Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Esther Nicholus Matiko

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipatia fursa ya kuchangia kwenye Wizara hii muhimu sana ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, nishati ni muhimu sana kwa maendeleo ya nchi yetu kwa maana nishati ni uchumi bila nishati hamna utekelezaji wa Tanzania ya viwanda. Pia nishati ikiwepo inaimarisha usalama popote pale Tanzania hasa vijijini.

Mheshimiwa Spika, kama nchi au Taifa tuna Vision 2025 na tumeigawa katika miaka mitano mitano. Malengo ya Mpango wa Pili ya Maendeleo ya Taifa kwa Wizara hii ya Nishati target ilikuwa kuzalisha megawatt 4,915 kuanzia 2016/2017 mpaka 2020/2021 kutoka ile ambayo ilikuwepo ya 1,501. Nimenukuu kwenye hotuba ya Waziri mwenyewe anasema mpaka Aprili, 2021 tuna megawatt 1,605 kwa maana tofauti kwa miaka yote mitano hii tumeweza kuzalisha megawatt 104 tu. Katika malengo haya tulisema tutazalisha hizi megawatt zaidi ya 3,014 kwa kipindi cha miaka mitano ili iweze kutosheleza mahitaji ya ndani ya nchi na kuweza kuuza nje ya nchi. Sasa hatujafikia hayo malengo tumezalisha megawatt 401 tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nini kimepeleka hiki? Nimejaribu kupitia pia hotuba ya Mheshimiwa Waziri, Ibara ya 22 anaeleza bayana mathalani fedha tulizozitenga hapa 2020/ 2021 shilingi trilioni 2.17 mpaka Mei walikuwa wamepokea shilingi trilioni 1.3 tu ambayo ni asilimia 60, anakiri hapo.

