi ya kundi fulani la watu. Tuwasaidie vijana wa nchi hii waweze kufanya vizuri maishani mwao na waweze kufanikiwa kwa sababu, hii ni nchi yao na wana haki ya kutajirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante kwa kunisikiliza. (Makofi)