Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Hussein Mohamed Bashe

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Nzega Mjini

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

0

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

NAIBU WAZIRI WA KILIMO: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa fursa hii na kutujalia sote afya na kushiriki kujadili mjadala huu unaohusu maslahi ya wananchi wa nchi yetu. Vilevile nitumie nafasi hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa dhati kabisa kwa michango yao ya hizi siku mbili na maoni waliyoyatoa.

Mheshimiwa Spika, ili nisipoteze muda, niende moja kwa moja katika hoja ambazo Waheshimiwa Wabunge wametoa. Hoja ya kwanza ambayo imejadiliwa kwa uchungu na maoni mengi ya Waheshimiwa Wabunge ni hoja ya stakabadhi ghalani. Kama unavyofahamu stakabadhi ghalani inatekelezwa kwa mujibu wa sheria. Mfumo wa stakabadhi ghalani ni moja kati ya mifumo ambayo inatumika katika mauzo ya mazao. Wizara ya Kilimo sio mara moja wala mara mbili tumesema hadharani msimamo na mwelekeo wa Wizara ya Kilimo katika suala la stakabadhi ghalani. Naomba nitumie nafasi hii kuliambia Bunge lako Tukufu na kuwaambia wakulima wa nchi hii kwamba msimamo wetu tutalinda haki za wakulima na tutafanya maamuzi kwa maslahi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kuhusu suala hili, hatuwezi kutumia mfumo wa stakabadhi ghalani katika kila zao. Kila zao lina tabia na mfumo wake. Yapo maeneo ambayo hatuwezi kuuondoa mfumo wa stakabadhi ghalani kwa sababu umefanya vizuri. Mfumo wa stakabadhi ghalani umefanya vizuri katika zao la korosho, hatuwezi kuuondoa mfumo wa stakabadhi ghalani wala mfumo wa ushirika. Mfumo wa stakabadhi ghalani umefanya vizuri katika zao la tumbaku, hatuwezi kuuondoa mfumo wa stakabadhi ghalani na mfumo wa ushirika katika zao la tumbaku. Tutarekebisha changamoto zilizoko katika eneo hilo lakini sio kuuondoa mfumo wa stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini hatuwezi kutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani kwenye maeneo ambayo hakuna miundombinu ambayo imeainishwa kisheria na kikanuni. Tumesema hatuwezi kutekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani katika Mikoa ya Dodoma, Singida, Manyara, Songwe na Katavi. Katika mikoa yote hii hatutekelezi siyo kwa nia mbaya bali ni kwa sababu mikoa hii haina mifumo ambayo inaweza kumfanya mkulima akafaidika na mfumo wa stakabadhi ghalani. Ni jukumu letu kuendelea kuijenga mifumo hiyo na wakati ukifika tutatoa elimu na tutaenda kwenye stakabadhi ghalani, lakini siyo sasa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini yako mazao hatuwezi kupeleka katika mfumo wa stakabadhi ghalani sasa hivi mfano ni ufuta, choroko, dengu na mbaazi. Hata katika mikoa ambayo tuna-practice mfumo wa stakabadhi katika Mikoa ya Shinyanga, Simiyu, Mara na mikoa ambayo inazalisha pamba, hatutatekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani katika dengu wala choroko, tutaweka nguvu katika mfumo wa ushirika na mfumo wa stakabadhi ghalani katika maeneo hayo. Kwa hiyo, nilitaka nimtoe hofu Mheshimiwa Mulugo, hatutatekeleza mfumo wa stakabadhi ghalani. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili, mwenye mamlaka na instrument na kanuni ya kutoa maelekezo zao gani liingie katika mfumo wa stakabadhi ghalani ni Waziri wa Kilimo. Huyu ndiye mwenye mamlaka. Sisi kama Wizara na nitumie nafasi hii kuwaambia Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote, atakayetoa mwongozo zao gani linaingia katika mfumo wa stakabadhi ghalani ni Waziri wa Kilimo na wala siyo mtu yeyote. Kwa hiyo, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge ambao walikuwa wamedhamiria kushika shilingi kwa sababu ya hoja ya mfumo wa stakabadhi ghalani kama kulitokea makosa tutarekebisha. