Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Innocent Lugha Bashungwa

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Karagwe

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

WAZIRI WA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunijaalia nguvu ya kusimama mbele ya Bunge lako Tukufu ili niweze kuhitimisha hoja ya Wizara yangu. (Makofi)

Pia nitumie nafasi hii kukushukuru wewe, Naibu Spika wetu na Mbunge wa Mbeya Mjini, juzi nilikuwa Mbeya kwa kweli nilifurahi kuona kauli chanya za Wana Mbeya Mjini wengi kukupongeza kwa kazi nzuri unayofanya. Hongera sana Mheshimiwa Naibu Spika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie nafasi hii kumpongeza na kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, mama mahiri, mchapakazi tunampongeza kwa kazi nzuri anayoifanya kuiongoza nchi yetu. (Makofi)

Nitumie nafasi hii pia kumpongeza Mheshimiwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Mpango kwa kazi nzuri anayoifanya kumsaidia Mheshimiwa Rais katika kutimiza majukumu yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nitumie nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa Majaliwa kwa miongozo na maelekezo anayotupatia Mawaziri katika kutimiza majukumu yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa kauli, kwa maandishi na kwa support kwa ujumla Bunge zima toka asubuhi kwa kweli imekuwa ni furaha tupu. Waheshimiwa Wabunge tunawapongeza kwa ku-support michezo, sanaa, utamaduni na habari toka asubuhi yaani muda ungekuwa unatosha kwa kweli michango tungepata mingi sana kwahiyo tunawashukuru wale 29 ambao mmechangia hoja yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia niwashukuru Kamati inayoongozwa na Mheshimiwa Nyongo na Makamu Mheshimiwa Kamamba na Waheshimiwa Wajumbe wote kwa maoni na ushauri ambao mmekuwa mkitupatia. Na niwaahidi Wizara yangu kwa maoni na ushauri ambao mmetupatia tutauekeleza kwa asilimia 100. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa nijibu hoja zilizotolewa kutoka kwenye michango ya Waheshimiwa Wabunge na nianze kwa kumshukuru Naibu Waziri Mhehimiwa Pauline Gekul kwa ufafanuzi mzuri wa hoja za Wabunge. Na nianze kwenye Tasnia ya Habari; kumekuwa na hoja kwamba Serikali tusaidie wanahabari kwenye stahiki zao na hoja hii ilichangiwa na Wabunge kadhaa, Mheshimiwa Bulaya pamoja na Waheshimiwa Wabunge wengine ningependa kuwaondolea wasiwasi Waheshimiwa Wabunge, Serikali ndio maana kwenye Sheria Na. 12 ya mwaka 2016 ukiangalia moja ya malengo ya sheria ile ni kuhakikisha stahiki na maslahi ya wanahabari yanazingaitiwa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ninachoweza kuwahakikishia pamoja na Wabunge sheria ile imeelekeza kuanzisha Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Wanahabari na vyombo hivi viwili moja ya majukumu ni kuhakikisha vinasimamia maslahi ya wanahabari. Na sisi Serikali kwa vile tunajali maslahi na stahiki za wanahabari tutahakikisha tunatumia sheria hii kuhakikisha mambo mazuri kwa mfano, bima kwa wanahabari, mambo ya pensheni na mazingira bora ya kazi yanazingatiwa kwa wamiliki wa vyombo vya habari kwa mujibu wa sheria. Kwa hiyo, ningependa kuwaondoa wasiwasi Waheshimiwa Wabunge pamoja na wanahabari kote nchini Serikali tupo pamoja nao.

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna hoja pia kwamba Serikali hufungia vyombo vya habari ambavyo vinafanya kazi za kiuchunguzi. Sheria Na. 12 ya mwaka 2016 kifungu 52(2) kinasema kwamba si kosa kuikosoa Serikali. Kwa hiyo, Serikali haijawai kufungia chombo chochote cha habari eti kwa vile kinafanya kazi za kiunchunguzi. Kwa vile magazeti ambayo yalifungiwa yalikuwa ni mambo ya kimaadili na uvunjifu wa Sheria ya Habari, lakini sio kwamba wanafanya kazi ya kiuchunguzi, hiyo si kweli.

Kwa hiyo, pamoja na Waheshimiwa Wabunge nitoe wito kwa wanahabari na wadau wote wa tasnia ya habari waendelee kufuata Sheria na Maadili ya Habari na Utangazaji. Nia ya Serikali ni kuweka mazingira wezeshi ili kazi zao ziweze kufanyika vizuri, lakini lengo la Serikali siyo kufungia vyombo vya habari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sasa niende kwenye upande wa michezo; na mimi niungane na Waheshimiwa Wabunge kuipongeza Azam kwa mkataba ambao walisaini na TFF kwa kweli mkataba huu utaleta mchango na mageuzi makubwa katika maendeleo ya sekta ya soka nchini. Lakini Azam tumewaona wakisaidia pia tasnia ya ngumi kwa hiyo nitoe wito kwa wadau wengine wafanye kama Azam ili tushirikiane pamoja na Serikali kuhakikisha tunaendeleza michezo nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna suala la utawala bora katika michezo na Waheshimiwa Wabunge sana sana wamejikita katika kuelezea changamoto zilizopo za utawala bora upande wa soka hasa hasa TFF.

Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua kwamba kwa utaratibu wa FIFA, Serikali inatakiwa iwe eyes on, hands off katika masuala ya michezo. Lakini pia Serikali tunatambua kwamba hata FIFA inashirikiana na Serikali kote inakofanya kazi katika kusimamia masuala ya michezo.

Kwa hiyo, kwenye suala la utawala bora Serikali tuko serious, zipo sheria za nchi ambazo zinasimamia masuala ya utawala bora na katika hili Waheshimiwa Wabunge, Wizara imepokea malalamiko, kwa hiyo, nikiri kwamba malalamiko haya na sisi tumeyapokea na tayari nimeelekeza Baraza la Michezo Tanzania kufanyia chambuzi malalamiko haya ili tuweze kuyafanyia kazi kwa mujibu wa sheria na taratibu za nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwenye suala la utawala bora Serikali tuko serious, tutahakikisha sheria na taratibu za nchi zinasimamiwa. Kwa hiyo, ningependa kutoa wito na nilishatoa wito huu kwa TFF waendelee kuzingatia misingi ya utawala bora hapa nchini katika suala zima la maendeleo ya soka.

