Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Grace Victor Tendega

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa fursa ilii na mimi nichangie katika hotuba hii ya bajeti iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ilikuwa inanipa ugumu sana kupongeza sana, lakini kwa mara ya kwanza ninapenda kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan kwa kuleta bajeti ambayo kiasi fulani imeakisi zile kelele ambazo tulikuwa tukizipiga. Ninasema hivi kwa sababu Mheshimiwa Rais alituita pia wanawake wote bila kujali itikadi. Tulikwenda, tulimsikiliza na tukaona kwamba vitu anavyovizungumza ni vitu ambavyo vikitekelezwa ipasavyo vitamkomboa Mtanzania na kuhakikisha kwamba nchi yetu inasonga mbele. (Makofi/ vigelegele)

Mheshimiwa Mwenyekiti, licha ya hivyo katika bajeti hii nitanukuu vitu vichache ambavyo tumeona angalau vinaweza vikasaidia Halmashauri zetu Mikoa yetu, Wilaya zetu, wananchi wetu wakasonga mbele kama tutatekeleza vile anavyotaka. Mheshimiwa Waziri amesema katika hotuba yake kwamba watahakikisha kwamba fedha ambazo zilikuwa zikitumwa katika Halmashauri mwishoni mwishoni, yaani kwa mfano mwezi Juni au Mwezi Mei wataniacha na wataziacha zitekelezwe lakini tunaomba Mheshimiwa Waziri mtuletee kanuni ili zikienda kule zisiende zikakae muda mrefu pia ili ziweze kutumika. Tunapongeza kwa hilo kwa sababu zilikuwa zikifika Juni na zinaondoka, kwa hiyo ilikuwa inaleta shida sana katika utekelezaji wa majukumu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia watu wamezungumza kuondoa ushuru wa nyasi bandia. Nasisitiza hili ni jambo jema kwa sababu tunakuza nyanja zote, ukikuza hata katika michezo hii itasaidia, lakini wasiishie mijini tunaomba Mheshimiwa Waziri waende mpaka vijijini, zile halmashauri ambazo zitaweza kuwa na viwanja wakanunua hizo nyasi basi wafanye hivyo, waliangalie wakati anakuja kuhitimisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi kupungua asilimia tano za mabango ya categories zote, hii ilileta shida sana, tukakuta kuna watu walianza sasa kuwa wanaweka kaa alama tu kadogo pale wakawa wanakosa kodi. Sasa kupunguza watu watalipa kodi na watapata mapato na kodi ikitolewa ndipo tutaweza kusonga mbele. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina mambo mawili pia ya kusisitiza katika hili. Kodi ya majengo wamesema itakuwa kupitia LUKU. Wamezungumza wengi hapa kwamba nyumba ikiwa na wapangaji wengi itakuwaje wataiwekaje sawa. Nataka wanapokuja kuhitimisha waniambie, kuna nyumba ambazo zinatumia solar, kuna nyumba ambazo zinatumia biogas, sasa hazina LUKU watapataje sasa kodi zake hapo? Mheshimiwa Waziri aje atuainishie namna ambavyo watapata kodi kupitia hii, kwa sababu siyo wote wana umeme na kuna maeneo mengine hakuna umeme. Kwa hiyo, waje na mkakati maalum wa kujua kwamba kama watachukua kwa kupitia LUKU watafanyaje, lakini waliweke sawa pia kwa sababu mwenye nyumba yupo, wakiwa wapangaji watupu pesa zile atakwenda kuchukua kwa wapangaji. Sasa hili watuwekee sawa hapa Waziri anapohitimisha ili tujue tunafanyaje katika hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye kodi ya mapato Pay As You Earn wamesema kiwango cha mwanzo hawatozi kodi, lakini kiwango kinachofuata kinatozwa kodi. Ukiangalia hii napongeza kweli wametoa asilimia moja safi kabisa, lakini haitoshi. Ukipiga mahesabu unakuta karibu tu ni Sh. 2,700. Sasa Sh.2,700 bado ni kidogo, ni ndogo sana. Kwa hiyo tuombe waiangalie vizuri kukata mzizi wa hili lote, tuwapandishie mishahara watumishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwapandishia mishahara watumishi, wataweza kulipa kodi, lakini pia ni motisha kwao kwa kufanya kazi kwa juhudi na vile vile wanaweza wakatoa kodi. Kwa hiyo Serikali itapata benefits humo kwa kufanya hivyo kwa sababu itawafanya wawe na moral kubwa kabisa ya kujenga uchumi wa nchi na vile vile kiinua mgongo kitapanda. Tunajua kabisa watu wanastaafu, viinua mgongo vinakuwa chini, wameona kwa miaka mitano watumishi hawakupandishiwa mishahara, kwa hiyo wakifanya hivyo wataondoa kero ambazo zinawaumiza