Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Seif Khamis Said Gulamali

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Manonga

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi kuchangia katika Wizara hii ya Nishati. Binafsi niipongeze Serikali ya Awamu ya Tano pamoja na Serikali ya Awamu ya Sita kwa kazi kubwa waliyoifanya kwenye sekta hii ya umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, usambazaji wa umeme kwenye nchi yetu ndani ya vijiji vya Tanzania kumeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza Afrika kusambaza umeme vijijini. Tanzania tumesambaza umeme kwa zaidi ya asilimia 90, kwa Afrika tumeshika nafasi ya kwanza kwa kuweka umeme kwenye vijiji vyetu. Ni jambo zuri, la kupongezwa na kwa kweli Mawaziri hawa wanastahili pongezi na pongezi hizi ni haki yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunatambua changamoto zilizopo za kukatika kwa umeme karibu nchi nzima. Tumuombe tu Waziri na timu yao wajipange kwa sababu tatizo la ukatikaji wa umeme lipo karibu katika kila eneo hata Igunga na sehemu nyingine. Kwa hiyo, pamoja na kupeleka umeme kwenye vijiji karibu vyote nchi nzima lakini uimara au stability ya umeme imekuwa ni tatizo.

Kwa hiyo, tuwaombe waliangalie suala hili kwa umakini mkubwa ili kuondoa tatizo la ukatikaji wa umeme katika maeneo mbalimbali. Kwa mfano, Igunga maeneo mengi ni majaruba, nguzo zile zinawekwa kwenye majaruba kila siku ni service. Kwa hiyo, kwa sababu Serikali iko kwenye project ya kutengeneza nguzo za zege, naomba zipelekwe kwenye maeneo ambako kuna majaruba kwani hizi nguzo za mbao hazina uhimilivu. Kwa hiyo, niwaombe walifanyie kazi suala hili kwa umakini zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala lingine ambalo nataka nichangie ni la vinasaba. Kwanza niipongeze Serikali kwa kulichukua suala hili na kulipeleka Serikalini na kuliondoa kwa wakandarasi ambao walikuwa wamejipa kazi hii. Hizi zilikuwa ni kampuni mbili za tajiri mmoja; mmoja anauza material kwa kampuni nyingine na kampuni nyingine inaiuzia Serikali au inafanya kazi ya kuweka marking kwenye mafuta. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa nini vinasaba? Tulikuwa tunaweka vinasaba kwenye mafuta yetu kwa sababu sisi ndiyo port tunapokea mafuta ya ndani ya nchi yetu na nchi jirani. Kwa hiyo, mafuta haya yanapoingia unashindwa kujua ya kwetu ni yapi na ya nchi jirani ni yapi. Kwa hiyo, ili kuondoa ukwepaji wa kodi ndiyo vinasaba vikatumika kuwekwa kwenye mafuta tunayotumia ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Spika, hata hivyo, kulikuwa kuna ujanja mwingi ukifanyika katika suala hili la uwekaji wa vinasaba. Mafuta mengine ambayo yalikuwa yakienda transit yalikuwa yanatumika ndani ya nchi na wanaweka vinasaba na maisha yanaendelea na wafanyabiashara wanapata pesa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa sababu suala hili limepelekwa ndani ya Serikali, umakini na uzalendo mkubwa sana unahitajika ili kuondoa ubadhirifu na ujanjaujanja utakaokuja kutokea kwa watumishi wa Serikali ili kuondoa ukwepaji wa kodi kwa wafanyabiashara kwenye sekta hii ya mafuta. Niombe sana Waziri wa Viwanda, EWURA isimamie na isishirikiane na watumishi ambao siyo waadilifu. Ni lazima hapa tukubaliane, pamoja na kuiondoa kwa wakandarasi tumerudisha Serikalini, uzalendo unahitajika. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, bahati nzuri tumechukua watumishi wale tumewaingiza Serikalini kwa ajili ya kutuongezea ujuzi lakini pia ndio waliokuwa wanafanya kazi hii. Ni lazima tuwafuatilie kwa ukaribu Zaidi, tusiliache jambo hili hivi hivi. Pamoja na wao kufanya tusiache liende tu ni lazima tuwafuatilie ili kudhibiti mianya ya upotevu wa kodi ya Serikali.