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna suala la rushwa. Kwamba, TAKUKURU ilikuwa inachunguza jambo ambalo limechukua muda mrefu. Nimefuatilia jambo hili na kwa vile bado liko kwenye uchunguzi basi niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge kuwa TAKUKURU italitolea ufafanuzi wake pale uchunguzi utakapokuwa umekamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na Waheshimiwa Wabunge ningependa kuzungumzia changamoto ambazo zimetajwa kwenye maendeleo ya michezo nchini kwa kutumia mfano wa pyramid. Pyramid ukiiangalia upande wa chini inakuwa ni pana halafu kadri unavyopanda inakuwa ni nyembamba. Sasa kwenye maendeleo ya michezo nchini kwenye hotuba yangu nimesema kuna mpango mkakati wa maendeleo ya michezo ambao tunauzindua Julai, 2021 yaani mwezi wa saba na katika mkakati huu Waheshimiwa Wabunge, kwenye hotuba yangu nimesema sports for all, kwamba lazima tuhakikishe shule za misingi na sekondari watoto wote wawe kwenye shule za msingi za umma au binafsi, shule za msingi na sekondari wanapata fursa ya kucheza michezo shuleni kama wanavyopata fursa ya kusoma masomo mengine. Jambo hili tayari tumeshashirikiana na Wizara ya Elimu, namshukuru Mheshimiwa Profesa Ndalichako pamoja na Mheshimiwa Waziri wa TAMISEMI Mheshimiwa Jafo kipindi kile, lakini hata Mheshimiwa Ummy tumeendelea kushirikiana katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tumeunda utatu wa kushirikiana kuhakikisha masuala ya UMITASHUMTA na UMISETA tunajipanga upya kuanzia mwaka huu na ndiyo maana Waheshimiwa Wabunge mtaangalia mkakati wa UMITASHUMTA na UMISETA wa mwaka huu uko tofauti na miaka iliyopita. Nimshukuru Mheshimiwa Waziri Mkuu, tarehe 8 Juni ataenda kutufungulia mashindano kule Mtwara. Lakini kuanzia mwaka huu kwenda miaka inayokuja Waheshimiwa Wabunge mtaona tofauti kubwa. Tumejipanga kuhakikisha kupitia UMITASHUMTA na UMISETA watoto wetu wanapewa mazingira mazuri ya kufanya michezo lakini pia tunashirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha watoto wanaofanya vizuri kupitia michezo hii basi tunawaendeleza badala ya kuacha UMITASHUMTA na UMISETA imeisha basi wanapotea mpaka mwaka unaofuata. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini pia miaka ya nyuma watoto walikuwa wanacheza unakuta wiki moja kabla ya UMITASHUMTA na UMISETA ndipo wanaandaliwa kwenda kushiriki kwenye michezo. Safari hii kupitia TAMISEMI tayari maelekezo yameshatolewa kwenye shule za msingi na sekondari kote kwamba somo la michezo ni somo muhimu kama masomo mengine. Kwa hiyo, tutaendelea kusimamia hili ili kuendelea kutengeneza vipaji kwa watoto wetu kuanzia shule za msingi na sekondari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, sambamba na hili tuanshirikiana na TAMISEMI kubainisha shule ambazo zitakuwa ni shule maalum za michezo kwenye shule za msingi kila mkoa na sekondari. Zoezi hili tumekubaliana likamilike kufika mwezi huu mwishoni ili kwenye mipango ya Serikali ya miaka ya fedha inayokuja, basi fedha iwe inatengwa tunahakikisha shule hizi maalum zinapata vile vifaa vya lazima ili watoto wanaofanya vizuri wenye vipaji wanaenda kwenye kwenye hizi shule maalum sambamba na combination ambazo zitakuwa zinatolewa form five na six ili kuandaa walimu wa michezo hapa nchini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pamoja na Waheshimiwa Wabunge kwa kutumia hii pyramid approach vipaji tutakavyoinua kupitia shule za msingi na sekondari katikati ya pyramid kuna upande wa sekta binafsi pia kushiriki kwa kujenga academies na tumeona academies mbalimbali hapa nchini. Tunaipongeza Serikali na kuwaunga mkono wawekezaji hawa na tutaendelea kushirikiana nao kuhakikisha suala la kuibua vipaji kutoka kwenye shule za msingi na sekondari basi hapa tunakuwa tuna sports academies nyingi na sisi Serikali ili kuonesha mfano tumetenga shilingi bilioni 1.3 kwenda kwenye Chuo cha Malya ili kuwe kuna sports academy, wale wanachuo wanaojifunza michezo wajifunze kwa vitendo huku wakifundisha kwenye shule hii ambayo itakuwa inaendeshwa na Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya hapo kwenye pyramid mwisho inakuwa nalo hapo ndiyo unakuta vilabu kama Simba, Yanga, Namungo, Ihefu na vilabu vingine. Lakini hapo ndipo tunaenda kwenye professional sports yaani wachezaji wa ndani kwenye vilabu, lakini na wachezaji wa nje. Tukitumia approach hiyo mimi sina shaka kwa namna Serikali ambavyo tumejipanga tutafanya vizuri na niwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu mizuri ambayo itatupa muelekeo na kusaidia kuboresha haya niliyoyataja. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini yapo mapitio ya sera, sheria na kanuni ili kuhakikisha mkakati huu tunaenda vizuri na unakuwa na matokeo ambayo mmetushauri. Katika hili mimi namshukuru Mheshimiwa Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, ametuelekeza kwamba pamoja na mikakati yote hii angependa kuona wanawake katika michezo nao wanafanya vizuri. Haiwezekani tukawa tuna mama mahiri, shupavu Rais wetu Mama Samia Suluhu Hassan, nina Naibu Waziri mwanamke, halafu timu za wanawake zinafanya vibaya. (Makofi)