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, mfumo wa stakabadhi ghalani kote unatumika kwa ajili ya financing. Sisi kama Wizara tunashirikiana na wenzetu wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya kufanya mapitio na kuungalia mfumo huu. Tunafanya pilot na benki za biashara, tumefanya Igunga na Katavi, sasa hivi wakulima wa mpunga wanahifadhi mipunga yao katika ghala, wanapewa risiti, ile risiti inaenda katika benki na kuwa discounted, anakuwa na fedha, akiwa na fedha wakati anasubiri zao lake liongezeke bei ataliuza wakati atakapoamua yeye.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nirudie tena kwamba stakabadhi ghalani itatekelezwa katika maeneo ambayo imeonesha mafanikio. Hatuwezi kuwa na mfumo mmoja ukahudumia mazao yote, tutatengeneza mifumo ya kuuza mazao kutokana na hitaji la eneo na zao lile. Kwa hiyo, niwaombe Waheshimiwa Wabunge walielewe hili na sisi tutaendelea kuwasiliana na wenzetu katika Mamlaka za Serikali za Mitaa wasiweze kubughudhi wanunuzi wanaonunua ufuta katika Mkoa wa Dodoma, wanaonunua mbaazi, choroko na dengu, mazao haya madogomadogo tunayaacha ili competition ichukue nafasi yake yaweze kukua na volume iongezeke. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo tuna zao la soya, kama nchi tumepata mkataba wa miaka mitatu wa kuuza zao la soya katika nchi ya China na wakulima ndio wameanza kwenda kulima. Itakuwa ni jambo la ajabu tunaenda kuchukua zao la soya ambalo linalimwa kule Songea Vijijini, mkulima anapewa na mnunuzi Sh.1,000/= bei ya shambani halafu tunalazimisha liingie kwenye stakabadhi ya ghala ili liingie katika mfumo wa ushirika aanze kukatwa tozo mbalimbali siku ya mwisho anaondoka na Sh.800/=. Hii hatutaruhusu Waheshimiwa Wabunge na ninataka niwape commitment ya Wizara ya Kilimo kwamba tutajenga mifumo ya masoko kutokana na zao na mahitaji. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, korosho iteandelea kubaki katika mfumo wa stakabadhi ghalani katika Mikoa ya Kusini. Tarehe 29 tunazindua mfumo wa kuuza ufuta katika Mkoa wa Lindi na tutauza kwa stakabadhi ya ghala kwa sababu umeonesha mafanikio katika maeneo hayo, hivyo hatuwezi kuua mfumo huu. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge tusiuwe mifumo tunayoijenga, turekebishe matatizo yaliyopo katika mifumo bila kuathiri mambo mengine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo lingine ambalo limeongelewa na Waheshimiwa Wabunge kwa uchungu mkubwa ni suala la export levy kwenye zao la korosho. Sisi kama Wizara ya Kilimo tunaamini mazao haya ya kilimo yana uwezo wa kujiendesha yenyewe. Takwimu, tathmini na experience imeonesha kwamba wakulima wanaweza kujiendesha wenyewe tukiwajengea mazingira mazuri na sisi ndiyo kazi yetu. Kwa hiyo, nataka niwahakikishie kwanza suala la intervention ku-disturb mifumo iliyojengwa vizuri hatuwezi kulirudia jambo hilo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini suala la export levy, nataka nitoe commitment katika Bunge lako kwamba tunalichukua tunaenda kulifanyia kazi, lakini sasa hivi tunaenda shambani. Tunazo takwimu zao la korosho lilifikia metric tons 320,000 wakulima walipewa pembejeo, uzalishaji wa korosho mkulima akienda shambani ili aweze kuzalisha korosho kwa gharama za input peke yake anatumia Sh.327/= kwa kilo, gharama zake za uzalishaji.

