Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jacquline Andrew Kainja

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipatia nafasi hii nami niweze kuchangia katika hotuba hii nzuri ya bajeti. Naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kutuletea bajeti nzuri. Nampongeza Waziri wa Fedha, Naibu Waziri na timu nzima ya Wizara. Ni bajeti ambayo ina matumaini kwa wananchi, bajeti ambayo imesikiliza mawazo asilimia 80 ya Wabunge na inaonyesha kwamba ile moja ya kazi ya Wabunge kuishauri Serikali, basi hapa katika bajeti hii inaonekana Serikali imesikiliza mawazo ya Wabunge nao wameenda kuyafanyia kazi na wametuletea hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niende kuchangia moja kwa moja kwenye upande wa afya. Naipongeza Wizara kwa kazi nzuri ya kutuletea bajeti ya shilingi bilioni 265.8 kwa ajili ya afya, dawa vifaatiba na kumalizia miundombinu iliyojengwa na wananchi kwa nguvu zao wenyewe ikiwepo zahanati 8,004, pamoja na Vituo vya Afya 1,500. Namwomba Waziri wa Fedha, bajeti hii kwa upande wangu naiona bado ni ndogo kwa afya, lakini pamoja na udogo wake tuweze kuipokea hivyo ilivyo ila iende ikatekeleze kama inavyosomeka hapa, kama mpango ulivyo. Hii bajeti iende kama ilivyo, itekelezeke kule, tuisaidie MSD.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kabisa ni jambo ambalo liko wazi kwamba MSD inafanya kazi katika hali ya uhafifu. Tunajua kabisa ina madeni nje na ndani ya nchi, lakini kama bajeti hii ambayo inaonekana hapa itapelekwa fedha hizi kwa ajili ya kuwezesha dawa na vifaatiba kama ambavyo imeelezewa, tunaona kabisa changamoto ya ukosefu wa dawa na vifaatiba itaenda kupungua. Kama Wabunge wengine ambavyo wameweza kusema na kumsifia Waziri wa Fedha, itakuwa ni Waziri wa kiwango cha juu kwa bajeti hii iliyokuja hapa. Naomba niseme, atakuwa ni Waziri wa Fedha wa kiwango cha juu sana kama bajeti hii itatekelezeka kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hapo atakuwa ameweza kututolea changamoto kubwa tunayopata akina mama na watoto mahospitalini kwa ukosefu wa dawa; na hasa kina mama zile changamoto za kupoteza uhai wakati wa kujifungua ambapo hata Mheshimiwa Rais wakati wa hotuba yake aliongea akasema katika moja ya vita atakayoenda kuipiga ni kuhakikisha vifo vya mama mjamzito wakati wa kujifunga vinaisha. Sasa vitaisha kama bajeti hii itatekelezeka kwa asilimia mia moja. Kwa hiyo, namwomba sana Waziri wa Fedha, bajeti hii ipeleke pesa zinakohitajika. Kama ni MSD tuisaidie iweze kuhudumia wananchi, waweze kupata dawa na vifaatiba kama inavyotakikana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala zima la Bima ya Afya. Ilani ya Chama cha Mapinduzi tuliyoinadi mwaka 2020, tuliwaomba wananchi kwamba wachague chama chetu, tutakuja na Bima ya Afya kwa kila mwananchi. Bajeti hii imeeleza na inaonyesha kwamba kwa mchakato wa mwazoni tunahitaji shilingi bilioni 145 kwa mwanzo wa fedha. Hata hivyo, naiomba Wizara, nilikuwa natamani Mheshimiwa Waziri atakapokuja ku-finalize aweze kutuelezea, hii pesa ambayo ameona kwamba ni shilingi bilioni 145: Je, ni pesa ambayo imekaa kwa bima ya mfumo upi? Ni Bima ya NHIF au ni CHF?

Mheshimiwa Naibu Spika, tunachotegemea ni wananchi wapate bima yenye tija, isiwe bima ile ambayo mgonjwa anaenda kutibiwa hospitali ya Serikali tu, hana option ya kwenda kwenye private hospital. Hii itatusaidia kuweka mahusiano mazuri kati ya Serikali pamoja na private sector. Ile sera yetu ya PPP itaweza ku-apply vizuri zaidi maana mgonjwa au mtu anayehitaji matibabu atakuwa na option ya kwenda sehemu yoyote aidha ni private au aende Serikalini na kote atapata huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, nilikuwa naomba sana Waziri wa Fedha, huu mchakato wa shilingi bilioni 145 wa Bima ya Afya uwe ni wa bima ambayo ni kama ya NHIF ambapo mgonjwa anaenda sehemu yoyote anapata ile huduma.

Mheshimiwa Naibu Spika, vilevile, nimeona hapa, inaonyesha bajeti yam waka 2034/2035 ndiyo tutakuwa tumeweza kumaliza suala hili zima la Bima ya Afya kwa kila mwananchi. Kwa hiyo, nikiangalia hapa naona kama tuna miaka 14 ya kuweza kukamilisha hili. Natambua kabisa universal health coverage siyo suala dogo la miaka miwili mitatu minne, iwe imeisha.

Naomba Waziri wa Fedha arudishe nyuma kidogo kwa sababu mwaka 2020 tumewaomba wananchi kwamba tutawaletea Bima ya Afya; mwaka 2025 tena tutaenda kuwaambia tena tunawaletea Bima ya Afya, wakati huo bado tuko kwenye process. Kuna wengine wamepata kuna wengine awajapata.

Mheshimiwa Naibu Spika, inavyoonekana, tena mpaka 2030 bado tutakuja kuwaambia wananchi tunawaleteeni Bima ya Afya kwa kila mwananchi. Bado naona ni muda mrefu sana, naomba tu apunguze. Japokuwa ni jambo kubwa, sawa, lakini hebu irudi nyuma kidogo tusiwe tuna muda mrefu wa kupeleka hii Bima ya Afya kwa kila mwananchi.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niongelee suala la kilimo. Natambua tuna benki ya kilimo, tuna Tanzania Investimate Bank ambazo zina riba kubwa. Nampongeza Mheshimiwa Rais ameweza kuona riba hizi ambazo ni kubwa na zinawakandamiza wananchi ambao wanashindwa kuweka maendeleo zaidi. Namwomba Waziri tuwe na mfuko wa kuchochea maendeleo ya kilimo na viwanda kwa sababu tunaelewa tuna Sera ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita ya Tanzania ya Viwanda.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, katika hizi sera tukiwa na mfuko wa kuchochea maendeleo, tunaona kabisa ni namna gani wananchi wataenda kukopa pesa kwa riba nafuu kwenye mifuko ya kuchochea maendeleo. Wakati huo huo, tunajua kabisa kilimo kinatupatia asilimia ya 65 ya ajira, asilimia 66 tunapata malighafi, asilimia 100 chakula tunachotumia sisi Watanzania kinatokana na kilimo.

(Hapa kengele ya kwanza ililia)

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, sorry ni kengele ya kwanza au ya pili?

NAIBU SPIKA: Ya kwanza.

MHE. JACQUELINE K. ANDREA: Mheshimiwa Naibu Spika, asilimia 100 tunapata chakula kwa Watanzania na vilevile asilimia 30 ni kwa ajili ya kuingiza pesa za kigeni.

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kwenye viwanda tunakuza thamani ya malighafi ya bidhaa zetu, tunaongeza ajira, tunakuza wigo wa kuongeza kodi. Kwa hiyo, tuliangalie eneo hili la kilimo na viwanda, ni namna gani tutachochea ili wananchi waweze kupata mikopo ya bei nafuu, huku tukiwa tumewaambia vijana wajiajiri? Anajiajiri vipi kama bado hawezi kujisimamia mwenyewe na akienda kwenye benki za kilimo riba ni kubwa ambayo mama amesema itakuja kupunguzwa? Kwa hiyo, tunaomba Waziri wa Fedha aliangalie hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kuipongeza Wizara na bajeti nzuri ambayo imesikiliza mawazo ya Wabunge wote. Wabunge walisimama katika Wizara ya TAMISEMI ilipokuwa inawasilisha bajeti yake, wakawa wanatetea sana suala la Madiwani. Limechukuliwa vizuri sana, wameleta hapa ufumbuzi kuhusu posho za Madiwani. Mama amelipokea, amelielewa na atatekeleza kwa mujibu wa taarifa hii ya bajeti iliyosomwa. Ameelekeza kwamba Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI wataenda wakakae.

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niombe tu Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI wanapokuja kukaa pamoja kuangalia Madiwani hawa wanaangaliwaje, waweze kuangalia na lile jambo ambalo kuna Madiwani wanalipwa, ni posho tu inalipwa lakini hawawekewi nauli. Unakuta kuna mtu anatoka kwenye kata yake mpaka anakoenda kwenye Halmshauri ambapo kikao kipo ni kilometa 30, lakini mtu anayetoka kilometa 60 atapewa nauli, sawa; atapewa na pesa ya kulala sawa; sasa huyu mtu ambaye hata kama atatembea kilometa tano, analipwa nini? Waweze kukaa wawapatie pesa hizo za nauli hawa Madiwani.

Mheshimiwa Naibu Spika, tunajua kwa hali ilivyo sasa hivi, watu kutembea kwa muda hata wa nusu saa ni kama unapoteza muda. Mambo ni mengi. Kwa hiyo, tujaribu kuwa tunarudisha nauli za hawa Madiwani ambao wanatoka kilometa 20 kilometa tano waweze kurudishiwa. Kwa hiyo, namwomba Waziri wa Fedha na Waziri wa TAMISEMI ambao wameagizwa na mama yetu kipenzi, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan wakakae pamoja, waweze kuangalia suala hilo la nauli. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema hivyo, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. (Makofi)