Kwa hiyo, nawahakikishia kwenye hili tutahakikisha michezo inaenda sawia wanaume na wanawake na timu za wanawake zinafanya vizuri. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, hoja ya viwanja vya CCM ni kwamba Wizara yangu imeratibu jambo hili; Azam, TFF na Chama cha Mapinduzi wako katika maongezi ya kuangalia namna ya kushirikiana ili kuendesha viwanja vya Chama cha Mapinduzi nchini. Katika hili niwaelekeze TFF, sauti ya Wabunge ni sauti ya wengi, katika fedha ambazo wanazipata kutoka FIFA pamoja na vyanzo vingine hebu tuanze kuangalia na kuweka nyasi bandia kwenye viwanja ambavyo viko kwenye mikoa mbalimbali. (Makofi)

Kwa hiyo, TFF kwenye hili najua mnajenga uwanja wa kisasa pale Kigamboni na Tanga lakini kwenye vipaumbele kuanzia mwaka huu ambao na mimi naomba nipitishiwe fungu basi TFF tuanze kushirikiana kuhakikisha nyasi bandia kwenye viwanja mbalimbali mikoani basi tunashirikiana katika kuvijenga. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini jambo lingine ni suala la wachezaji wa kigeni vs local content kwa maana ya kukuza vipaji ndani ya nchi ni suala ambalo lina mjadala na lina pande mbili. Ningependa kuwakumbusha Waheshimiwa Wabunge, mwaka jana mlituelekeza tushirikishe wadau ili tuweze kulipatia mwelekeo. Baada ya kuwashirikisha wadau, mwongozo unasema maximum ya wachezaji wa ndani kwenye klabu ni wachezaji wasiozidi kumi.

Kwa hiyo, kama kutakuwa na ushauri na maboresho katika hili sisi tuko tayari kupokea ushauri wenu ili tuone namna ya kulipeleka lakini nia hapa ni ku-balance import substitution ni jambo zuri ili tuweze kutengeneza vipaji vya hapa ndani. Lakini hiyo isiweze kuathiri malengo ya vilabu katika kutafuta wachezaji wazuri. Katika hili nipende kusisitiza na kuelekeza wale wanaoleta wachezaji kutoka nje basi leteni wachezaji ambao wana-profile ambazo zinaeleweka na zitaleta mageuzi katika kufundisha vijana wetu ambao wanacheza hapa ndani. Ipo kasumba unakuta mchezaji ametoka nje lakini akija anacheza, anazidiwa na wachezaji wa ndani. Sasa hiyo inakuwa na maana gani? (Makofi)

