Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

Hon. Stanslaus Haroon Nyongo

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Maswa Mashariki

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi.

Mheshimiwa Spika, kwanza kabisa nichukue fursa hii kuwapongeza sana Simba Sports Club, kwa kuweza kufika katika nafasi ya robo fainali ya kombe la Afrika kwa maana ya African Champions League na hili nichukue fursa hii vilevile kuwapongeza Young African kwa sababu kwa kitendo cha Simba kufika katika robo fainali itawafanya Yanga kama watafanikiwa, basi na wao kuwa na nafasi ya pili kwa maana ya kwenda katika mashindano ya Champions League. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ni nafasi ambayo imetengenezwa na Simba, kwa hiyo, niwapongeze sana na wao kama watafanikiwa basi wajue kwamba Simba imefanya kazi nzuri na wao kupata nafasi ya kwenda Champions League. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini niendelee tu kuwaambia watu wa CAF ikiwezekana wabadilishe kanuni kwamba, anayefanikiwa kusababisha timu nyingine kwenda kwenye mashindano hayo, waangalie hizi kanuni upya isiwe nafasi ya pili ikiwezekana huyu aliyeshinda ndio achague nani wa kwenda naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nasema hili kwa sababu haiwezekani mtu anayekuzomea, anapokea wageni ambao ni maadui zako yeye ndio anawapokea airport na kuwa- support halafu mwisho wa siku tukishinda yeye apate nafasi ya kuendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tutawaomba CAF waangalie namna nyingine ya kupanga kwasababu, haiwezekani anayetuzomea twende naye. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo niendelee na mchango wangu, niwaombe tu Watanzania wote, niwaombe Wabunge na watu wote kwa ujumla. Tunawanamuziki wazuri sana Afrika, lakini Diamond ameonesha kuwa ni mwanamuziki ambaye ameonekana duniani kote na leo ametajwa kuwa ni mmoja wa wanamuziki bora duniani wanaokwenda kupigiwa kura. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Diamond katika ile BET Award yaani Black Entertainment Award ametajwa kwamba ni mmoja wa nominee yaani wanaopendekezwa wapigiwe kura. Na niseme tu waliotajwa duniani yuko mwanamziki anaitwa Aya Nakamura wa Ufaransa, Burna Boy wa Nigeria, Diamond wa Tanzania, Emicida wa Brazil, Headie One wa UK, Wizkid wa Nigeria, yaani sijui na nani mwingine huyo wa UK. Kuna Youssoupha wa Ufaransa. Kwa Afrika wapo watatu na kwa Afrika Mashariki ni mwanamuziki mmoja tu kutoka Tanzania ambaye ni Diamond Platinum. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini cha kusikitisha ameanza kupata vikwazo tena kutoka kwa watanzania wenyewe na kibaya zaidi wanaingiza hadi masuala ya kisiasa, na kibaya zaidi wanamsema kwa sababu ali-support CCM, wana-CCM mliomo humu na wana-CCM Tanzania wote tumpigie kura Diamond. Sasa hivi sio suala la chama, hili ni suala la Tanzania, tumpigie kura nyingi, tumpigie kampeni aweze kushinda na hii atakuwa amekwenda kutanga nchi yetu katika nyanja za muziki duniani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niendelee na mchango wangu vilevile kuhusiana na masuala haya ya TBC. TBC wamefanya kazi nzuri, niishukuru Serikali imeweza kutoa shilingi bilioni tano kwa ajili ya kuongeza usikivu wa TBC. Tunawaomba TBC hizo shilingi bilioni tano mlizopewa mzifanyie kazi usikivu uongezeke, wananchi wanataka kusikia habari za uhakika kutoka TBC. Kuna mikoa ambayo ipo pembezoni mwa nchi yetu usikivu sio mzuri wa TBC, watu wanasikia redio za nchi za jirani. Tunaomba muongeze usikivu ili kusudi watanzania waweze kupata habari za uhakika kutoka TBC.

Mheshimiwa Spika, kuna suala ambalo Mheshimiwa Tarimba alikuwa analiongea hapa kuhusiana na masuala ya mpira wa miguu. Ni lazima tufike sehemu tuamue kuna timu ya Taifa na mashindano ambayo yanashirikisha timu za Taifa, lakini kuna ligi za ndani pamoja na champions league katika mabara yetu. Sisi Tanzania tuna Simba na Yanga zimejitangaza vizuri kuna Azam na timu nyingine. Vilevile kuna timu za Taifa ambazo kwa mfano timu za Nigeria na nchi nyingine wamekuwa na timu nzuri sana za Taifa. Niombe tu kueleza kwamba timu za ligi zinazocheza ligi, hii siyo mpira wa kawaida inaitwa commercial football ni mpira wa kibiashara. Uingereza leo hana timu nzuri kweli World Cup, lakini amejitangaza kwa maana ya ligi yake imekuwa ni ligi maarufu duniani na amejikita hapo tu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tunaona timu za Waingereza zimeingia fainali champions league, Chelsea na Manchester City na wanaingiza fedha nyingi sana. Hata sisi Afrika, Simba tumekomea robo fainali sawa, lakini Simba ingechukua ubingwa wa champions league ingeingiza fedha nyingi, ingetangaza Tanzania. No matter what katika timu ya Taifa hatuna timu nzuri, lakini tunapojikita kwenye commercial football tunaangalia kwenye champions league tunakwenda kufanya nini. Sasa niwaomba TFF, niwaombe na Wizara msi- limit sana wachezaji kuajiri wachezaji kutoka nje ya nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kama Azam, kama Simba, kama Yanga amekwenda kwenye commercial football ambayo ni ligi kuu hapo ni biashara hata kama angeweza kuleta wachezaji kutoka sehemu nyingine alete lengo lake ni kwenda kushinda champions league ili aingize fedha atangaze na nchi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ukiangalia timu kwa mfano ile timu ya Congo ile TP Mazembe ambayo ilikuwa inakwenda kushinda inakwenda kwenye champions league ilikuwa inaingiza wachezaji, ilikuwa inasajili wachezaji wakati mwingine hata timu nzima, angalia Real Madrid alikuwa anasajili wachezaji sio kutoka Spain, alikuwa anasajili wachezaji kutoka Portugal na maeneo mengine analenga kwenda kwenye champions league kwa sababu akishinda tayari anaingiza fedha na ameitangaza Spain.

