Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

Hon. Martha Festo Mariki

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Nishati

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, nashukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Nishati.

Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijalia uzima na afya njema. Kipekee sana napenda kumpongeza Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Medard Kalemani na Naibu wake kwa jinsi ambavyo wanaendelea kufanya kazi kwa umakini mkubwa na nampongeza sana Katibu Mkuu wa Wizara. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kipekee sana naipongeza sana Serikali yangu Tukufu kwa kutekeleza mradi wa Mwalimu Nyerere. Mradi huu utakwenda kuleta tija na mapinduzi makubwa sana katika Taifa letu la Tanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, pia naipongeza Serikali kwa ajili ya mradi wa REA. Katika Mkoa wetu wa Katavi wananchi wanaipongeza sana Serikali kwa jinsi ambavyo imeleta umeme katika vijiji mbalimbali. Hata hivyo kuna maeneo ambayo bado hayajafikiwa na umeme huu. Hivyo, niiombe sana Serikali kupitia Waziri wetu Mheshimiwa Medard Kalemani vijiji hivi viweze kupata umeme huu ili kuleta tija kwenye uzalishaji katika maeneo mbalimbali.

Mheshimiwa Spika, vijiji hivi ni pamoja na Vijiji vya Mwamkulu. Kata ya Mwamkulu inaongoza sana kwa uzalishaji wa mpunga lakini kwa masikitiko makubwa bado haijaweza kupata umeme. Hivyo kumekuwa na changamoto katika mashine zile za kukoboa mpunga wananchi wamekuwa wakikwamisha na umeme.

Mheshimiwa Spika, pia katika Kijiji cha Kakese na chenyewe kina uzalishaji mkubwa sana wa mpunga lakini hakina umeme. Baadhi ya vijiji ambavyo pia havina umeme ni pamoja na Vijiji vya St. John, St. Maria, Mkwajuni na Ikokwa. Tuiombe sana Serikali yetu sikivu…

SPIKA: Vyote viko katika Wilaya gani?

MHE. MARTHA F. MARIKI: Mheshimiwa Spika, viko katika Wilaya ya Mpanda, Jimbo la Mpanda Mjini lakini ni Pembezoni, Kata ya Mwamkulu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia katika Wilaya hiyo Mpanda maeneo ya Ulila kuna Kijiji cha Usense na chenyewe hakina umeme, maeneo ya Ugala, Kambuzi na Litapunga. Tunaiomba sana Serikali vijiji hivi viweze kupata umeme. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, katika Mkoa wetu wa Katavi kwa muda mrefu sana tumekuwa tukitumia umeme wa generator. Upo mkakati wa kuleta umeme wa Gridi ya Taifa lakini tunaomba sana Wizara iweze ku-push na kuhakikisha kwamba mradi huu unaenda kukamilika kwa muda uliopangwa ambapo umeme huu ambao unatokea Sikonge kupitia Inyonga umepangwa kukamilika mwezi Septemba.

Mheshimiwa Spika, pia ombi letu sisi wananchi wa Katavi, wananchi wa Wilaya ya Mpimbwe wanasema kwamba kwa kuwa mradi huo utakwenda kukamilika kule Inyonga na Inyonga mpaka Mpimbwe ni takribani kilomita 135, wanaomba kuungiwa line ili umeme uweze kutoka Inyonga kwenda Mpimbwe. Kwa kuwa hiyo ni wilaya moja na ni karibu sana tungeomba sana na wananchi wa Mpimbwe waweze kuungiwa line hiyo ili umeme uweze kutoka Inyonga na kufika Mpimbwe. Kwa kuwa wananchi wa Mpimbwe wamekuwa wakipata adha kubwa wanatumia umeme wa gridi ambao unatokea Zambia kupitia Rukwa na umeme huo umekuwa ukikatika mara kwa mara kutokana na matumizi kuwa makubwa. Hivyo, tunaiomba sana Serikali yetu sikivu kuhakikisha kwamba mkakati huu unaenda kukamilika na wananchi wa Mpimbwe, Inyonga na Katavi yote wanapata umeme ili waweze kufanya shughuli zao za uzalishaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la kukatikakatika kwa umeme limekuwa ni changamoto kubwa ambayo pia imekuwa ikiwakwamisha sana baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Katavi hususani vijana wenzangu ambao wamekuwa wakijikita katika shughuli za uchomeleaji. Hivyo nikuombe sana Mheshimiwa Waziri kuhakikisha changamoto hii inatatuliwa.

Mheshimiwa Spika, ahsante sana, naunga mkono hoja asilimia mia moja. (Makofi)