Kwa hiyo, ningependa kuwasisitiza vilabu pamoja na wadau wa mchezo wa soka tuangalie profile za wachezaji tunaowaleta ili watakapokuja kweli waweze kutoa chachu kwa wachezaji wetu wa ndani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna hoja ya uwanja wa michezo hapa Dodoma ambao uliahidiwa na Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliuliza Mheshimiwa Mavunde. Ningependa kumhakikishia kwenye hili tuko katika hatua nzuri. Eneo la kujenga tumeshalibainisha na Serikali kupitia Wizara ya Fedha maana mkakati wa Serikali ni kupitia mradi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere kwenye corporate social responsibility hapo ndipo tutapata fedha za kujenga uwanje huu. Kwa hiyo, commitment ya Serikali iko pale pale na jambo hili tutalisimamia katika utekelezaji wake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia kulikuwa kuna suala la Muungano. Ningependa kuwahakikishia Waheshimiwa Wabunge michezo inatuunganisha, ni sehemu ya fursa ya kujenga Muungano wetu. Kwa hiyo, changamoto zilizopo TFF na ZFF tutawaelekeza na kuwasihi waendelee kushirikiana kwa sababu michezo na sanaa ni maeneo ambayo yanatuunganisha vizuri sana katika Muungano. Kwa hiyo, mimi kama Waziri mwenye dhamana nitaendelea kuhakikisha kupitia michezo ZFF na TFF wanashirikiana katika kuleta mageuzi ya maendeleo na michezo Bara na Visiwani. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye upande wa Sanaa niungane na Waheshimiwa Wabunge kumpongeza mdogo wangu Naseeb Abdul a.k.a Diamond. Nami niendelee kutoa wito kwa Watanzania, katika hili tumuunge asilimia 100 ili kijana wetu ashinde. Hii ni heshima kwa nchi yetu, lakini katika hili pia niwapongeze vijana wetu waliopata tuzo za AFRIMMA ya mwaka 2021 alikuwepo Diamond, Nandy na Zuchu, na wenyewe tunawapongeza. (Makofi)

Katika hili niendelee kusisitiza iwe kwenye michezo, sanaa, timu au mtu anapoliwakilisha Taifa letu hebu turudi kuwa wamoja kama Watanzania tuweke ushabiki wetu pembeni. Kwa hiyo, hata hili la Diamond, najua kwenye muziki pia kuna ushabiki, kuna timu fulani na timu fulani. Ningependa kutoa wito kwa wadau na Watanzania kwenye hili tuungane na tumuunge mkono kijana huyu akifanikiwa kupata award ya BET inaleta inspiration na hamasa kubwa kwa vijana wengine wanaochipukia katika sanaa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala la sports and arts arena; Serikali inachukua jambo hili kwa uzito sana Waheshimiwa Wabunge. Ningependa kuwatoa wasiwasi. Sasa hivi kwenye bajeti tumetenga shilingi milioni 20.9 yaani milioni 20 na laki tisa kwa ajili ya kumlipa mtaalam elekezi aweze ku-design mchoro na kusanifu ili tuweze kujua gharama halisi ya kujenga hii sports and arts arena. Kwa hiyo, kwenye bajeti inayokuja ya mwaka unaokuja tutakuwa tumeshajua gharama halisi ni nini ili tuweze kuziombea fedha kwenye bajeti inayokuja. Kwa hiyo, kwenye mwaka huu tumetenga hela ya kumlipa consultant afanye usanifu halafu mwaka unaokuja tutaweza kujua gharama halisi ni kiasi fulani ili tuweze kuiombea fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kulikuwa kuna suala la BASATA. Waheshimiwa Wabunge, kwenye hili Wizara tuko na ninyi. Tunatambua hata kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi fursa ziko kubwa sana katika tasnia ya sanaa kutengeneza ajira kwa vijana wetu. Lakini sambamba na hili, tutafanya kila linalowezekana kuweka mazingira wezeshe. Ndiyo maana nilielekeza kanuni ya 25 tu-withdraw, tushirikishe wadau tuweze kufanyia maboresho, kwa sababu lengo la Serikali ni ku-promote sector itengeneze ajira na kuchangia Pato la Taifa, lakini tusifanye hilo kwa cost ya kudidimiza maadili. Kwa hiyo, hata kanuni tunayoiandaa tunatafuta balance ya ku-promote sector kama Ilani ya Chama cha Mapinduzi inavyoelekeza, lakini sambamba na hilo, maadili lazima tuyalinde. Katika hili tumeenda mbali, tupo tunaandaa mwongozo ambao tutashirikisha ma-producer na Idara za Muziki kwenye redio na tv ili kila mmoja katika eneo lake ajue kwamba jambo hili tumekubaliana ni katazo kwa hiyo hata mimi ninawajibika kulisimamia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, ninaamini tukifanya hivyo tutaondoa urasimu unaolalamikiwa lakini tutasaidiana katika kuhakikisha maadili hatuyadidimizi kwa gharama ya kuangalia tu ku-promote sector. Hakuna Taifa ambalo halina maadili, Taifa lolote linajivunia na utambulisho wake ni mila na desturi zake. Kwa hiyo, ningependa kutoa wito kwa wasanii wetu waendelee kuipa ushirikiano Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na tuangalie na tusaidiane kuhakikisha mwongozo tutakaoutoa wote tunashirikiana katika kuusimamia pamoja na Kanuni mpya ambayo niwahakikishie hatutachukua muda mrefu kuikamilisha ili iweze kuingia katika utekelezaji. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kulikuwa kuna hoja pia kuhusu COSOTA, suala ya mirahaba. Nilivyoangalia kiasi ambacho COSOTA imekusanya nikaona ni kidogo sana, lakini pia nikaangalia potential ya kukusanya mirahaba kupitia COSOTA nikaona ni kubwa sana. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge tulichokifanya katika hili TCRA kwa teknolojia iliyopo muziki ukipigwa kwenye redio au tv, hata ukipigwa kwa sekunde 15 tunajua redio fulani imepiga muziki wa msanii fulani. Kwa hiyo, TCRA inashirikiana na COSOTA kutengeneza mfumo ambao tutautumia kuboresha mfumo wa ukusanyaji mirahaba kwa wasanii wetu. Mimi ningependa siku tunawaita wasanii, tunagawa bilioni kadhaa sio milioni 199 ambayo iko hivi sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wabunge, kwa hiyo ningependa kuwaomba mtupe muda mpaka mwisho wa mwaka ili jitihada hizi nilizozitaja tuziweke katika utekelezaji angalau tutakapoandaa tukio la kutoa mirahaba kwa wasanii, hata ukimkaribisha Mheshimiwa Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu aje kuzindua hilo tukio liwe linaendana na hadhi yake. Lakini huwezi ukamkaribisha Mheshimiwa Rais au Makamu wa Rais au Waziri Mkuu aje kugawa mrahaba wa milioni 190. Kwa kweli mimi kwa ninavyotazama fursa ya kukusanya mirabaha hii, najua mpaka kufika mwisho wa mwaka tutakuwa tumepiga hatua nzuri. (Makofi)