Mheshimiwa Spika, sisi Simba tukishinda ni Tanzania no matter Morison anatoka wapi? Sasa tukitaka kutengeneza timu ya Taifa twende kwenye football academy.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, tutengeneza football academy hizo zitakwenda kutengeneza timu ya Taifa.

T A A R I F A

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, Taarifa.

SPIKA: Unapewa taarifa Mheshimiwa Haroon Nyongo.

MHE. MUSSA R. SIMA: Mheshimiwa Spika, pamoja na mchangiaji kueleza vizuri sana lakini lengo la Serikali nakupa taarifa tu, ni kuimarisha ligi yetu na kuhakikisha vijana wetu ndio wanakuwa na uwezo mzuri kabisa kwa ajili ya soka letu hili badala ya kuleta vijana wengine kutoka nchi zingine. Nadhani lengo ndio hilo.

SPIKA: Je, uko tayari na vijana wa Tanzania wasiende nje pia kwenye nchi za wenzetu? Kwa taarifa hiyo unapewa Mheshimiwa Haroon Nyongo. (Makofi)

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, ahsante sana umeuliza swali la msingi zuri sana, kwamba je, wachezaji wetu wasiende nje?

Mheshimiwa Spika, leo Mbwana Samatta amekwenda kucheza huko nje, amekwenda kucheza hadi Aston Villa naomba niwaeeleze mbona Samatta angepeleka Aston Villa ingekwenda kucheza champions league ya Ulaya ina maana ile timu ingeshinda wale wangejitangaza kama Waingereza wala siyo Mbwana Samatta kutoka Tanzania. The same na sisi timu yetu ikifika huko tutaitangaza kwamba ni Tanzania, Simba imeshinda au Yanga imeshinda iliyoshinda champions league ni timu kutoka Tanzania no matter hawa wachezaji waliomo humu wanatoka nje ya nchi nyingine.

Mheshimiwa Spika, kingine timu ya Taifa ninachotaka kusema, tutengeneze football academy nzuri mfano mzuri ni Zambia ilipopata ajali kule Gabon watu walivyofariki karibu timu nzima wale makocha walirudi kwenye football academy zao wakawa kumbe tayari wana-infrastructure nzuri ya kutengeneza wachezaji wao, wakatengeneza timu nyingine ikaenda kwenye mashindano hayo hayo na timu ile ikafika hadi fainali, ikaenda kufungwa na Nigeria. Wasingekuwa na football academy nzuri wasingekuwa na timu bora hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba niwaeleze hakuna timu ya Taifa inayotengenezwa na timu za ligi, timu ya Taifa inatengenezwa na Serikali kwa kutengeneza miundombinu mizuri na walimu wazuri wanaoweza kutengeneza na ukishapata wachezaji wazuri utawauza sasa kwenye ligi yako ya ndani kwa maana hiyo inayochezwa champions league na wachezaji wengine utawauza nje ya nchi ikacheze kwenye vilabu vingine. Ukizungumzia timu ya Taifa ndio maana leo utaizungumzia Brazil na Ujerumani, lakini ukizungumzia ligi bora inayoweza kuifikisha timu kwenye champions league ni Uingereza. Watu tubadilishe mindset zetu, tuangalie kama tunaamua kwenda kwenye commercial football twende na kama tunaamua kutengeneza timu Taifa ni jukumu la Waziri na Serikali yake.

Mheshimiwa Spika, kuhusiana mchezo wa Simba na Yanga; amezungumza kidogo Mheshimiwa Gulamali hapa. Derby ni mechi za watani wa jadi na hizi mara nyingi zinakuwa na sifa ya kukusanya watu wengi na kuteka hisia za watu. Ukichukua ten derbies za Afrika; ya kwanza alikuwa anajinanii hapa ya kwanza Al-Ahly pamoja na Zamalek; ya pili ni Kaizer Chiefs na Orlando Pirates; ya tatu ni Club Africana na Esperance ya Tunisia; ya nne ni Wydad Casablanca na Raja Casablanca za Sudan; ya tano kwa Afrika ni Simba na Yanga ambayo ni Kariakoo derby inafuatiwa na ya sita ya kule Kenya wanajiita Mashemeji derby. Hizi zinabeba hisia za watu na mara nyingi huwa zinasababisha fujo na sintofahamu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, Serikali ina jukumu la kulinda hizi mechi, mechi ya Simba na Yanga sio suala la vilabu ni suala la Serikali, lazima muangalie usalama, muzipe usalama na ulinzi wa kutosha. Kwa sababu hizi mechi zinavuta hisia za watu wapenzi wa mpira ndani na nje ya nchi. Kuna wapenzi kutoka Zambia, Kenya, Rwanda, Burundi walikuwa tayari kuangalia ile mechi ikasogezwa mbele, mimi nakubali kuwa Yanga walichukua uamuzi sahihi, lakini na wao wawe wazalendo ilisogezwa kwa masaa mawili wangevumulia tu wapate kichapo chao. (Makofi)

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Nyongo.

MHE. STANSLAUS H. NYONGO: Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ahsante sana. (Makofi)