Mheshimiwa Spika, mimi namshukuru sana Mbunge wa Liwale na Mheshimiwa Nape, msimu uliopita baada ya maua ya korosho kuanza kuanguka walipiga kelele tukatuma watu wa TARI Naliendele waende wakafanye study kwa nini maua ya korosho yanaanguka. Spika nawe ni mkulima wa korosho unafahamu changamoto ya kuhudumia zao la korosho, hatuwezi kumuachia mkulima wa korosho mfumo wa huria katika ku-finance input, ni lazima tutafute njia ya kumpunguzia gharama.

Mheshimiwa Spika, dude lile la kupulizia peke yake, mimi nimefika shambani kwako nimekukuta wewe ukihangaika na Afisa Magereza wa Gereza la Mpwapwa, lile bomba peke yake linauzwa shilingi 1,000,000, mkulima gani anaweza kulinunua bomba lile, ni difficult.

Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge tukiwa wakweli ni lazima tutafute njia ya ku-finance namna hii. Hatua ya kwanza tuliyochukua ni kuanzisha bulk procurement system. Kule Kusini na Bunge lako lifahamu, mkulima wa korosho inapofika wakati wa kwenda kununua sulphur anaenda kukopa. Akienda kujiandikisha kwamba anataka kukopa kuna microfinance ziko kule, sulphur ambayo mkulima anaenda kukopa kwenye market price ni shilingi 32,000 lakini wakulima wananunua mpaka shilingi 40,000 mpaka shilingi 50,000.

Mheshimiwa Spika, akienda kukopa kwenye microfinance anajaza idadi ya mifuko anayotaka halafu yule mwenye microfinance anaenda kwa supplier anamwambia nipe sulphur, yeye anaichukua kwa shilingi 32,000 halafu anampa mkulima kwa shilingi 40,000 halafu ile shilingi 40,000 inatozwa interest ya 2% kila mwezi. Wanao-benefit ni service provider na wala sio farmer. Tumechukua hatua, tumeamua safari hii vyama vyote vya ushirika vimeleta mahitaji, tumekitumia chama kimoja, bei ya sulphur imeshuka mpaka shilingi 29,750. Kwa kukokotoa kwetu huku katika market rate mkulima alikuwa anatumia shilingi 300 kwa kilo kwenye input.

Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, nataka niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge la kwanza, suala la export levy tunaenda kulifanyia kazi, tumewasikia, tutatafuta solution, lakini wakulima watagawiwa pembejeo zote kutokana na mahitaji yao. Kwa mara ya kwanza mpaka sasa sekta hii inadaiwa zaidi ya shilingi bilioni 30. Sisi sote tunafahamu, Mheshimiwa Katani na Mheshimiwa Nape wanafahamu, kila mmoja anafahamu kule kwenye korosho mkulima akivuna anaeenda kukopa kwenye chama cha msingi ni Hussein, anayeenda kuuza ni Nape. Matokeo yake sekta yote inadaiwa, mkulima anadaiwa, chama cha ushirika kinadaiwa, Bodi ya Korosho inadaiwa, sekta haikopesheki, taasisi za fedha zinajitoa kuhudumia sekta hii. Kwa hiyo, njia pekee na sisi tuwaahidi kwamba tunaamini katika kuanzisha mifuko ya kuendeleza mazao, hiyo ndio njia itakayomsaidia mkulima. Kwa hiyo, hii hoja ya export levy tunaichukua tunaenda kuifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, leo hapa tumejadili suala la korosho ya Pwani. Kwa muda mrefu humu ndani tunazungumzia korosho ya Pwani haina ubora, kwa nini haina ubora? Majibu yanakuja kwamba inapata unyevu. Korosho ya Pwani inapata unyevu, iki-mature inakuwa nyeusi.