Kwa hiyo, ningependa kuwaomba Waheshimiwa Wabunge mtuamini katika hili na wasanii tutafanya vizuri. Tumejipanga vizuri kuhakikisha tunatumia mifumo na teknolojia katika kuwasaidia wasanii kupata mirahaba na haki zao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sambamba na hili ni suala la aggregate ambalo limetajwa; tunafanya mawasiliano na tunajadiliana na wasanii, Mheshimiwa Babu Tale, Mheshimiwa Mwana FA mmekuwa washauri wazuri katika hili. Tutaangalia namna bora ya kulipeleka hili ili liweze kuwasaidia wasanii wasinyonywe kama ilivyo hivi sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kumekuwa kuna michango mingi ya Waheshimiwa Wabunge, lakini mimi kama nilivyosema hapo mwanzo, nikiri kwamba tumepokea na hoja zote tutaziwasilisha kwa maandishi na niwashukuru sana, hii Wizara ni Wizara ambayo kazi kubwa ni kuratibu. Kwa vile tunawasikia na mnatupa ushauri mzuri mimi niwahakikishie nitaendelea kushirikiana na Mheshimiwa Naibu Waziri, Katibu Mkuu na timu yangu ya Wizara ili kuratibu mawazo na ushauri mzuri ambao Bunge hili tukufu mnatupatia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru sana kwa nafasi hii, natoa hoja. (Makofi)

WAZIRI WA MAMBO YANJE NA USHIRIKIANO WA AFRIKA MASHARIKI: Mheshimiwa Naibu Spika, naafiki. (Makofi)