T A A R I F A

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Nakuruhusu, taarifa.

MHE. BONIPHACE M. GETERE: Mheshimiwa Spika, nataka kumpa taarifa mzungumzaji kwamba asubuhi ya leo nimekwenda kuweka mafuta hapa Dodoma yameongezeka kwa Sh.80 kutoka Dar es Salaam kuja hapa, yaani siku hizi ni kila siku mafuta yanaongezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukitaka kutazama suala hili na mimi naliangalia mara mbilimbili; duniani kote mafuta hayatumiki kwa sababu ya Corona maeneo mengi biashara hazifanyiki, mafuta mengi sasa hivi yamekwama kule yanakuja huku ndani lakini Tanzania mafuta yanaongezeka bei, nadhani kwa sababu ya vinasaba, mimi nina mashaka nalo hili. (Makofi)

SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, anachokisema Mheshimiwa Getere ni kweli; kuna ongezeko la haraka na kubwa sana la bei ya mafuta hivi sasa. Labda Mheshimiwa Waziri atatuambia baadaye kidogo tatizo ni nini. (Makofi)

Endelea Mheshimiwa Gulamali.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, taarifa naipokea lakini kwa uelewa ni kwamba kila tarehe za mwanzo za mwezi mpya EWURA wanapanga bei mpya kulingana na bei ya soko la dunia. Ila nachoomba ni kwamba waangalie bei hizi zisije zikaathiri mzunguko wa uchumi wa nchi yetu. Kwa mfano, bei iliyopanda juzi kwa Dodoma hapa ilikuwa ni Sh.1,800, ime-shoot mpaka Sh.2,300. Kwa hiyo, ni kiwango kikubwa sana cha upandaji wa bei. Niziombe Wizara hizi kwa sababu najua bei zinapangwa na watu wa EWURA na EWURA iko Wizara ya Maji...

T A A R I F A

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, taarifa.

SPIKA: Taarifa, endelea hapo ulipo.

MHE. CHARLES J. P. MWIJAGE: Mheshimiwa Spika, napenda nimpe taarifa Makamu Mwenyekiti wa Kamati inayohusika kwamba mfumo huu wa kuagiza mafuta wa Tanzania umerejewa kwenye bei za dunia na bei zetu ni mwezi tuliomo toa mwezi uliotangulia.

Kwa hiyo, kadri bei za dunia zitakavyopanda, sisi ni price taker, hatuna ujanja lazima tufuate kanuni bei ipande au ishuke. Hata hivyo, bei hupanda na bosi wangu wa zamani anajua, kuna contango na backwardation. Kwa hiyo, sisi price taker hatuna ujanja.

SPIKA: Japo hatuna ujanja lakini ile trend ni ya ghafla na ni kubwa mno, ndiyo maana kwa binadamu wa kawaida atahitaji maelezo fulani tu. Mkiangalia hivi karibuni bei imepanda sana, tukiambiwa ni World Market nalo ni jibu pia lakini ni vizuri kujua kuna nini kwa sababu zimepanda sana. (Makofi)

Mheshimiwa Gulamali, malizia.

MHE. SEIF K. S. GULAMALI: Mheshimiwa Spika, mwisho katika mchango wangu, naomba kuzungumzia usimamizi wa flowmeter yetu. Naomba ikiwezekana pale tujenge ukuta kama wa Mererani, tuweke ukuta na kufuli kubwa na funguo wapewe Waziri na Katibu Mkuu ili kulinda wizi na uchezeaji wa flowmeter pale bandarini. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Spika, ahsante kwa nafasi, nawasilisha mchango huo. (Makofi)