Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuchangia katika Wizara hii muhimu ya Maliasili. Kwanza kabisa nianze kwa kuwapongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa jinsi ambavyo wameendelea kufanya kazi vizuri katika Wizara hii. Hata hivyo, kipekee sana nampongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara hii.

Mheshimiwa Naibu Spika, kutokana na uchache wa muda, moja kwa moja nitaanza kwa kuchangia kwa Mkoa wangu wa Katavi kuhusiana na suala la TFS kutokana na tozo mbalimbali ambazo wamekuwa wakizitoza kwenye vitu vinavyotengenezwa kwa mbao.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Mkoa wetu wa Katavi, TFS wamekuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa wananchi. Huwezi kuamini, mfano mwananchi anaponunua kitanda chake pale Mpanda Mjini na anataka akipeleke katika Wilaya ya Mlele, Halmashauri ya Mpimbwe, kumekuwa na tozo mbalimbali ambazo zimekuwa kama double payment.

Mheshimiwa Naibu Spika, mfano, juzi tu hapa kuna wananchi ambao wamenunua vitanda vyao na meza Mpanda Mjini na wanavipeleka katika Halmashauri ya Mpimbwe. Vitanda hivi, huyu mtumiaji anakuwa ameshalipia na amepata risiti lakini wanavyopita kwenye mageti wanatozwa tena pesa na watu wa TFS wakiambiwa tena walipie gharama za vitu hivyo. Hii imekuwa ni kero kubwa sana kwa wananchi wa Mkoa wa Katavi. Nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aje ashughulikie suala hili kuangalia tozo hizi, ikiwezekana ziondolewa kwani wananchi hawa wamekuwa wakipata adha kubwa na watu hawa wa TFS. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kumekuwa kuna migogoro mbalimbali baina ya wananchi na TFS kwa mfano, katika Wilaya ya Mlele Kata ya Kamsisi; kumekuwa na mgogoro mkubwa baina ya watu hawa na mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu, wananchi wamekuwa wakichomewa nyumba zao, wananchi wamekuwa wakichomewa mazao yao, lakini pia TFS hawa wamediriki kabisa kuwachomea hata maduka wananchi, wananchi hawa wamefanyiwa ukatili, mgogoro huu umekuwa ni wa muda mrefu na Mheshimiwa Waziri tumekuwa tukimwambia mara nyingi na hata Hayati Dkt. John Pombe Magufuli alikuwa anafahamu suala hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tunaomba sana Serikali yetu sikivu iweze kushughulikia mgogoro huu ili wananchi hawa waweze kuishi kwa amani, kama tunavyojua ardhi haiongezeki, lakini wananchi wanaongezeka, tuombe sana tuangalie mgogoro huu, ikiwezekana kabisa tuumalize mgogoro huu kwani wananchi hawa wamekuwa wakipata adha, mama zangu na baba zangu wa Kijiji cha Kamsisi, Kata ya Utende, maeneo ya Ilunde na Ilela wamekuwa wakichapwa sana, wakiadhibiwa, wakiambiwa kwamba wanaingilia maeneo ambayo ni ya mapori. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri waje washughulikie suala hili, ikiwezekana waje katika Mkoa wetu wa Katavi,waweze kufanya ziara, waje wawasikilize wananchi, wasiwe wanasikiliza tu watendaji wakati mwingine imekuwa ikipotoshwa. Hivyo, waje wafanye ziara kule wajihakikishie wajue je, mwenye kosa ni mwananchi au wenye kosa ni watu hawa wa TFS. Niwaombe sana Wizara wafanye ziara kule ili waweze kujua nini chanzo cha tatizo hili na ikiwezekana tulimalize ili wananchi wetu waweze kuishi kwa amani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, vile vile kumekuwa kuna tatizo la kubambikiziwa kesi. Watu wa TFS wamekuwa na tabia ya kuwambambikizia kesi wananchi wale wanaoizunguka Katavi National Park. Sasa tunachotaka wananchi wale wa Katavi waweze kufurahia kuwepo kwa Katavi National Park hifadhi ambayo Mwenyezi Mungu ameibariki na siyo waone ni kero kuwa karibu na hifadhi hiyo. Wamekuwa wakibambikiziwa kesi mbalimbali, wakiambiwa kwamba wengine wamekutwa na nyara za Serikali, wengine wamekutwa sijui na nyama za pori kama hizi za Nyati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nimwombe sana Mheshimiwa Waziri aje katika maeneo hayo atafanye ziara aangalie kesi hizo hasa zile ambazo zimekuwa hazina vithibitisho, ikiwezekana ziondolewe. Wananchi wa vijiji hivi wamekuwa wakihangaika, wananchi wa Vijiji vya Majimoto, Mamba, Chamalendi na Mwamapuli wamekuwa wakiteseka sana. Hivyo nimwombe sana Mheshimiwa Waziri afanye ziara Mkoa wa Katavi, tunataka wananchi wa Mkoa wa Katavi wafurahie kuwepo kwa Katavi National Park na siyo hifadhi hiyo iwabugudhi wananchi. Wananchi tunawapenda na hifadhi pia tunaipenda kwa sababu inatuingizia mapato. Tunachotaka tu ni kwamba migogoro hiyo ikiwezekana iishe na hasa hiyo migogoro na kesi ambazo hazina uthibitisho. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)