Mheshimiwa Spika, Pwani kuna mvua nyingi. Kwa hiyo, kama Wizara tumechukua hatua gani ambayo tunaanza kuitekeleza sasa hivi? Vyama vyote vya msingi na nimshukuru sana Mheshimiwa Ulega, Mheshimiwa Mchengerwa na Mheshimiwa Twaha, safari hii tumeamua wakulima wote wa Pwani kuanzia mwezi ujao vyama vya msingi vyote tutavigawia maturubai kwa ajili ya kuanikia korosho zao, hili ni jambo la kwanza. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo la pili, katika sekta ya korosho kuanzia Pwani, Lindi, Mtwara mpaka Ruvuma wana AMCOS 623, tumeamua kila AMCOS tutaigawia bomba kwa ajili ya kupulizia korosho za wakulima wao kwa sababu watu wana-make profit in the middle. Tutatumia mifuko ya mazao ku-finance na ku-subsidize input kwenye sekta ya kilimo na hili linawezekana. Kwa hiyo, tunaomba Waheshimiwa Wabunge mtupe fursa tuweze kulifanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, suala la export levy tumelichukua, sasa hivi tunaenda kwenye msimu na tutalifanyia kazi. Tutajadiliana ndani ya Serikali ili tuweze kupata solution ambayo haitamuumiza mkulima.

Mheshimiwa Spika, niongelee suala la tumbaku. Takwimu zinaonesha tumbaku ilifika metric tons 120,000. Mimi nishukuru humu ndani kwa siku hizi mbili nimejifunza, jedwali lile linaonesha trend ya tumbaku kwa kipindi cha miaka kumi, kuanguka kule kwa tumbaku hakujasababishwa na mkulima hata mmoja. Humu ndani tumekuwa tukisikia kauli kwamba korosho, tumbaku, pamba na kahawa ni mazao ya siasa, sio kweli, haya ni mazao ya kibiashara. Kwa hiyo, let us put aside politics kwenye kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tumbaku hii imeporomoka kwa sababu ya policy zetu mwaka 2014-2015 tulienda kushtaki makampuni yote na pressure ilitoka ndani tukayapiga faini ya trilioni saba TLTC aliondoka kwenye nchi hii tunachukua hatua gani. Mwaka jana kupitia Bunge lako Tukufu hili, tulibadilisha sheria ya LCC, tukawaondolea faini zote makampuni haya. Wakalipa tozo ya shilingi dola 300,000 kutoka trilioni saba it was unfair na haikuwa haki, hawa wanafanya biashara matokeo yake makampuni yaka-pull out sekta ya tumbaku ikaanguka mpaka tani 36,000 mwaka jana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini kwa hatua tulizochukua mwaka huu wakulima wa tumbaku wamepeleka sokoni tani 67,000 ambazo tumeanza kuziuza. Just kwa maamuzi madogo tu ya kufuta tozo tulizowapiga, faini kuwapiga na kukaa nao mezani wanunuzi wamekuja zao letu tunalouza safari hii ni tani 67,000 kutoka tani 39,000 na sisi tuwaahidi kwamba tutalinda wakulima na tutawalinda wanunuzi wanaonunua mazao ya kilimo hakuna njia nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo la pili ambalo tunafanya kwenye tumbaku, mkulima wa tumbaku zao za tumbaku linakuwa determined na biashara ya dunia unapozalisha tani moja ya tumbaku mnatakiwa mpande miti 600 lazima wanunuzi wajiridhishe. Kinachotokea mkulima anakatwa 0.092 dola kwa kilo kwa ajili ya ku-finance mfumo wa kupanda miti. Nataka nikwambie kwa mwaka wakulima wa nchi hii wanachangia bilioni 25 lakini miche hile haipandwi popote tumechukua hatua tumebadilisha mfumo sasa hivi fedha zile zitakusanywa kwenye one account tutatangaza tender tutaingia makubaliano na TFC miche itapandwa na itaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kwasababu hivi zilikuwa ni shughuli za watu wanagawana viongozi Mikoani Mheshimiwa Kakoso anafahamu watu wanaotoka Katavi wanafahamu kilichotokea baada ya maamuzi haya tunabadilisha mfumo wa uharamiaji kwenye tumbaku. Mkulima wa tumbaku anakwenda kukopa yeye na AMCOS yake at the interest of 7 percent USD hawezi kupata faida, atapata hasara tu tumeamua tumebadilisha mfumo kwanza procurement ya input yote tunaagiza kutoka kwa producers hatutotumia watu wa kati. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, la pili tumesema kwamba tunatumia LC model kwamba supplier anapeleka pembejeo tunamlipa baada ya siku 360 baada ya mnada mkulima anapata bila riba na tumevizuia vyama vyote vya ushirika kwenda kukopa katika benki zinazozalisha tumbaku kwa dola na kwa riba kwa sababu mbolea tutapeleka, dawa tutapeleka, supplier atapewa LC baada ya siku 360 mtoa huduma atapata fedha yake na tumekubaliana na taasisi za fedha hili tunalifanya.

