Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

Hon. Susan Limbweni Kiwanga

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Mlimba

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa Mwaka wa Fedha 2016/2017

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi na mimi nichangie kwenye hotuba hii ya Waziri wa Afya.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kabisa na kwenye kitabu cha Mheshimiwa Waziri, ukurasa wa 75 - 76, naomba kunukuu, nitakwenda pale mwishoni kidogo; “Naomba kutoa taarifa kwamba Serikali inatarajia kuwasilisha katika Bunge lako Tukufu Muswada wa Mabadiliko ya Sheria ya Bima ya Afya. Muswada huo una mapendekezo mbalimbali ikiwemo sharti la ulazima wa wananchi wote kujiunga na Bima ya Afya na wale wote wenye uwezo kuchangia bima hiyo.”
Mheshimiwa Mwenyekiti, hiki kipengele kimenitetemesha mwili mzima nikaikumbuka Mlimba, wananchi watakaolazimishwa kuchangia ikishakuwa sheria ya nchi hii. Mlimba yenye kata 16, yenye kituo kimoja cha afya yaani sitaki hata kusema, ndiyo maana nilikuomba Mheshimiwa Waziri ufike uone mwenyewe. Kama alivyosema Mbunge aliyetangulia kwamba unaonekana una haiba na kweli ndivyo ulivyo, lakini mzigo huu wa Wizara uliyopewa ni mkubwa sana, lakini bila pesa utaishia kulia jinsi kina mama, wazee na watoto wanavyoteseka katika nchi hii.
Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo maana Mheshimiwa Waziri nimekukaribisha uje Mlimba, mnakwenda tu kwenye yale maeneo ambayo mmeyazoea, naomba mje Mlimba, Jimbo lenye kata 16, vijiji 61, vitongoji mia mbili na zaidi. Mimi nitakupeleka kwenye kitongoji, kutoka kwenye kitongoji mpaka kijiji ni kilometa 20 yaani kutoka kitongojini mpaka katika kijiji kilometa 20 halafu hapo kwenye kijiji hakuna zahanati, unatakiwa uende tena kilometa 30, ukiongeza na 20 zinakuwa 50, mtoto anaumwa umembeba, wakati wa mvua barabara hazipitiki, maji mpaka kiunoni unaweza kuogelea, jamani kama kuna watu wanakufa nchi hii basi ni Jimbo la Mlimba, hali ni mbaya kuliko maelezo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa napenda kuuliza ni lini katika bajeti hii itatambua kwamba Mlimba kuna wananchi? Bahati mbaya sana Mlimba tulikuwa wachache, lakini leo tumewapokea watu wa aina mbalimbali, kila kabila unaloliona humu ndani liko Mlimba, ndugu zenu wako kule. Kwa sababu gani, Mlimba ni eneo la rutuba, ukipanda ndizi twende, mpunga twende, kokoa twende, ufuta twende, miti usiseme, mahindi twende, kwa nini wasikimbilie kule, kila kitu kinakubali. Gesi ndiyo iko kule, umeme wa Kihansi upo, kuna shida tena Mlimba? Kwa hiyo, watu wameingia wengi lakini huduma sifuri.
Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, mimi nimesimama hapa kuchangia hii hotuba, siwezi nikachangia maeneo makubwa sana ya Kitaifa kwa sababu nina wajibu ndani ya Jimbo la Mlimba. Naomba chonde chonde, mje mtembelee Mlimba, mlinganishe na haya ninayoyasema halafu mtaona wenyewe kama hamkulia huku mimi nawaambia. Mimi wakati wa kampeni nilikuwa nalia, hata nilivyokuwa nasikia ooh, waganga wa kienyeji wanafungiwa, fungieni huku huku, kule watu wanatibiwa na waganga wa kienyeji. Hakuna hospitali, hakuna zahanati, hakuna chochote, kwa nini mtu asiende kwa mganga wa kienyeji. Hiyo huduma mnayosema ya wazee labda mjini huku. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini dada yangu hapa Mheshimiwa Mollel anasema alikuwa huko Muhimbili, ameshuhudia kwa macho yake mzee amekuja Muhimbili aliambiwa aende akapimwe lakini amekwenda kule laboratory akaambiwa baba shilingi 40,000 ni mzee anatembelea mkongojo. Mheshimiwa Mama Mollel akaingilia kati kwa uchungu, kwa nini mnaacha kumtibu huyu baba, wanasema bila shilingi 40,000 hakuna bure, ikabidi atoe amalipie yule mzee apate matibabu. Sasa hii huduma ya wazee iko wapi? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama Dar es Salaam namna hii Mlimba kuna kitu tena kule? Giza totoro, haki ya Mungu kama hatujapata uhuru.
Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba chonde chonde, mfike Mlimba. Kwa sababu kama kuna kata 16 kituo cha afya kimoja na chenyewe kinademadema, hawana wodi ya wazazi yaani ni aibu kwa Jimbo la Mlimba. Kutoka Mlimba mpaka Ifakara ambapo kuna Hospitali ya Wilaya ama St. Francis ni kilometa 150 barabara zote kama zina makaburi ya watoto kutokana na hayo mashimo, tumewakosea nini? Kule ni hatari jamani, naomba mje muone. Halafu unamwambia ananitania tu, jamani pelekeni vitu kule Jimboni vya Bunge, aah sasa hivi hatuwezi kwenda mvua, kwani tunaoishi kule wanyama? Twendeni hata wakati wa mvua mkaone hali halisi.
Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa TAMISEMI kama mpo hapa mchukue, haiwezekani vijiji 61 kuna zahanati 18, haiwezekani! Wananchi kule wanapata wapi matibabu! Hali ni mbaya kuliko maelezo! Kina mama wanakufa kule, kina baba wazee wanateseka kule, watoto wanakufa kule.
Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kwa ukurasa wa 75 mlivyoandika kwamba mnakwenda kuleta bima ya afya lazimishi, Mlimba muitoe katika hayo mambo, hiyo sheria iseme kabisa Mlimba aah aah, tutalazimisha maeneo mengine tu. Kwa sababu haiwezekani, kwanza dawa zenyewe hawapati sasa unalazimishaje?
Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachoomba, muandae kwanza mazingira ya kuandaa vituo vya afya venye Madaktari, Manesi na dawa za kutosha, mkilazimisha hiyo ni sawa. Msilete sheria kabla hamjaandaa mazingira sahihi ya watu kupata huduma, nendeni mkakague mjiridhishe. Kwa hiyo, mimi naomba hii sheria mmeiandika tu hapa lakini ichelewe kabisa, bado tuko miaka 20 nyuma. Ni nzuri sana kwa sababu nchi za wenzetu wanatekeleza sheria hiyo. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, nilichukua takwimu kutoka kwenye halmashauri yangu, nina takwimu hapa na nitakuletea lukuki, kama za TAMISEMI ziende TAMISEMI, kwenye Wizara yako, maana hapa tunapiga, uchungu mwingine, mateso mengine wanatuletea TAMISEMI, ninyi TAMISEMI ninyi, ni matatizo makubwa! Haiwezekani sera inasema zahanati kila kijiji lakini vijiji vyote havina zahanati. Wananchi maeneo mengine wamechangia, wamejenga zahanati, haijamaliziwa, hakuna choo, hakuna mtumishi, hakuna chochote. Kwa nini mnawafanyia hivyo Watanzania? (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi sina maneno mengi, nasema mje Mlimba mjionee wenyewe kama haya maneno ninayosema ni ya uongo ili watu wapate huduma yao kwa mujibu wa kodi wanazolipa, mtushirikishe. Kambi ya Upinzani wamesema vizuri, lakini sasa Serikali hii hata mkishauri mpango mzuri hapa, basi kwa mpango huu CHF na dawa, ili Wizara ya Afya ipate hela ingizeni hata shilingi 50,000 kwenye mafuta ya magari, uongo, kweli? Tukikubaliana hapa kama REA hela sijui mmeipeleka wapi, ninyi vipi? Yaani hapa hata tukipitisha mpango mzuri wa kukusanya shilingi shilingi kwa Watanzania mnapeleka hela sehemu nyingine. (Makofi)
Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, naomba niishie hapo.