Mheshimiwa Spika, kwa mwendo huu ndio maana tunashindwa kutekeleza mipango ya miaka mitano ambayo tulikuwa tumejiwekea kwa sababu haina uhalisia. Siku zote nimekuwa nikisema tuwe tunakuja na bajeti zenye uhalisia ili tunavyojipangia tuwe tunajua kabisa kwamba tuna kiasi fulani cha fedha tunakipa kipaumbele ili kutekeleza mradi A kama ni mradi wa Julius Nyerere Hydropower, LNG kwa maana gesi asilia tuweze kujua ni kiasi gani kinaenda na kiweze kutelekezeka. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pamoja na kwamba tukifikia malengo ya kuuza umeme nje na kuzalisha kutosheleza Tanzania bado umeme wa Tanzania ni ghali sana. Mathalani, wenzetu wa Kagera wanalalamika kwamba hawajaunganishwa na Gridi ya Taifa lakini wanaponunua umeme kutoka Uganda kwa Sh.10 wanapata unit zaidi ya 80 lakini kwa category ile ile kwa Tanzania ukinunua umeme wa Sh.10,000 unapata unit 28. Kwa hiyo, kwanza umeme unavyouzwa kwa wananchi ni ghali sana, Serikali iangalie ni vipi inafanya standardization ya bei ili Watanzania wapate huduma hii, tunawapelekea lakini waweze ku-afford kununua kulinganisha na nchi zingine lakini tunapofikia wakati wa kuuza nje pia bei yetu ikiwa ghali sana hatuwezi kupata wateja. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ambacho napenda kuzungumzia ni kutokuwepo na uhalisia wa takwimu ambao tunazitoa kwamba Watanzania wamefikiwa kwa kiasi gani. Nimesoma hotuba ya Waziri hapa anatuambia wameunganisha vijiji 10,312 kati ya vijiji 12,000 na zaidi, wanatuambia kwamba wameunganisha kwa asilimia 86. Wewe Spika umekalia Kiti jana na leo umeona kila Mbunge akisimama analalamika, Mbunge wa Mbinga Vijijini amesema ana vijiji 117 vimeunganisha 34, Mbunge wa Busanda jana amesema ana vijiji 83 vimeunganishwa 26 tu, nikizungumzia Mkoa wa Mara vijiji vilivyounganishwa ni chini ya asilimia 40. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa kila siku najiuliza hizi takwimu ambazo wanatuletea kwamba wameungnisha Tanzania kwa asilimia 86 zinatoka wapi? Wameenda mbali wakasema Watanzania milioni 47 wamefikiwa na nishati ya umeme. Wabunge tupo hapa tujiulize kule tunapotoka kwenye wilaya yako umepata umeme kwa asilimia 86? Hii kitu ni hatari sana tukitoa takwimu feki Wizara husika au Serikali ina relax hata wahisani hawawezi kutusaidia wanajua tuna-deficit kuwafikia Watanzania wote asilimia 13 tu which is a false, tutoe takwimu zenye uhalisia ili tuweze kupanga bayana kuhakikisha kwamba umeme unawafikia Watanzania wote kuliko hizi cooked data. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine hapo hapo napenda kushauri, tunapopitisha umeme tunasema tumepitisha kijiji fulani kwamba vijiji 10,000 ukiangalia miji 6, miji 10 kama ilivyo kwenye Sera ya Maji wanasema ndani ya mita 300 basi na sisi tuseme tunapopitisha huo umeme uwe ndani mita 400 au 300 au 200. Unapopitisha kwenye Kijiji A mtu yuko kilometa 8 au 10 unahesabu kwamba Kijiji cha Nyabilongo nipeleka umeme wakati ume-cover only ten percent or twenty percent. Hii siyo sawa tutakuwa tunajidanganya hatuwezi kulisaidia Taifa. Wana dhamira ya kweli na unyenyekevu kama wengine walivyosema, mimi mwenyewe nampongeza nikimfuata ni mnyenyekevu sana lakini tufikie target yetu, tuwafikie Watanzania kwa uhalisi sio kwa namba kwenye vitabu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kitu kingine ni uwiano wa mgawanyo wa fedha hizi. Wizara kweli inatengewa fedha na haziendi kwa uhalisia lakini hata zinazoenda basi tuweze kuangalia hii miradi yote iweze kupata kwa uwiano ili tuweze kutekeleza miradi hii kwa wakati vinginevyo inasababisha gharama kuwa kubwa. Mathalani katika hizi shilingi trilioni 2.3 za mwaka huu zaidi ya shilingi trilioni 1.44 zinakwenda kwenye Julius Nyerere Hydropower Project ambacho mimi na-support kwa sababu mradi ule ukiisha utasaidia sana kupatikana umeme nchini lakini pia unaangalia kwenye REA, tunapeleka shilingi bilioni 415 tu. Hizi takwimu zenu ndiyo zinasababisha mnapeleka fedha hizi, shilingi bilioni 415 haziwezi kwenda ku- cover maeneo yote na sasa hivi hii ni phase ya tatu. Tuangalie tukipeleka kwenye REA zaidi ya asilimia 70 au 65 ya Watanzania wataenda kupata umeme tuwekeze fedha huko kwa uwiano ambao unatoa uhalisia kuweza kutatua changamoto za nishati ya umeme kwenye maeneo yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kingine ni utekelezaji wa gesi asilia, kama nchi tukiamua kuwekeza kwa kasi kwenye mradi wa gesi asilia itasaidia sana. Kwenye hotuba yake amesema kwamba target ni kufikia nyumba 10,000 magari 700 na viwanda zaidi ya 20. Pia anasema by 2021 wamefikia nyumba 1,191 tu out of nyumba 10,000 ina maana kutoka nyumba 500 za mwaka 2020 mpaka nyumba 1,191 ni nyumba 691, kwa hizo 10,000 ina maana tutachukua zaidi ya miaka 20 kuzifikia kufikia. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tuamue kuwekeza, ndio maana nikasema uwiano na vipaumbele ni muhimu. Tukiwekeza kwenye gesi asilia kwanza hata kwenye magari inaondoa hata environmental pollution, ukitumia petrol na diesel tunajua uchafuzi wa mazingira ambao unatokea. Tukiamua kuwekeza magari mengi Tanzania yakatumia hii gesi asilia tutakuwa tume-save matatizo ya kimazingira. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie kwa upande wa Tarime, nimekuwa nikiuliza sana na ndiyo maana nikirudi pale kwenye takwimu kwa mfano Tarime Mjini sijataka kwenda hata huko Susuni, Mwema na wapi, nilikuwa namwambia Mheshimiwa Waziri kila siku tangia Bunge la Kumi na Moja kuna kata sita hazina umeme akasema vinaisha by phase II lakini hata phase III bado umeme haujafika. Kwa mfano Kata ya Nyandoto, Mitaa ya Masulule, Nyagesese, Nyasebe, Kemonge, Itinunu Nyatenene hakuna umeme. Kata ya Kenyemanyori tunahitaji umeme Kebaga, Nyamitembe, Chila, Longa na Mwibari. Kata ya Nkende tunahitaji umeme Iteve, Mtulu, Lomoli, Kitale, Kirumi, Nyamitebe na Kalamoloni. Kata ya Ketale tunahitaji umeme Ntabulo, Binagi, Wigoronto, Nyagesese, Malulu Center, Nyamahisana, Tebakiri na Nyamihobo na Kata ya Tura tunahitaji umeme Gimenya na Kikogoo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini zaidi nilikuwa nikiongoelea hapa ndani tunavyoenda kuwekeza tuwekeza basi umeme uende kwenye taasisi; sekondari, vituo vya afya na zahanati ili mfano kwenye sekondari watoto wetu waweze kujisomea baada ya masomo ya kawaida. Mama anavyokwenda kujifungua pale kama hamna umeme wanatumia vitochi au vikarabai hivi hatutakiwa kuwa hapo. Tunapoenda kupeleka umeme priority namba moja iwe ni taasisi muhimu tuhakikishe kwamba zimefikiwa na umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimalizie tu kwa kuwapongeza, wameainisha kwenye hotuba yao kwamba kuna viwanda hapa Tanzania vinazalisha vifaa ambavyo vinaenda kutumika kwenye miradi ya ujenzi ya umeme ambapo tumeweza ku- save zaidi ya shilingi bilioni 162, kwa hilo nawapongeza sana. Tuendelee kuwahamashisha watu wetu waweke ili kuzalisha hapa nchi kuliko kuagiza kutoka nje.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi)