Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Jackson Gedion Kiswaga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kalenga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana nami kupewa nafasi hii adhimu kabisa kwa ajili ya kuchangia Bajeti Kuu ya Serikali. Kwanza nami nianze kumshukuru sana Rais wetu, Mheshimiwa Mama Samia Suluhu Hassan kwa upendo wake mkubwa na usikivu mkubwa ambao ameuonesha kwa sisi Wabunge na Watanzania wote kwa ujumla. Namshukuru kwa sababu ya yale ambayo tayari wenzangu wameshayazungumza kwa kupewa zile shilingi milioni 500 kwenye Majimbo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, namshukuru Rais kupitia Waziri wake wa TAMISEMI, Mheshimiwa Ummy Mwalimu ambapo Wabunge tumeelekezwa kwamba tupeleke mapendekezo ya eneo gani tutapenda shule zetu zijengwe angalau shule moja ya Kata. Hii inanifanya niendelee kuamini misemo mingi ambayo imekuwa ikisemwa na majukwaa mengi ya Kimataifa, hata World Economic Forum wakati fulani walisema, nanukuu: “Having women in leadership roles is more important now that ever.”

Nikiendelea kunukuu makala moja iliyoandikwa na mama mmoja anaitwa Lynn Camp ambaye ni CEO wa EVERGREEN, hawa wanajihusisha na biashara za mitandao na digitali, anasema: “Women led Government is taking bigger steps forward on behalf of the state economy, they have shown the real desire to listen to experts in wider world of business.” (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nikiendelea kunukuu anasema: “the survival of planet requires new thinking and strategies we are in the pitched battle between the present array of resources and the attitude and the future struggling to be born. Women get it, young get it, they are creating a whole different mindset.” Sasa ukisoma hizi nukuu zote zinaonesha huko tunakoelekea sasa akina mama pamoja na vijana wanachukua nafasi. Inaonekana kwamba wameleta mchango mkubwa sana katika kufikiri na kuleta mikakati mipya ambayo itakwenda kukuza uchumi wetu kama nchi na biashara za dunia kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia, hata Deloitte and Tosh walisema kwamba; companies led by women in leadership they have six times innovative than other companies and also, they meet financial targets two times. Kwa hiyo, wakimaanisha kwamba kampuni ambazo zinaongozwa na akina mama inaonekana zina ubunifu mara sita dhidi ya kampuni nyingine ambazo zinaongozwa na akina baba. Kwa hiyo, kwa kweli namshukuru sana Rais. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kutokana na hilo nitumie nafasi yangu ya Kibunge kuishauri Serikali na kumshauri Mheshimiwa Mama Samia, kwa kuwa sasa imeonesha kwamba mwelekeo sasa katika uongozi wanawake na vijana sasa wanachukua hatamu, nilikuwa napendekeza kwamba hata katika miradi mikubwa ambayo tunafanya sasa, tuanze sasa kutaja wanawake ambao walileta mchango mkubwa kwenye Taifa hili…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru. Napenda nimpe Mheshimiwa Kiswaga taarifa. Nampongeza sana kwa jinsi anavyotambua kwamba wanawake na vijana watachukua hatamu. Kwa maana hiyo, mwaka 2025 ni dhahiri kwamba Mheshimiwa Mama Tendega atakuja kwa Jimbo la Kalenga. Ahsante. (Kicheko/Makofi)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa hiyo ina utata kwa sababu Jimbo lile la Kalenga lilitawaliwa na Chifu Mkwawa. Kwa hiyo… (Makofi/ Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Kiswaga, sina hakika kama hii ilikuwa ni taarifa, lakini malizia mchango wako. (Kicheko)

MHE. JACKSON G. KISWAGA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Kwa hiyo, nimesema kwamba tuwe na maeneo sasa ambayo yanatajwa kwa ajili ya akina mama. Kwa mfano, wako akina mama ambao walileta michango mikubwa katika Taifa hili kama akina Mheshimiwa Getrude Mongella na Mheshimiwa Anne Makinda. Tunaweza hata tukajenga hospitali fulani ya akina mama tukaiita Anne Makinda au Gertrude Mongella. Tunafanya hivyo ili ku-inspire vijana wengi wa kike. Hata mimi nina binti ambaye ninatamani aje awe mtu mkuu sana. Kwa hiyo, wakianza kuona waliotangulia wanaheshimiwa, basi na wengine watafuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kweli bajeti hii ina mambo mengi sana mazuri ambayo nimeyaona yametajwa humu. Moja ya jambo muhimu sana ambalo nimeliona ni lile la kuwa na sensa. Ni muhimu sana katika kukuza uchumi wetu, kuwa na data muhimu kwa wakati. Unajua katika mipango mingi ya maendeleo duniani inategemea sana takwimu. Unaweza ukasema kwamba tunahitaji shule 10 katika Jimbo la Kalenga; kwa sababu ya takwimu tulizonazo ambazo siyo za kweli, kumbe takwimu halisi zinataka tujenge shule 20. Kwa hiyo, naipongeza Serikali kwa kutenga bajeti karibu shilingi bilioni 328 kwa ajili ya kufanya sensa mwakani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niendelee kumpongeza sana Waziri wa Fedha pamoja na msaidizi wake na pia pamoja na Mwenyekiti ambaye ni jirani yangu hapa kwa kuchambua bajeti vizuri na kuzingatia mawazo mengi ya Wabunge pamoja na Watanzania kwa ujumla. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika bajeti hii kuna mambo mengine ambayo tunataka tuchangie kidogo labda kwa kuboresha. Kama nilivyosema mimi nimekuwa kwenye mitandao miaka mingi; kwenye hii kodi ambayo tumeianzisha kwenye mitandao hasa kwenye laini za simu, tumesema tuna- charge kati ya shilingi 10/= mpaka shilingi 200/= kwa siku. Ukweli ni kwamba ukiangalia kwenye watumiaji wa simu, asilimia 65 ya wateja wao, wengi wana-charge kwa mwezi shilingi 500/=. Asilimia 59 mpaka 65 wanaweka shilingi 500/= kwa mwezi. Sasa ukisema kwamba uta-charge kila siku shilingi 10/=, maana yake unasema shilingi 300/=. Kwa hiyo, maana yake kuna kundi kubwa ambalo linakwenda kuathirika.

