Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

3

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipatia nafasi. Mimi kwanza napenda kuchukua fursa hii kumpongeza sana Mheshimiwa Waziri, yeye na timu yake kwa kazi nzuri wanayofanya, Mwenyezi Mungu awabariki sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mimi kwa Jimbo langu la Maswa Mashariki na Maswa nzima kwa ujumla kwa kweli tatizo la kukatika umeme limekuwa sugu. Kila siku tunasikia mipango mizuri na nini lakini hatuoni juhudi ya kuondokana na kero hii ya kukatikakatika kwa umeme. Kwa hiyo, nakuomba sana Mheshimiwa Waziri mfanye basi jitihada za ziada ili kuweza kuondokana na kero hiyo.

Mheshimiwa Spika, vilevile kuna vijiji vyangu vingi ambavyo havina umeme. Tumeona mradi wa REA umefanya kazi vizuri sana lakini wamefanikiwa kufikisha umeme kwenye Makao Makuu ya Kata, tunakubaliana na hilo, hata hivyo, vijiji vya pembeni mwa kata hizo havina umeme. Kwa hiyo, katika records zetu zinaonesha kama vile kata zote Wilaya ya Maswa zimepata umeme lakini ukiangalia vijiji vya pembeni mwa kata hizo hakuna umeme.

Kwa hiyo, tunaomba sana msifikishe tu umeme kwenye kata basi mpeleke na vijijini, maeneo ya pembezoni mwa kata hizo. Kwa mfano pale Maswa kuna Kijiji cha Jilago, Mwabadini, Mbugamita, Mbalagane, Chugambuli, Mwabalogi, Mlimani, Mwabalatulu, Mwamashindike, Ikungulyankoma, kote huko tunaomba umeme ufike jamani. (Makofi)

SPIKA: Yaani majina hayo, sijui urudie tena ili Waziri aandike? Endelea Mheshimiwa. (Kicheko)

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, naomba nirudie; Jilago, Mwabadini, Mbugamita, Buhangija, Chugambuli, Mwabalogi, Mlimani, Mwafumbuka, Mwabalatulu, Ifungilo, Mwamashindike na Ikungulyankoma. Mheshimiwa Kalemani atakuwa amenielewa vizuri sana, tunaomba umeme ufike tumetoa ahadi siku nyingi. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nichukue tena fursa hii kukushukuru na kukupongeza wewe na Mheshimiwa Waziri kwa uamuzi wenu mliouamua wa kupeleka ile huduma ya vinasaba kwenda TBS. Pamoja na kwamba Mheshimiwa Spika umeshaamua na Wabunge tumeshaamua kwamba tubadilishe sheria, lakini kuna data fulani napenda Watanzania waielewe; tunapopeleka huduma ya vinasaba TBS kuna advantage kubwa sana.

Mheshimiwa Spika, nimezunguka kuna watu wengine mpaka wakawa wananiuliza tena wengine mpaka Wabunge wanakuuliza, hivi vinasaba ni nini? Vinasaba kwa lugha nyepesi ni rangi ya kutia kwenye mafuta na uamuzi huu tuliuamua mwaka 2010. Mafuta yanapotoka bandarini kuyatofautisha na mafuta yanayokwenda nchi za jirani ilibidi mafuta yetu tuyatie rangi, ni uamuzi mzuri sana ili kuepukana na yale mafuta yanayokwenda nje ya nchi kushushwa njiani. Hata hivyo, kitendo kinachofanyika kwa kweli kilikuwa kinafedhehesha sana kwa sababu bado mafuta yalikuwa yanashushwa njiani na kwa sababu vinasaba vilikuwa vinamilikiwa na mtu binafsi ilikuwa rahisi kuwauzia watu wengine kisha wanaenda kutia ile rangi kwenye mafuta ambayo yako on transit. Tunawashukuruni sana kwa uamuzi huu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa harakaharaka hii Kampuni ya Global Fluid International (GFI) tunakubaliana walikuwa wanalipa kodi lakini naomba nikutaarifu kodi waliyolipa mwaka 2020, corporate tax, ilikuwa ni shilingi bilioni 1.86 tu na VAT walikuwa wanalipa wastani wa milioni 650 kila mwezi. Mafuta yanayopita kwa siku tuna wastani wa lita milioni tisa, wana-charge shilingi 14 kwa lita, ukichukua milioni 9 mara shilingi 14 mara siku 365 za mwaka walikuwa wanachuma Sh.45,990,000,000 halafu wanalipa corporate tax bilioni 1.86 na VAT wastani wa milioni 650 kwa mwezi.

Mheshimiwa Spika, tukiwapa TBS kwa bei hiyohiyo ya shilingi 14 mara lita milioni 9 kwa siku mara siku 365 wanapata hiyo bilioni 45.9 gharama zao ni bilioni 33. Vilevile watatoa fedha kwa ajili ya development bilioni 2.5 na bilioni 9 itakwenda kwenye Government Consolidated Fund, tutapata bilioni 9. Hii ni fedha nyingi. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Nyongo.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi. (Makofi)