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo nilitaka niliongelee ni zao la pamba, zao letu la pamba lilidondoka mpaka tani 120,000 na sisi wote tunafahamu na graph ile inaonekana tulifika tani 348,000 mwaka 2019 mkulima alivyopewa mbegu alipewa dawa tukabadili policy zao likadondoka, hatua gani tumechukua safari hii, cha kwanza tumewagawia wakulima wa pamba wote mbegu bila kulipia, la pili tumewagawia dawa zote bila usumbufu wowote tumekaa na wanunuzi na vyama vya ushirika lakini tumewapatia input hizi bila wao kwenda kukopa benki. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, benki zimetupa LC watoa huduma wamepeleka pembejeo baada ya kupeleka pembejeo zitalipwa pembejeo baada ya mkulima kuuza zao lake. Mwaka huu tunavuna metric tonnes kati ya 350,000 hadi 400,000 na mkulima ataenda kuuza kwa bei ya kuanzia 1050 bila ukatwa hata shilingi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nataka niliombe Bunge lako Tukufu tupo tayari kufanya mabadiliko, tupo tayari kuchukua hatua tutakubaliana na maoni na ushauri wenu tusaidiane kwa sababu jambo hili hatuwezi kulifanya peke yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, jambo jingine ambalo nilitaka niliongelee ni suala la umwagiliaji ni kweli bila mfumo mzuri wa umwagiliaji hatuwezi kupiga hatua. Wizara kwanini tunafanya tathmini? Tunafanya tathmini kwa sababu experience yetu ya muda mfupi imetuonesha kwamba tunahitaji kufanya mabadiliko makubwa kwenye tume yetu ya umwajiliaji, tutawaleteeni sheria hapa. Tunataka kuibadilisha tume kuwa wakala wa umwagiliaji kuwa agency kama ilivyo TARURA kama zilivyo nyingine. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini la pili tunabadili mifumo kwasababu hii mifumo ya umwagiliaji tunatumia gharama nyingi kujenga mradi mmoja tumeamua katika bajeti hii ambayo mtatupitishia Waheshimiwa Wabunge la kwanza tumeanzia kitu kinaitwa irrigation development fund ambayo kwa kutumia fedha zetu za ndani tumetenga zaidi ya bilioni 30.

Mheshimiwa Spika, lakini hatua ya pili tutakayoichukua ni kwamba tume ya umwagiliaji tumewaagiza kwamba watangaze tender kwa ajili ya kununua vifaa, ili kuanzia mwaka huu wa fedha kwenda mbele kazi yetu ya kwanza pamoja na ku-repair miradi iliyopo lakini nikuchimba mabwawa maeneo yote ambayo tunaona kwamba kuna uwezekano wa kuhifadhi maji, hii ndio itakuwa priority yetu tutaangiza vifaa tutakuwa navyo wenyewe tumefanya pilot project kwenye mradi wa Ruaha chini na Mheshimiwa Mbunge yule pale shahidi tumetumia excavator zetu wenyewe bila kutumia fedha nyingi kwa ajili ya kuu-repair ule mradi.

Mheshimiwa Spika, nilitaka niliongelee jambo jingine kuhusu suala la mahindi, ni kweli mwaka jana mahindi yalifika mpaka kilo 1,000 -1,100 lakini sasa hivi mahindi yameonekana bei imeshuka. Nashukuru nimalizie tu kuwaambia waheshimiwa Wabunge kwamba tunaamini kwamba bila kui-engage sekta binafsi katika sekta ya kilimo hatuwezi kwenda mbele na sisi tutajenga mazingira kuhakikisha kwamba sekta binafsi inakuwa sehemu ya safari ya kilimo ili tuweze kupiga hatua. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, nashukuru naunga mkono hoja. (Makofi)