Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Athumani Almas Maige

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Tabora Kaskazini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ATHUMAN A. MAIGE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kupata fursa hii ndogo, tuko wengi tunagombania muda huu. Mimi nitajikita kwanza kutoa shukrani kwa Wizara hii na Serikali yetu lakini pia malalamiko kidogo kwenye jimbo langu.

Mheshimiwa Spika, nashukuru sana Serikali ya Awamu ya Tano na ya Sita kwa mradi huu mkubwa wa REA na hasa hasa kueneza umeme nchi nzima. Vilevile kujiandaa kuwa na umeme wa kutosha kwa kuleta miradi mingi ya kuzalisha umeme na baba yao ni Mradi mkubwa wa Mwalimu Julius Nyerere kule Rufiji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Wizara hii si kwamba ameivaa Mheshimiwa Kalemani, Mheshimiwa Kalemani amevaliwa na Wizara hii. Mheshimiwa Kalemani Wizara hii anaichukua kama familia yake. Mimi kwangu tulipoanza uongozi hapa mwaka 2015 hapakuwa hata na kijiji kimoja chenye umeme jimboni kwangu. Kwa kujua hilo, huyu Waziri amekuja jimboni kwangu mara nane. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuna wilaya saba Mkoani Tabora. Kote mradi ulikuwa unaenda vizuri lakini Jimbo la Tabora Kaskazini halikuwa hata na kijiji kimoja chenye umeme, leo tuna vijiji 32 vina umeme. Alikuwa anasikiliza maoni ya wananchi wangu anatoka machozi, hili si jambo la kawaida kwa Waziri kuumia kama vile wale ni familia yake yeye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaambieni alipita jimboni kwangu kuzindua umeme REA III sehemu ya pili siku saba kabla ya kumpoteza Mheshimiwa Rais aliyetangulia mbele za haki. Hii ni kuonyesha kiasi gani alikuwa na uchungu wa kufanya kazi akijua kwamba ana matatizo ya familia yake, lakini akaweka familia ya Watanzania wote mbele. Huyu ndio Waziri Kalemani nayetaka kumtaja leo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, matokeo yake vijiji 12,000 vimepata umeme kutoka vijiji vichache vilivyokuwepo mwaka 2015 bado vijiji 1,900 na kitu basi nchi nzima iwe ya umeme. Ameitoa nchi hii kule chini kwa umeme leo ni nchi ya kwanza katika Afrika kuwa na umeme. Huyu ndiyo Waziri ninayesema Wizara imemvaa naye kaivaa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Jimbo langu tuna vijiji 96 Jimbo zima, 32 vina umeme na 64 havina umeme. Hata hivyo, kwa imani kubwa niliyonayo kwa Mheshimiwa Waziri ameshakuja na kuzindua REA III round II pale kijijini kwetu Kanyenye na kutoa ahadi kwamba vijiji vyote vilivyobakia vimo katika REA III round II na wilaya yote ya Uyui imepewa vijiji 100 vitakavyopatiwa umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, licha ya hivyo tulikuwa tumebakiwa na vijiji vitatu kujumuisha vijiji vyote vya Wilaya ya Uyui. Alipokuja tumeongea naye na wakandarasi wote tumekubaliana vijiji vile vitano vilivyobakia vimo pia katika mpango huu wa REA III round II. Kwa hiyo, mimi nina imani kwamba baada ya mwaka 2022 kama tunavyosema miezi 18 Jimbo langu na Wilaya yote ya Uyui itakuwa na umeme. Hili si jambo dogo, nimesimama hapa kuishukuru Serikali ya Awamu ya Tano na Awamu ya Sita kwa kazi nzuri inayofanya. Tusingoje mtu fulani afariki ndipo tumpongeze tunampongeza Mheshimiwa Kalemani yuko hai na anatusikia amefanya kazi nzuri. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la usalama wa mitambo inayoitwa Business Continuity Planning. Mitambo hii inafanya kazi kila siku lakini lazima kuwe na mbadala wake. Tumepata tatizo sana la LUKU wiki tatu zilizopita ilipoanguka awamu moja waliyonayo ya kuendesha mitambo hawakuwa na awamu ya pili jambo hilo limeleta mushkeli. Naomba waangalia kuwa na mitambo mbadala.

Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana. (Makofi)