Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Sebastian Simon Kapufi

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Mpanda Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. SEBASTIAN S. KAPUFI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Nianze kwa neno la shukrani kwa Mheshimiwa Waziri na timu yake. Ni kweli Mheshimiwa Waziri ni mtu rahimu. Mimi niseme hadharani kwa zaidi ya mara mbili nilipokuwa na udhuru na yeye alipotembelea jimbo langu, alifikia hatua ya kupiga simu akaniunganisha na wananchi wangu. Huyu ni mtu muungwana, namshukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba shukrani nyingine ziende kwako wewe. Bunge lililopita uliunda Kamati Teule ya Bunge ya kukushauri kuhusu suala la gesi na mimi nilikuwa mmoja kati ya Wajumbe uliowachagua. Rai yangu ni nini? Naomba Serikali iendelee kufanya rejea kwenye taarifa ile kubwa na kuona ni mambo gani tuliyoishauri Serikali. Nashauri sana katika hilo. Katika masuala yote ya gesi ujumbe mzima uko pale, kwa hiyo Serikali iendelee kufanya rejea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mara ya mwisho Waziri alikuwa Uganda wakati Rais wetu na Rais wa Uganda walipokuwa wakitia saini moja ya mikataba. Nilijifunza mambo kama matatu na mambo hayo yalinifanya nipate wivu lakini wivu ambao ni chanya. Rais Museveni alisema mafuta ni jambo la kupita tu, linaweza likawa jambo la muda, lakini utajiri huo uwasaidie kwenda kufanya sekta nyingine kama kilimo, utalii na mambo mengine ya namna hiyo. Pia aliwasimamisha vijana akasema ugunduzi ule umefanywa na Waganda wenyewe, vijana ambao waliwapeleka shule wakasoma. Akasema pia eneo ambalo limechimbwa ni asilimia 40 bado asilimia 60. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi suala hili limenitia wivu wa maendeleo. Watanzania tunajifunza nini kutoka hapa? Je, tuna mpango gani wa makusudi wa kuhakikisha vijana wetu ama kupitia shule au na mambo mengine kwa sababu wao watakuwa na uzalendo kufanya kazi hizi? Mtu mwingine anaweza akaenda kufanya utafiti hapa na akakuta labda kuna mafuta na kwa sababu ya masuala ya kiuchumi asikupe taarifa sahihi lakini kwa wale ambao ni wazalendo, kama walivyofanya wale vijana wa Uganda hawatafanya hivyo. Naomba tuendelee kujifunza kutoka kwa wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, najua kuna maeneo kama Eyasi, Wembele ambapo jitihada zinaendelea lakini twende mbali zaidi. Sisi kule Tanganyika, kwa maana ya Mkoa wangu wa Katavi, utafiti umekuwa ukiendelea katika bonde lile. Ni vizuri basi tukaongeza kasi ya kuendelea kufanya tafiti katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, nikitoka hapo nirudi tena kwa Mheshimiwa Waziri. Pamoja na sifa nilizokupa za kutembelea maeneo yangu, changamoto ambayo naipata mimi katika eneo langu, nasomeka niko Manispaa lakini umbali wa kijiji cha mwisho watu wa TANESCO wanasema wao ndiyo watashiriki na siyo suala la REA wakati huo wale watu wanasomeka wako kijijini. Kwa mfano, ukienda Kata ya Mwamkulu, japo inasomeka mitaa lakini ni vijijini; maeneo kama Mkwajuni, Kabwaga, Mkokwa, Nguvumali na Seso. Ninayo pia Kata ya Kasokola maeneo ya Kasolwa, Ivungwe na Isungamila.

Mheshimiwa Spika, mwisho ninalo eneo la Kakese, kuna eneo linaitwa Kamakuka. Mheshimiwa Waziri, ni shahidi, mara ya mwisho alikuja pale na akatusaidia kuhakikisha umeme unafika hata kwa maeneo yale yanayowagusa wachimbaji. Katika hilo mimi nakushukuru sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, eneo la mwisho ambalo napenda kulizungumzia tuliambiwa ongezeko la mapato lilikuwa ni pamoja na suala la LUKU. LUKU ilivyokuwa ikitumika vizuri ilifanya TANESCO wafanye vizuri. Tuliambiwa mara ya mwisho kulikuwa na shilingi bilioni 72 katika mwaka 2016 kwa mwezi, lakini mwaka 2021 ilikuja shilingi bilioni 160 kwa mwezi na hii yote ilikuwa asilimia 102. Sasa kama LUKU ilisababisha TANESCO wakapata matokeo mazuri na kipato kikapanda, hii juzi tumeona LUKU ikichezewa; wanataka kuleta ujumbe gani? (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, nakushukuru kwa nafasi, naunga mkono hoja. (Makofi)