Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Sophia Hebron Mwakagenda

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kunipa nafasi na mimi kuchangia Wizara hii, mimi nitazungumizia upande wa ngumi kwa sababu toka asubuni sijaona uwakilishi kwa watu wa ngumi. (Makofi/ Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ngumi kama ilivyo michezo mingine ni ajira kwa vijana na mara nyingi sana na kwa muda mrefu ngumi iliyoonekana wapiganaji ngumi ni wakorofi, ngumi ni uhuni, ngumi sio kitu sahihi, ninamshukuru kipekee, Mheshimiwa Waziri aliyepita Mheshimiwa Mwakyembe alijitahidi sana na hasa baada ya kumpa ushauri wa karibu aliweza kuitengeneza tasnia ya ngumi angalau kuonekana ipo katika Wizara.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwenye ngumi Waziri aliyemaliza muda wake aliamua kuweka Kamisheni ya Ngumi, siku za nyuma watu wa ngumi wachache wajanja walikuwa wanachukua vijana kwenda kupigana nje ya nchi, unafahamu ili uweze kupanda daraja kwenye ngumi ni lazima umpige adui yako ndipo unapanda cheo. Hivyo wale tunawaita wasimamizi wa ngumi ikiwepo ma-promoter walikuwa wanachukua vijana wetu wanawapeleka nje ya nchi wakijua kabisa hawana uwezo wa kwenda kupambana na wale wanaoenda kuwagombanisha ili tu wale watu wa nje wapande daraja kwa kutumia vijana wetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, huo ulikuwa uuaji na ilikuwa ni tabia mbaya sana. Sasa Mheshimiwa Waziri nina kuomba sana ninajua kwamba wako wachache waliobaki wanachukua vijana wetu wanapeleka nje kuwachezisha kwa mchezo ambao hawajakidhi kwa maana ya kilogram. Wapiganaji ngumi huwa tunapimwa uzito wako na uzito wa kwako na mwingine ndio unakuwa sawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wanakuchukuwawewe wa kilo 59 wanakupambanisha na mtu wa kilo 70 wa Uingereza promoter apate fedha wakati mpambanaji toka Tanzania anakuwa ameumizwa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, tabia hii Dkt. Mwakyembe aliikomesha, lakini bado inaendelea; ninaomba kiongozi wa sasa aisimamie na kuiangalia.

Mheshimiwa Naibu Spika, kuna Kamisheni ya Ngumi, mtu mmoja asubuhi amengumza habari ya majina ya Urais, sijui nani wa Kamisheni, mimi ninafikiri naunga naye mkono kwamba huyo anayejiita Rais wa Ngumi iweze kubadilishwa. Kwa hiyo, ninaomba Wizara muangalie Katiba ya wanangumi ibadilishwe, maana utendaji wao ubabaishaji bado unaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ni promoter pia, baada ya kuacha masumbwi, umri umekwenda sasa nimekuwa promoter. Katika u-promoter wangu nimejikita sana kwa mabondia wa kike akina Feliche, akina Asha Ngedere na wengineo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mabondia hawa hawajui mikataba ambayo wanakwenda kuchezeshwa promoter amelipwa shilingi ngapi; huo ndiyo ugomvu wangu mimi na ma-promoter wengine, hata mkisikia natukanwa, jua kwamba mimi ninapambana. Sisi ma-promoter lazima tuoneshe mikataba na wale tunaoingia nao ili mcheza ngumi akienda kupigana ajue anapigania nini. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, mcheza ngumi anatolewa Tanzania anapandishwa basi kwenda Zambia na wala siyo ndege, anafika amechoka, anakwenda kupambana ngumi kwa kutumia nguvu zake, halafu unamlipa shilingi 200,000; hii siyo sawa. Ninaomba Wizara isimamie hilo. Na hasa ma- promoter wa mabondia wanawake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiwa unacheza ngumi ukishapigwa kwa KO mara nyingi thamani yako inashuka, unazeeka hata nyumba hujajenga. Leo hii mimi nimekuwa Mbunge, nashukuru angalau lakini wengine, mabondia wenzangu walioko nje, hawana hata nyumba kwa sababu ya kipato kidogo.

Mheshimiwa Naibu Spika, ninajua Tulia Trust inasaidia sana, ninakuomba sana waone mabondia wa kike, ili uweze kuwasaidia kama ambavyo unasaidia wengine. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba bima za afya kwa mabondia. Serikali tunawaomba kama ikibidi mtulazimishe sisi ma-promoter tuwakatie bima mabondia wetu. Maana wasipokuwa na bima kuna wakati unapigwa ngumi moja unarudi chini ya ulingo hata pesa ya kujitibia huna. Ninaomba ma-promoter sasa waweze kuwalipia mabondia bima ya afya kwa faida ya maisha yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kutoka kwenye ngumi, sasa nije kwenye TBC. Televisheni hii ni Televisheni ya Taifa na ina manufaa kwa Watanzania wote. Lakini nimekuwa nikimpigia simu Mkurugenzi wa Shirika hili; kuna wakati vyama vya siasa ambavyo ni walipa kodi na wana uhalali na tv hii pamoja na redio, lakini wanapokuwa na shughuli zao ni vigumu sana kukubaliwa kutoka live kama ukiwa chama mbadala na wala siyo chama tawala. Ninaomba sana Mkurugenzi ufikirie, tv hii pamoja redio ni ya Watanzania, tuhudumiwe kwa usawa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini si hivyo tu, usikivu hasa mipakani, bado unasumbua. Ninaomba Serikali iongeze fedha ili tuweze kuongeza usikivu kwa ajili ya Televisheni ya Taifa pamoja na Redio Tanzania ya kwetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niweze kuzungumzia Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema kila mtu ana haki ya kupata habari, ya kutoa maoni, lakini kwa nyuma kidogo kulikuwa kuna ugumu wa kutoa maoni kwenye mitandao ya kijamii, kwenye redio na vitu kama hivyo. Lakini tunamshukuru Rais, amesema vyombo vyote viwe sawa na akaruhusu baadhi ya vyombo vilivyofungiwa virudishwe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo, nitumie nafasi hii kuiambia Wizara irudishe magazeti yote, irudishe vyombo vyote kwa…