Mheshimiwa Naibu Spika, labda pengine kuna shida kwenye uchapishaji, tuseme kwamba labda tuna-charge shilingi 10/= kwa kadri mtu anavyoweka fedha. Tukiangalia pia kwenye ile miamala, tumesema kwamba tuta-charge kati ya shilingi 10/= mpaka shilingi 10,000/=. Ukiangalia muamala wa juu kwa mfano shilingi 1,000,000/= tuna-charge shilingi 8,000/=. Hili limeleta malalamiko sana wakati hivi viwango vinapandishwa kwa wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hili nilikuwa nafikiri Serikali ione uwezekano. Kodi tunaitaka kwa sababu tunataka kufanya mambo mengi na mama ameshaonesha njia kwamba tunataka kufanya transformation kwenye uchumi. Ingekupendeza ungekaa na watu wenye mitandao wakupe uhalisia wa hili jambo, kwa sababu tukiongeza shilingi 10,000/= kwenye shilingi 1,000,000/= inakuwa shilingi 18,000,000/=. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiangalia kwa mfano Airtel, imechukua muda mrefu sana kufanya miamala ya bure ili angalau kuchochea watu wengi waweze kufanya hiyo miamala. Wamechukua muda mrefu sana. Sasa leo tukisema tunaongeza kwenye shilingi 10,000/= inaweza ika-slow down na hiyo kodi ambayo tunategemea kuipata tusiweze kuipata. Kwa hiyo, hili ninaomba pia tukaliangalie.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kwenye mambo ya kodi yanayohusiana na ardhi, kuna viwanja ambavyo vimepimwa vingi na Watanzania wengi hawalipi. Tunakushukuru umesema kwamba kwenye Property Tax tutaweka kwenye Luku. Watu wengi wamechangia hapa, najua utapata hekima ya namna gani utaweza ku-charge kama mtu ana kiwanja, ana nyumba nyingi ana Luku nyingi, hiyo hekima Mungu atawaongoza.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna eneo hili lingine la viwanja, watu wengi sana hawalipi kwenye land rent, na huko tuangalie tutafanya nini? Kwa sababu kuna kodi nyingi huku zimelala na zinaweza kusaidia sana uchumi wetu na tukafanya mambo mengi ya kimaendeleo. Kwa hiyo, hilo nalo tunaweza tukatengeneza task force ambayo itakwenda kusaidia kukusanya hizi kodi, vyovyote mtakavyoona inafaa naomba tuweze kutupia jicho.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kuna jambo lingine ambalo nilikuwa nalifikiria, huko tuendako uchumi mwingi utatoka kwenye kilimo. Sasa ningeomba kwamba, mkakati kwenye kilimo uwe namna hii kwamba, tumekuwa tuki- acquire ardhi kuwapa wawekezaji, sipendi hilo jambo la kuchukua ardhi kwa wananchi kuwapa wawekezaji; napenda hivi kwamba, tuwe na ardhi kwa ajili ya uwekezaji kama walivyofanya Dubai wanasema land for equity. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukija pale Iringa kwangu, nina eka zangu 2,000 sijaziendeleza, Chalamila ana eka 2,000 hajaziendeleza, Mkoa naye 5,000 hajaziendeleza, tunazitambua zile eka kwa pamoja tunasema eneo hili lina eka 20,000 wanaomiliki hapa ni Mheshimiwa Kiswaga, ni Mkwawa, ni fulani. Muwekezaji aje awekeze pale na tumeshaiainisha ardhi, lakini sisi tuchukue asimilia 20 ya uwekezaji. Akae miaka 33, miaka mingapi, lakini sisi tuwe na hisa kutokana na ardhi tuliyonayo na yeye anakuja na pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ndio maana Dubai leo watu wamekuwa matajiri kwa sababu walikuwa na ardhi. Hili suala la kuichukua ardhi tuwape wawekezaji linaleta shida, unakuta kwamba, muwekezaji anakwenda kwenye kijiji anapewa eka labda 500 eti kwa sababu amejenga ofisi ya vyumba viwili. Baada ya hapo mnakwenda kumuomba pesa ya maendeleo 500/= tu, labda 100,000/=, anasema mpaka muandike barua, hii haiwezekani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kama ile ardhi kijiji kingeamua kushirikiana naye kwamba, wewe njoo wekeza katika eka hizi 500 tunakupa, lakini katika mazao utakayopata utupatie sisi asilimia 20 kwa miaka yote, sisi tutakuwa na uchumi wetu kama kijiji na hatutakuwa na tatizo tena la kwenda kuombaomba. Tukiacha hili jambo ardhi yetu itapotea na Watanzania hawatakuwa na ardhi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana. ninaunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)