Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

Hon. Joseph Anania Tadayo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mwanga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Maliasili na Utalii

MHE. JOSEPH A. THADAYO: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana kupata nafasi hii la kwanza niungane na wenzangu kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri Katibu Mkuu pamoja na timu nzima ya Wizara kwa dhamana kubwa hii ambayo wamekabidhiwa ya Wizara hii nyeti kwa ajili ya mapato ya nchi yetu ajira na kuitangaza nchi yetu nje. Wanafanya kazi nzuri na kwa kweli tuna kila sababu ya kuwapongeza.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali yetu ya Awamu ya Tano na ya Sita imetumia nguvu nyingi sana katika kutangaza utalii jambo ambalo hapo kale pengine halikuwahi kufanyika sawasawa na kwa sasa naamini kabisa kwamba duniani hakuna asiyejua kwamba Kilimanjaro iko Tanzania, Olduvai Gorge iko Tanzania na Fukwe za Zanzibar zenye Dolphins wengi ziko Tanzania, pamoja na Serengeti.

Mheshimiwa Naibu Spika, katika hili pia tuipongeze Bodi ya Utalii chini ya Mheshimiwa Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, walionekana kabisa kuwa kutumia nguvu ya ziada kwenye hili, tunawapongeza sana. Juhudi hizi zisipunguzwe kwa sababu washindani wetu bado wako kazini. Hii ni sawasawa tu na vita ya kiuchumi, kwa hiyo tuendelee kujitangaza kwa nguvu.

Mheshimiwa Naibu Spika, nisiache kuzungumzia suala la tembo kwa sababu Jimbo langu la Mwanga liko katika mazingira magumu zaidi kwa sababu liko katikakati ya mbuga mbili, upande mmoja kuna Mbuga ya Tsavo ya Kenya na upande wa pili kuna Mbuga ya Mkomazi. Naishukuru sana Wizara, Naibu Waziri alitutembelea. Alifanya kazi nzuri sana na kwa kweli niwashukuru wananchi wangu wa Mwanga pamoja na viongozi wote wa Chama na Serikali, walijitokeza kwa wingi na kimsingi wananchi wa Mwanga wamekubaliana na wito wa kuwa wadau wakubwa sana wa hifadhi na kazi inaendelea vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo matatu ambayo wananchi wa Mwanga wanayatarajia. La kwanza, ni kuongezewa idadi ya Askari wa Wanyamapori ili angalau waweze kuvuna vile walivyovipanda na pia watoto waweze kwendaa shule, ahadi hiyo ilitolewa na tunaamini itatekelezwa. La pili, ni kufungua lile lango la la Kaskazini kwenye Mbuga ya Mkomazi kwenye maeneo ya Kata ya Toloha, ambayo kwa kweli wananchi wa Mwanga wanaisubiri kwa hamu na wameshajiandaa kwa ajili ya fursa za biashara zitakazotokana na lango lile la pale. La tatu, ni kwamba bado wananchi wa Mwanga wanaona kwamba watafiti wetu, Vyuo Vikuu vyetu pamoja na wataalam bado wanacho cha kutuambia juu ya tatizo hili la tembo.

Mheshimiwa Naibu Spika, yako mambo ambayo Serikali imefanikiwa tu, kwa mfano; tatizo lile la majani yaliyokuwa yanaota kwenye mbuga ambayo siyo mazuri, yalimalizwa kitaalam na kitafiti na hali inaendelea vizuri sana. Sasa kwa vile tumeshajua kwamba kinachowatoa kule tembo ni nini kuwaleta huku, basi tuwajengee mazingira ili waendele waweze kuendelea kukaa kule. Kama yako aina ya malisho ambayo inawafanya watoke kule, naamini yanaweza yakapandikizwa huko huko kwenye mbuga ili waendelee kukaa kule. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia liko suala la matumizi ya electronic fence ambacho taarifa nilizonazo ni kwamba pale Tsavo National Park wenzetu wameweka electronic fence upande unaoelekea kwenye maeneo ambayo hawataki tembo waende, ndiyo maana wanakuja kwa wingi huku. Hata ukienda Amboseli National Park kuna maeneo mawili wametumia electronic fence moja linaitwa Namelok, ambalo limefanikiwa sana na fence nyingine inaitwa Kinama bado inachangamoto, lakini inaendelea kufanyiwa kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachoamini ni kwamba watafiti wetu; Vyuo vikuu vyetu na wataalam wetu, wakiingia kazini sawasawa, bado tunao uwezo mkubwa sana wa kuweza kupata suluhisho la kudumu kuliko kutegemea hizi measures ambazo ni kama za dharura za kushughulikia jambo kama hili.

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa nasoma utafiti wa Cambridge University kwenye journal yao moja online, wanasema hata suala la kutumia nyuki bado lina changamoto, tena walifanyia utafiti mwaka 2018 kwenye Hifadhi ya Udzungwa, bado lina changamoto. Kwa hiyo nadhani, watafiti wetu wanapaswa kuingia kazini zaidi ili kusaidia juhudi hizi za Serikali nazo zifanywe katika kuzuia hili tatizo.

Mheshimiwa Naibu Spika, sina zaidi ya hapo, naunga mkono hoja, Wizara inafanya kazi nzuri, Serikali iwape fedha walizoomba ili waweze kutekeleza majukumu yao. Ahsante sana. (Makofi)