Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Hamis Mohamed Mwinjuma

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Muheza

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. HAMIS M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa nafasi hii na mimi niweze kuongeza senti 50 zangu kwenye bajeti hii ya Wizara ya Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, asubuhi wakati wa michango, moja ya wachangiaji dada yangu Ester Bulaya aliongelea wanahabari na kidogo kukawa na lawama ya kwamba Wabunge wote ambao walitangulia kutoa michango hawakuwa wamewaongelea wanahabari. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niseme hili ni suala ambalo tumekuwa tukilifikiria kwa muda mrefu ya kwamba Wizara hii ina matawi mengi kiasi kwamba matawi mengine yanafichwa sana. Ningetoa pendekezo heshima kwa mamlaka husika kuona kama tunaweza kuipunguzia matawi Wizara hii kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mfano habari imekaa sana kama inafanana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari na hali kadhalika utamaduni umefanana sana na Maliasili na Utalii ili tubaki na Michezo na Sanaa ambavyo kusema kweli asilimia 98 ya michango iliyotoka leo ilikuwa inaelekea huko, kama itazipendeza mamlaka kwa hisani yao naomba waliangalie. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine nitoe pongeze kwa Serikali na Azam Media kwa mkataba mzito wa haki za television za ligi yetu kuu, mkataba ule ambao haujawahi kutokea kwa nchi za Afrika Mashariki ni mkubwa sana na sisi watu wa mpira tunaimani kwamba unakwenda kusaidia mpira wetu. Watu wa mpira tunafahamu masuala ya fedha yalivyokuwa yanaathiri ubora wa ligi yetu, timu nyingi zilikuwa haziwezi hata kusafiri zenyewe mpaka zichangishe washabiki wake na hili lilikuwa linafanya michezo mingi iamuliwe siyo kwa sababu ya ubora wa michezo yenyewe, ubora wa wachezaji na ubora wa timu, isipokuwa kwa uwezo ama kutokuwa na uwezo wa fedha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na ndiyo maana unasikia kila siku kuna maneno maneno mara huyu anasema ametaka kupewa milioni 40, hivi vitu ni vya kweli na ninaamini sasa Azam kwa namna moja ama nyingine wamekwenda kuzirekebisha. Kule kwetu tunasema kila harusi inamshenga wake na sisi tunaamini ya kwamba Azam Media ndiyo washenga wa mpira wa nchi hii, kwa hiyo, hii naomba nichukuwe nafasi hii kupitia Bunge lako Tukufu kuwapongeza sana. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pendekezo langu kwa Wizara ni iwekeze nguvu zake kwenye kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kuwekeza kwenye ngazi za chini, mashuleni na huku kwenye field. Ukienda majimboni moja ya matatizo makubwa ambayo unaulizwa kila siku na vijana ni vifaa vya michezo na viwanja; hawataki nyasi, hawataki viwanja vya milioni 300 kama alivyopendekeza ndugu yangu Senator Sanga asubuhi wanataka tu viwanja vinavyotosha kuweza kufanyia kazi vipaji walivyojaliwa na Mwenyezi Mungu.

Mheshimiwa Naibu Spika, na kusema ukweli ni gharama kubwa, naona Wabunge hawana uwezo wa kuyamudu hayo. Mimi mara ya mwisho kuna kata inaitwa Kwaibada katika jimbo la Muheza vijana waliniomba niwasaidie wakati TARURA wakienda kule wawasaidie kuchonga/kurekebisha uwanja wao ambao umekaa upande mmoja uko mlimani, upande mmoja uko chini, nilivyowaomba TARURA wakaniletea bill ya milioni 13 kwa ajili ya kurekebisha uwanja ule, nikaona sasa TARURA nao hawataki uwanja utengenezwe bado nawaza namna ya kuwasaidia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini nipendekeze kwamba Wizara ione namna ambayo kama inaweza kupeleka fedha zaidi mashuleni na majimboni ikiwezekana kwa ajili ya vifaa na kurekebisha viwanja hivi sehemu za vijana kufanya michezo hii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, lingine ni ushiriki wa wachezaji wa nje kwenye ligi zetu, ukiangalia ligi yetu na idadi ya wachezaji wa nje ambao wanatupa burudani kubwa naweza kuwataja wengi hasa walioko katika timu ya Simba unaweza kuona kabisa kwamba kama siku moja wachezaji wale wa nje wataondolewa kwenye ligi yetu, ligi yetu itakuwa na ladha tofauti na itakuwa kwenye kiwango kidogo kuliko ilivyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ushiriki wa wachezaji wa nje ni mzuri sana, unawapa changamoto wachezaji wetu, lakini niiombe tena Serikali namna ya kulifanya hili ni kuhakikisha kwamba tunapeleka nguvu huku chini ili na sisi tutengeneze wachezaji ambao wanaweza kucheza nje ya nchi ama ambao peke yao kama wataweza kucheza kwenye ligi yetu basi ligi yetu itakuwa na msisimko kama iliyonayo sasa hivi. Lakini bila Serikali kutilia mkazo michezo ngazi hizi za nchini, uwezo wa timu yetu ya Taifa utaendelea kuwa dhahifu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ni hili jambo la BASATA; kwanza niseme kwamba mimi bado niko kwenye majukwaa mengi ya wasanii na asilimia 98 ya wasanii wa nchi hii tunakubaliana mambo mawili; aidha, BASATA inahitaji major reform ama sheria inayowekwa kuundwa kwa BASATA iondolewe kabisa tuwe na chombo kingine kwa ajili ya kulea wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Baraza hili liliundwa mwaka 1984 kwa sheria namba 23 na liliunganisha Baraza la Muziki Tanzania - BAMUTA na Baraza la Sanaa la Taifa kwa wakati huo, na malengo yake ukiyasoma kwenye sheria ya mwaka 1984 ambalo ililiunda unaweza kuona kabisa hayakuwa na walakini, hayakuwa na viashiria, hayakuwa na maelekezo ya moja kwa moja kwamba baraza hili linakwenda kuwa polisi kama ambavyo liko sasa.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa mujibu wa sheria ya mwaka 1984 kazi za baraza ni pamoja na kufufua na kukuza maendeleo na utengenezaji wa kazi za sanaa, kufanya utafiti wa maendeleo kutoa huduma za ushauri na msaada wa kiufundi kwa ajili ya maendeleo na shughuli za biashara na sanaa, kupanga na kuratibu shughuli za sanaa na nyinginezo nyingi, lakini hakuna mahali popote kwenye sheria hii ya mwaka 1984 ambapo baraza lilikuwa na kazi ya kusajili na kuhakikisha kwamba linapitia na kupitisha mashahiri ya nyimbo kama linavyofanya sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, wengine tumefanya muziki kwa takribani miaka 19; sijawahi kukaguliwa wimbo wangu na sijawahi kufungiwa wimbo wangu kwamba nimewahi kutumia lugha ya matusi. (Makofi)