sana Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mama amezindua kule Mwanza SGR kwa Mwanza. Sasa waharakishe basi ikamilike, kwa sababu kwa SGR tutaondoa mrundikano unaokuwepo pale Dar es Salaam. Kwa hiyo mizigo itakuwa inakwenda kwa haraka na uchumi utapanda. Hivyo, wakiweka mikakati mizuri wataweza kufika mbali na kuondoka kero za wananchi ambazo zipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa niende katika suala la kodi. Naomba Mheshimiwa Waziri anisikilize, mkoloni alikuja, alivyokuja hakuja na hela, alipokuja alikuja na wazo, alikuja na idea kwamba atafanya nini, kaikuta nchi ya Tanzania, akakuta kuna ardhi, alivyokuta kuna ardhi akaona hii ardhi itanufaisha watu kwa kilimo, kukawa na kilimo cha mkonge, katani na vitu kama vile. Akasema anatunga Sheria ya Kodi, kwa hiyo alivyotunga Sheria ya Kodi wananchi wao wenyewe waliinuka kwenda kufanya kazi pale ili waweze kupata pesa, watoe kodi na ndiyo hayo unayoyaona, tukachenjua barabara hizo mnazoziona, kodi ilitumika kujenga nchi, tukaweza kufanya mambo mengi sana ambayo yalifanyika kipindi hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hapa katikati tulilegalega, kodi inatolewa lakini mambo hayaendi, watu wakawa hawajui kodi inaenda kufanya nini. Sasa nimwombe Mheshimiwa Waziri, hawa watu wa Wizara wawe na mikakati maalum ya ukusanyaji wa kodi. Huu ukusanyaji usiwe wa kinguvu, iende ifike mahali wananchi wenyewe waone kwamba kutoa kodi inamlazimu, yaani akinunua kitu asitoe kodi yeye mwenyewe kwa maumivu. Hivi kweli unaletewa barabara nzuri, kuna maji safi na salama, una afya unapata madawa na nini hospitalini, nani atakataa kutoa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kila kitu kikionekana kinafanyika vipi, wananchi watakuwa tayari kutoa kodi. Kwa hiyo waende wakafanyie kazi. Naomba niwape mfano tu wa Rwanda; Nchi ya Rwanda walikuja na sera ya kuondoa majani kwenye nyumba zao, lakini lengo lao lilikuwa siyo kuweka bati pekee, ilikuwa pia ni kukusanya maji. Kwa hiyo, walisema tunaondoa nyasi watu waezeke kwa mabati, japokuwa hapa kwenye mabati Wizara wameongeza tozo, ili katika mabati yale wakusanye maji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa baada ya kupata maji, yale maji yakawa yanatiririka kwenye udongo, yanaharibu ardhi unakuwa mmomonyoko wa udongo, wakatunga tena sheria kwamba hakuna kutiririsha maji, kila mtu lazima hata awe na matuta mawili, matatu ya mboga kwenye nyumba zao. Kwa hiyo hii siyo tu kwamba mna-save vitu vingi, watu watapata vitamins kwenye mbogamboga, watu watapata maji, vile vile watu watapata pesa. Wale wanaouza gator zile watapata biashara, mafundi watapata kazi, kunakuwa na chain pale ya watu kupata ajira na fedha inapatikana. Kwa hiyo sheria ndiyo mzizi wa kila kitu wa kupata pesa na kupata kodi. Kwa hiyo, naomba waangalie, watuletee tuone ni zipi ambazo zitafuatwa ili Watanzania waweze kuona namna gani wataweza kujenga nchi yao kwa mapenzi, siyo kwa shuruti, ili tuweze kupata fedha za kuendeshea nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama hiyo haitoshi, kuna kitu kimoja naomba nishauri, kuna mapendekezo ya kodi kwenye laini za simu kutoka Sh.10 mpaka Sh.200 kwa siku. Maana yake ni kwamba mtu atalipa Sh.6,000 kwa mwezi na kwa mwaka Sh.72,000, lakini tumesema tunataka tuingie kwenye teknolojia. Naomba isubiriwe kwanza, siyo Watanzania wengi wanaomiliki hiki kitu na Mheshimiwa Rais ametoka kuzungumza siku mbili, tatu hizi, kwamba tuangalie tujifunze kwa wenzetu masuala haya ya teknolojia yakoje na sisi twende nayo. Kwa hiyo tukianza kutoza huku tutakimbiza Watanzania wanaoweza kumiliki simu, Watanzania ambao wanaweza wakafanya biashara na uchumi ukakua kwa kutumia simu. Kwa hiyo waliangalie suala hili linaweza likawa zuri, lakini linaweza likaathiri kwa upande mwingine wa ukuaji wa teknolojia ili tuhakikishe kwamba Watanzania na sisi tunakwenda kama nchi zingine zinavyokwenda. Kwa hiyo twende na sisi tukazidi kusonga mbele na kuleta maendeleo.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Grace.

MHE. GRACE V. TENDEGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. (Makofi)