Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

Hon. Jumanne Kibera Kishimba

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kahama Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa Unaokusudiwa Kutekelezwa na Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023 pamoja na Mwongozo wa Kuandaa Mpango wa Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2022/2023

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipatia nafasi ya kuchangia kwenye Muswada huu wa Bajeti ya mwaka 2022/2023. Pia mimi nam- support, namuunga mkono Mheshimiwa Rais kwa kazi kubwa sana aliyofanya, hasa hii juzi kwa hizi fedha shilingi trilioni moja, ukilinganisha na wakati huu wa Corona ambapo hali ya dunia kiuchumi siyo nzuri. Namshukuru sana na imetufikia kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza kwa malalamiko makubwa hasa kwa upande wangu wa Jimbo la Kahama Mjini. Nimekuwa nikipata zawadi, heshima kubwa, nimekuwa wa kwanza kwenye mapato, kwenye makusanyo na kwenye kila kitu. Hata hivyo, ninavyoongea, barabara zangu za mjini ni mbaya sana. Haiwezekani mtu anayeongoza kwa mapato halafu unamnyima fedha ya barabara. Atapataje hizo fedha bila barabara? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata sasa hivi, zile shilingi milioni 500 za Mheshimiwa Rais bado sijapata. Ninavyoongea nina shilingi milioni 18 peke yake. Sasa itawezekana mnanipa mimi zawadi na matunzo. Afadhali mtoe zile zawadi za ushindi, mnipe fedha za barabara. Baadaye nikiwa salama, mrudishe yale matunzo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ulipita juzi Kahama ukiwa unaenda Chato. Kweli ukiwa barabarani pale unaona mji unang’aa, lakini kule ndani hali ni mbaya sana. Mapato ya Serikali yanayokuja yanatoka maeneo yale. Kwa hiyo, tunamwomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha, atupatie hizo fedha ili wananchi hawa wakati huu msimu wa mvua unapoanza waweze kufanya kazi zao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala ambalo umeliongea, nami nilikuwa nakuja huko huko. Labda tu sasa kwa wachumi wetu tuone kama wanaweza kufanya namna. Maana yake wote tunaziona kero. Ujenzi unaoendelea kwa zahanati, hospitali; madarasa hatuna shida sana. Unaangalia, kweli vijiji vyetu au kata zetu hazikukatwa kama madarasa. Wananchi walikuwa wanakaa maeneo yale, lakini unapotamka kijiji ukasema utaweka zahanati kila kijiji au Kituo cha Afya kila Kata, unatumia uwiano gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zahanati zile ni kubwa, Vituo vya Afya kwa michoro ile, inatugharimu kweli shilingi 400/= mpaka shilingi 500/=. Mahudhurio ya wagonjwa ni wagonjwa 20 au 18 kwa siku. Kwa nini Serikali wasijenge jengo dogo la shilingi milioni 30, ile shilingi milioni 370 ikawekwa benki kwenye fixed account, fedha itakayopatikana iwatibu wagonjwa bure iwape mpaka uji? Maana yake wagonjwa hawafuati jengo, wagonjwa wanachofuata ni dawa na huduma. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vijiji kwa leo baada ya mabadiliko makubwa ya pikipiki, WhatsApp, kila kitu vipo karibu karibu sana. Ni bora hizo fedha watupatie tuweke fixed deposit, wataalam watuchoree michoro ya kawaida ya fedha kidogo. Hizi fedha tuziweke fixed deposit, ile interest iwasaidie wagonjwa kwa kuwatibu bure pamoja na chakula. Sasa hivi sisi kule Kanda ya Ziwa tuna-compete na Waganga wa Kienyeji. Haiwezekani wewe una hospitali nzuri haina watu, Mganga wa Kienyeji ana nyumba ya makuti amejaza wagonjwa. Ina maana kuna tatizo pale kwako. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukweli mimi najua tunachenga chenga, lakini mfungwa ni mali ya Magereza, mhalifu ni mali ya Polisi, huyu mgonjwa ni mali ya nani? Maana yake mgonjwa hana mwenyewe. Katiba yetu inasema, Serikali italinda watu wake na mali zake kwa nguvu zote, kwa hali na mali mpaka na jeshi. Kwa nini hatuna namna yoyote ya kumwokoa mtu anapokuwa anaumwa? Mimi nafikiri nimwulize Mheshimiwa Waziri wa Fedha kwa nini hapo panachengwa? Ila baada ya kifo tunakuwa na misiba, tunakuwa na mambo mengi yanakuja, lakini kwenye dawa hakuna mtu anataka kupagusa wala kwenye matibabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba sana Mheshimiwa Waziri wa Fedha alifikirie sana. Nafikiri hili linaweza likawa ndiyo kero kubwa kuliko kero yoyote. Leo hii bei ya dawa/matibabu, wote ni mashahidi humu, sasa hivi umezuka mtindo, unapokuwa na mgonjwa mahututi, wanasitisha matibabu kwa sababu bill imekuwa kubwa. Sasa kama wamesitisha nawe huna fedha, ina maana unatakiwa ukabiliane na kifo. Je, ni sahihi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Serikali haina namna yoyote? Nani tumwombe na nani tumwulize? Hali ya kule vijijini, maisha ni magumu sana, na ugonjwa hauna kusema huyu ni tajiri, huyu ni masikini, huyu ni nani? Mtu yeyote anaweza kuugua wakati wowote. Nafikiri mambo mengine ni kwa ajili ya mabadiliko makubwa ya uchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti na Mheshimiwa Waziri wa Fedha, labda Serikali ingefikiria baadhi ya miradi kama mnaweza kuitazama upya, inatakiwa kuendelea sasa hivi au tuishie wapi? Kwa sababu, ninachosema, leo bei ya container kutoka Dubai kuja Dar es Salaam ni dola 15,000, kutoka dola 3,500. Je, hii miradi ikipanda mara nne, tutapata wapi fedha? (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. JUMANNE K. KISHIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. naunga mkono hoja. (Makofi)