Sasa tunajua umuhimu wa kuangalia maadili na hatuna wasiwasi nao, hatuna matatizo nalo, lakini suala la Baraza kujipa jukumu ambalo linatuongezea urasimu, ambalo linafanya kazi yetu iwe ngumu, wakati halina msaada wowote kwenye maisha ya msanii wa Kitanzania wala sanaa lenyewe ni suala ambalo sisi halikubaliki kwetu.

Mheshimiwa Naibu Spika, sisi hatuombi haki ya kutukana kwenye nyimbo, wala hatuombi haki ya kuchochea, kuleta uchochezi kwenye nyimbo, tunachoomba ni haki ya kutengeneza muziki, kufanya sanaa yetu bila kuwa na vikwazo vingi ambavyo baraza hili kwa sheria hii ya mwaka 2019 linajaribu kuifanya. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi ninachoona ni kwamba Baraza linajaribu kwa nguvu nyingi sana kuichonganisha Serikali na wasanii, hiki kitu wasanii wote nchi hii wamekikataa na tunashukuru hekima za Waziri na Katibu Mkuu wetu wa Wizara hii ambao walikwenda wakahamua kukisimamisha. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninachikiomba ninajua sheria bado ipo na Waziri na Katibu Mkuu wameisimamisha kwa hekima zao kuona namna ambavyo kitu gani kinaweza kufanyika kuirekebisha.

Sasa mimi sitaki kuhitumia hii kama ground ya kushika mshahara wa Waziri, ninachoomba ni commitment ya Waziri wakati hakija kufanya majumuhisho kuonesha commitment ya Serikali kwamba sheria hii inarekebishwa road map ya marekebisho ya sheria hii ili isiende kuendelea kuwakwaza wasanii. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na la mwisho ni suala la COSOTA. Nimefurahi kwamba COSOTA sasa inaamka na pamoja na mambo mengine inaanza kukusanya blanks up levy ambayo ni kodi inayokusanywa kwa sababu ya vifaa vyote ambavyo vinaweza…

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

MHE. HAMISI M. MWINJUMA: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba dakika moja.

NAIBU SPIKA: Haya, malizia.

MHE. HAMISI M. MWINJUMA: Sasa tunachoomba sisi kwa Wizara kuwe na mgawanyo separation ya copyright office na collective management organization, kwa sababu Serikali najua mnaanza kuchukua fedha kutoka media houses mbalimbali, sisi tunaomba tukusanye fedha kutoka sehemu nyingine ambazo zinatakiwa kupewa leseni ya kutumia kazi za sanaa kama mahoteli, kama mabasi, hair saloon na barber shop. Sheria ya Namba 7 ya mwaka 1999 imeshasema haya waziwazi na kabisa hata uki-charge shilingi 7,000/8,000 kwa haya maeneo haya yote na tumeshafanya research unaweza kujikuta na bilioni 54 kwa units ambazo zipo zinazotakiwa kukusanya mapato haya. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, sisi tunaomba wakati Serikali inatusaidia kukusanya kwenye media houses, sisi tukusanye kwenye haya maeneo mengine na tuisaidie Serikali pamoja na mambo mengine kukusanya kodi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, naomba niseme nina grounds kadhaa ambazo naweza kuzitumia kushika mshahara wa Waziri lakini sitaki kuzitumia ninachoomba..

NAIBU SPIKA: Ahsante sana, dakika niliyokuongeza imeisha.