Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Ester Amos Bulaya

Sex

Female

Party

CHADEMA

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru, kwanza na mimi nikiri ni mwanahabari, nilikuwa newsroom takriban miaka sita magazeti ya Uhuru, Mzalendo na burudani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nimeona watu wengi wamejikita katika michezo lakini pia Mheshimiwa Waziri waandishi wako wa habari wanalipwa vibaya sana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, utakubaliana na mimi na Waheshimiwa Wabunge waandishi wa habari wamekuwa wakifanyakazi kubwa sana na Taifa letu linawategemea waandishi wa habari kuielimisha jamii, lakini waandishi hawa wamekuwa na maslahi madogo sana, nani waandishi wa vyombo vya habari vyote vya Serikali na vyombo vya habari binafsi, siyo walioajiriwa tu mishahara yao midogo haiongezwi, hata correspondent journalist na wenyewe wanalipwa vibaya sana hapo nimezungumzia correspondent kwenye print media, sijazungumzia kwenye electronic media/ watangazaji nimezungumzia tu kwneye magazeti. Lakini wote wanalipwa vibaya sana na hawana watu wa kuwasemea.

Mheshimiwa Spika, sisi wanahabari kazi yetu ni kusemea wengine, lakini Bunge hili linapaswa kuwasemea waandishi wa habari wanatumia kalamu zao, wanatumia midomo yao kuhakikisha wananchi wanajua taarifa mbalimbali. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri na Mheshimwia Waziri wa Sera dada yangu pale Jenista baadhi ya vyombo vya habari havipeleki michango. Kwa hiyo, hatma ya waandishi wa Habari baada ya kumaliza kazi zao haieleweki nimekutana tu na baadhi ya wanahabari hapo wachache nje na wenyewe imebidi waanze kufuatilia kama michango yao inaenda, michango yao haiendi kwenye mifuko ya hifadhi. Kwa hiyo, Mheshimiwa Waziri mbali ya maslahi madogo kile wanachokatwa hakipelekwi, hilo nalo naomba ulifanyie kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini Mheshimiwa Waziri tabia ya kufungia fungia vyombo vya habari, tukubali/tukatae vyombo vya habari ni CAG mwingine, tusitake tu kutolewa habari za kufurahisha, lazima tukubali na kukosolewa zote ni habari za kujenga Taifa letu. Kwa mfano unakuta unafanyiwa interview mwandishi wa habari anakwambia Ester usiende huko tutafungiwa sasa unafungiwaje wazo nililolitoa mimi? (Makofi)

Kwa hiyo, kuna shida na ukweli soko la magazeti limekufa, sasa hivi hamna mtu ambaye wengi hawanunui magazeti kwa sababu anaona habari zile zile, habari za uchunguzi saa hivi zimepungua makala za uchunguzi zimepungua hebu hata ukienda kwenye mijadala angalia tathmini mbalimbali zinapotolewa watu wanatoa kwa hofu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, sasa hatusemi kwamba hakuna uhuru usiokuwa na mipaka, lakini tukiwahakikishia hawa waandishi wetu wa habari wafanyekazi zao kwa weledi hata kama wanapotukosoa magazeti haya hayafungiwi fungiwi hovyo, Mheshimiwa Waziri ukifungia gazeti moja ina maana umesimamisha zaidi ya familia 50; zaidi ya wafanyakazi 50 hawana ajira ina maana watoto hawaendi shule unawaweka hizo familia katika hali ngumu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwa mfano tuzungumzie faini imekuwa kama chanzo cha mapato, watu walikuwa wanazungumzia upande wa michezo, hata huku kwenye magazeti, kwenye vyombo vya habari kuna shida, unamtoza mtu faini kubwa mtoze faini kidogo ajirekebishe, lakini siyo faini ikiwa chanzo cha mapato.

Sasa natolea tu mfano mlifungia Wasafi pale Babu Tale Mbunge anajua alivyofanya mpaka Wasafi ikafunguliwa, lakini je, hizi media zingine ambazo hazina watetezi? (Makofi)

T A A R I F A

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, Taarifa. (Kicheko)

SPIKA: Taarifa Mheshimiwa Babu Tale, declare interest.

MHE. HAMISI S. TALETALE: Mheshimiwa Spika, dada yangu Ester sijafanya chochote ni utaratibu umefanywa na Serikali ndiyo maana tumefunguliwa, ahsante. (Makofi)

SPIKA: Pokea hiyo taarifa Mheshimiwa Ester Bulaya.

MHE. ESTER A. BULAYA: Nimetolea mfano lakini anajua tulipokuwa tunakunywa canteen alisemaje.

Mheshimiwa Spika, kama nilivyosema hizi faini zisiwe chanzo cha mapato mnapofungia gazeti moja mbali ya kumuathiri yule mwenye chombo, lakini mnawaathiri hawa waandishi wengine ambao mbali tu ya maslahi yao madogo, lakini pia unamfanya sasa anakosa kabisa kazi, anashindwa kuendeleza maisha yake. (Makofi)

Kwa hiyo nilikuwa naomba maslahi ya waandishi wa Habari tabia ya kufungia fungia vyombo hebu acha waandishi wa habari wafanye kazi kwa uhuru, tukosolewe, tujenge taifa letu, tusipongezwe tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini pia mmezungumzia hapa mpira, mmoja tu ndiyo amezungumzia timu ya wanawake, tena amegusa tu, hapa mnapozungumzia uwekezaji kwenye mpira wa miguu timu ya mpira wa miguu ya wanawake imekuwa kama mtoto yatima kwenye Taifa hili mbali ya kufanya vizuri timu ya Taifa ya Wanawake imekuwa ikichangiwa changiwa, aibu. (Makofi)

Lakini Mheshimiwa Waziri kwenye kurudisha michezo mashuleni hakuna programu ya timu ya mpira wa miguu ya wanawake hivi kweli ndiyo tunataka timu zetu zikashindane na Brazil, tukashindane na Senegal ambazo zinaenda ku- compete kwenye kombe la dunia. (Makofi)