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, taarifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda, kuna Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Taletale.

T A A R I F A

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa promoter, kabla Mheshimiwa Waziri hajarekebisha hilo neno la rais, ukisema rais sema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mnavyosema Rais tunajua Rais wa Ngumi, ahsante. (Makofi/Kicheko)

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Sophia Mwakagenda.

MHE. SOPHIA H. MWAKAGENDA: Mheshimiwa Naibu Spika, ninaikubali taarifa hiyo, ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni mmoja, lakini Rais wa Ngumi, Rais wa Yanga, wote hao wafutwe abaki Rais wa Simba. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, tuendelee, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amesema vyombo vyote vilivyofungiwa virudishwe na mimi nakubaliana naye, nami ninasema leo hii kwenye Wizara hii, ninaomba kabisa zile sheria ambazo zililetwa hapa tukazipitisha, kama ikiwekezana Wizara ilete tuweze kurekebisha baadhi ya sheria tulizozipitisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano ile sheria ya kukubali haki ya vyombo vya habari irudiwe, marekebisho ya Sheria ya Huduma ya Vyombo vya Habari ile ya 2016, kama inawezekana iletwe tena tuone kama kuna sehemu ya kurekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Sheria ya Makosa ya Mtandao pia nafikiri kuna haja iletwe sasa tuweze kuirekebisha. Dunia ya sasa mtandao uko kiganjani, tukianza kushikana kwa cybercrimes kwamba umeongea kitu hiki facebook, umefanya hivi, haiwi sawa sawa.

Mheshimiwa Naibu Spika, baada ya kusema haya, naomba nizungumzie suala la BAKITA. Tunafahamu kwamba Kiswahili ndiyo lugha yetu ya Taifa, na Marehemu Rais Nyerere, wote hao walizungumzia sana suala la Kiswahili. Leo hii ukienda nchi zingine, kwa mfano Afrika Kusini ilitaka shule zake, vyuo vyake viweze kuwa vinatumia lugha ya Kiswahili. Lakini walioshinda tenda ya kufundisha ni Wakenya ambao wao ni wanafunzi wetu sisi.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi naomba sana BAKITA ni lazima mchukue nafasi ya kuwasaidia Watanzania fursa mbalimbali ambazo zinajitokeza, muwe wa kwanza na mfanye kwa haraka kuhakikisha hatuachwi nyuma kama waanzilishi wa lugha hii ya Kiswahili.

Mheshimiwa Naibu Spika, mimi ninafahamu wengine wamezungumza habari ya sanaa, ni kweli wasanii, wakiwemo waimbaji wa maigizo, wamekuwa wakijitumikisha wenyewe na kufika mahali tunawasifia, ni baada ya wao kutumia jitihada zao binafsi kufika hapo walipofika. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo hii wamezungumza habari ya kuweza kumpigia kura Diamond. Mimi nafahamu yupo mtoto anaitwa Sonia wa Monalisa. Huyu ni binti wa sekondari lakini ameingia kwenye kuchaguliwa na ametaka wananchi tumchague, ni juhudi za bibi yake anatoa Instagram, na mimi ninayemfuatilia ndiyo ninaona.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini Wizara inafanya nini kuwasaidia vijana kama hawa? Wizara inafanya nini kumsaidia Diamond kuweza hata kutangaza kwenye TBC, ndiyo kazi ya Televisheni ya Taifa, wala siyo kusikiliza taarab, ni vyema tukaangalia vitu vya msingi kuliko kuweka vitu ambavyo ni vya kujiburudisha na wala havijengi wala kusaidia sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, sanaa; mwingine amezungumza, vijana wetu kwa sababu ya kutokuwa na ajira, lakini wakati mwingine wana vipaji, wamekwenda kuingia kwenye sanaa. Leo mtu anaigiza amekaa chini ya mwembe lakini inadondoka nazi, ni kwa sababu ya kutokuwa na elimu. (Kicheko)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba tuwasaidie. Ninaomba Wizara itumie fursa ya makusudi kuwasaidia. Wanahitaji kuigiza, lakini hawana elimu, hawana msaada kutoka kwenye Serikali. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninaomba, siyo kuunga mkono, lakini ninaomba Serikali ihakikishe inasimamia hayo bila kusahau kuwasimamia ma-boxer wangu. Ahsante sana. (Makofi)