Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

Hon. Aloyce Andrew Kwezi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Kaliua

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Hali ya Uchumi wa Taifa kwa Mwaka 2020 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 pamoja na Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, nikushukuru kwa kunipatia nafasi hii ya kuweza kuchangia, lakini kwa nafasi ya pekee naomba tu nianze kwa kuwapongeza sana Wizara ya Fedha kwa maana ya uratibu mzuri wa bajeti kuu.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba pia nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa nafasi ya pekee mama huyu kwa kweli ni msikivu sana na usikivu huo utauona kabisa, kwa mfano mimi katika bajeti iliyopita nilichangia sana kwenye masuala ya Utumishi nikaongelea stahili za Watendaji wa Kata pamoja na Wabunge wenzangu, tukaongelea stahili za Maafisa Tarafa na tukaongelea masuala ya promotion kwa watumishi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivi ninavyokwambia karibu halmashauri zote wapo busy kuendelea na upandishaji wa vyeo kwa watumishi. Sio hilo peke yake utekelezaji tumeuona kwa ile laki moja moja ambayo inakwenda sasa kwa Maafisa Tarafa na pia kwa Watendaji wa Kata. Siyo hilo peke yake bado kwa wale wastaafu tulilalamika hapa, tumeona mkakati ambao amekuja nao, Mheshimiwa Waziri na usikivu wa Serikali unaonekana moja kwa moja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo naomba nisimame nitembee kifua mbele na niwaombe wenzangu tutembee kifua mbele kwa kuamini kwamba, ushauri tunaoutoa ni shauri ambao unasikilizwa na unatekelezwa. Maana yake hakuna kitu kizuri unaposhauri halafu kikafanyiwa kazi na ndiyo maana ya Ubunge, tungekuwa tunashauri halafu msifanyie kazi, kwa kweli tungekuwa tunasema mbona ili tulilisema hakuna ambacho kimefanyika.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwaweli nimejisikia faraja sana, ndiyo maana narudia kumpongeza sana Mheshimiwa Rais kwa usikivu wake. Kwa namna hii naamini kabisa Watanzania wengi hata ukipita vijiweni wanajisikia furaha na amani kwa Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ni Serikali sikivu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niwapongeze kwa miradi ambayo inaendelea, ukifuatilia bajeti kuu miradi mikubwa yote ya kimkakati bado inaendelea na mama mpaka tunavyoongea yuko Mwanza ametoka kuzindua reli, lakini jana nimeona anazindua masoko ya dhahabu. Pakubwa zaidi ambapo amepalenga na ambapo ndiyo kilikuwa kilio kikubwa cha Wabunge ni suala kubwa la TARURA. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Mwigulu Nchemba sitaki nimpongeze kwa namna ya kuuma ulimi, nampongeza hapa akiwa ananiangalia kwamba kazi aliyoifanya na ushauri aliofikisha Mwenyezi Mungu ambariki sana, kwa sababu kwenye TARURA mazao ya wananchi wote wanafahamu yanauzwa bei ya chini kutokana na barabara. Mwananchi anatoka na mzigo wake kule wa mahindi, vitunguu, nyanya na alizeti, anakutana na barabara hakuna daraja, hakuna karavati na maji yapo kiunoni. Kwa hiyo matokeo yake yananunuliwa mazao yao kwa bei ya chini.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo kwa alternative hii ambayo waekuja nayo, naomba niwapongeze sana na wasimamie hilo. Wasimamie hilo ili waturahisishie sisi kujibu maswali, maana yake tukimaliza Bunge hapa tutakuwa kwenye majimbo yetu, tutakuwa kwenye mikoa yetu, kwa hiyo itakuwa ni fursa nzuri ya kuwaambia nini ambacho tumekisema na nini ambacho Serikali sikivu imetekeleza.

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo kubwa lingine ambalo nimeliona hapa na ni lazima niliseme kwenye Kamati yetu ya Ardhi, Maliasili na Utalii. Pale kwenye utalii nimefurahishwa sana kwasababu tulikuwa tunapata wasiwasi kwenye Kamati kwamba utalii ni sekta ambayo inatuingizia fedha za kigeni, lakini baada ya kuondoa yale mapato yanaenda moja kwa moja kwenye Mfuko Mkuu ule, tukawa na wasiwasi watatuzoroteshea maendeleo ya utalii. Sasa niwaombe kwasababu wanatoa in advance labda miezi miwili, wamefanya akili ya ziada sana, kwa hilo nawashukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, bado nawaomba jambo kubwa kwenye mapato yetu ya ndani, ni lazima zaidi ya hapa tuimarishe sehemu gani kwenye utalii. Kwenye utalii, katika hifadhi zetu kuna maeneo au hifadhi wakati wa masika hazifikiki kabisa. Sasa tunahamasisha Watanzania waende kwenye maeneo ya hifadhi, naomba nitoe mfano wa Kitulo National Park, tulitaka kwenda pale Kitulo tukaambiwa kwa muda huu wa mvua, Kitulo barabara haifikiki. Pia tukataka kwenda kuna Ziwa moja linaitwa Ngosi ikashindikana, sasa hizo ni sample mbili, lakini nilikanyaga Biharamulo kuingia kule Burigi ikawa na yenyewe kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa naomba hapa tushauriane vizuri, tunahitaji fedha kwa ajili ya maendeleo ya nchi yetu na kwa ajili ya miradi, nashauri tu-inject fedha nyingi kwenye kuboresha miundombinu ile ya kwenye hifadhi zetu ili hata kama ni masika watu wanataka kwenda Christmas kupumzika mwezi wa Tatu wanataka kwenda mle, pamoja na sikukuu zetu hizi za kuchinja, wawe na uwezo wa kwenda kule kula vitu vyao vizuri wakati wa masika na wakati wa kiangazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine ambalo ningeweza kuwashauri, kwenye sekta ya afya nafahamu kabisa ziko kata hatujakamilisha shule na zipo tarafa ambazo hatuna vituo vya afya, hebu tujaribu kwenye hizi fedha ambazo wameangalia, nafikiria tuwabane kidogo, unajua unapoenda kutoa fedha kwenye M-pesa, kwenye Halopesa, kwenye Tigo pesa na kwenye Airtel Money, kama unatoa milioni moja au unatuma milioni moja unakatwa labda 3,500 au 4,000. Unapokwenda kutoa unakatwa tena 8,000/=.

Mheshimiwa Naibu Spika, naomb tujaribu kuangalia hapo je, hatuwezi kuongea na makampuni yetu, yalipe kodi kama kawaida maana yake tusichezee kodi, lakini bado tuangalie ile fedha ambayo ilikuwa inapotea pale kwenye zile transactions, naona ile fedha ni kubwa. Yaani muamala nimekutumia hapo Mheshimiwa unaupokea, mimi niliyetuma nakatwa, wewe ukinyanyuka kwenda kutoa unakatwa karibu 8,000 mpaka elfu 10,000 na zaidi. Sasa ile fedha ni nyingi, kwa nini tusiongee, kwa sababu ni suala la uzalendo na wana- exist nchini kwetu na tunafanya nao kazi, tuwashawishi kwamba if possible, basi angalau na wenyewe wajaribu kuachia shilingi elfu moja moja ziende kwenye TARURA, kwa sababu barabara za vijijini ndiyo mishipa ya uchumi wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, tukitaka tuyapunguze maneno mengi ni hapo ambapo tumelenga kwenye TARURA, afya, elimu na maji. Haya maeneo tukibana vizuri, naamini kabisa mwelekeo wetu utaendelea kuwa vizuri na kama nchi tutaendelea kutembea kifua mbele kwa kuhakikisha tunawasaidia wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, jambo lingine kubwa naendelea kupongeza ni la Madiwani wetu, nawaambia kabisa by professional mimi ni Afisa Utumishi, kwa hiyo nimekaa halmashauri karibia miaka 15 ninachokiona…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ndiyo ya kwanza?

NAIBU SPIKA: Malizia sentensi yako unachokiona…

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, ninachokiona ambacho ningekishauri, inawezekana kuna halmashauri ambazo wakawa na wasiwasi kuwalipa moja kwa moja, naomba kupitia ule Mfuko Mkuu wajaribu kuziangalia zenye uwezo mkubwa sana, ndiyo iwe hivyo kwa maana yale majiji makubwa yenye fedha, lakini hizi halmashauri zingine zote zinasuasua, wahakikishe wanawalipa kupitia hii Serikali Kuu moja kwa moja, kusiwepo kwamba hiki na hiki, zile za daraja A, zile halmashauri kama Kinondoni hapo sawa.

NAIBU SPIKA: Haya ahsante sana Mheshimiwa.

MHE. ALOYCE A. KWEZI: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba nikupongeze sana na naunga mkono hoja, ahsante sana. (Makofi)