Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

Hon. Judith Salvio Kapinga

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Kilimo

MHE. JUDITH S. KAPINGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi. Mkoa wa Ruvuma ni mojawapo ya mikoa inayoongoza kwa uzalishaji wa chakula nchini. Kwa nini Mkoa wa Ruvuma unaongoza ni kwa sababu tuliwaambia Wanaruvuma nendeni mkalime muongeze chakula katika nchi hii na walitumia jembe la mkono na mbinu duni za kilimo na mpaka mwaka jana wakaongeza tani 50,628 za mahindi kwa ajili ya akiba ya chakula cha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini tuliwaambia Wanaruvuma nyie ni kati kati ya mikoa mnayozalisha mazao ya chakula kwa wingi katika nchi hii. Mwaka jana waliongeza ziada ya chakula tani 877,048 kwa kuwa mahitaji ya chakula ya kimkoa yalikuwa tani 469,172 na wao Wanaruvuma kwa mikono yao walizalisha tani 1,346,220.

Mheshimiwa Spika, leo hii baada ya kuwapetipeti sana wazalishe mazao ya chakula kwa ajili ya akiba ya nchi hii, tumewasahau. Tumesahau jasho walilolitoa kwa dhati ya mioyo yao kulima, tumesahau nguvu waliotumia kwa mikono yao kulima na leo hii wanalala na mahindi yao ndani, wanahangaika na mahindi yao ndani, wanalia na mahindi yao ndani. Kwa takribani miaka mitatu hakuna soko la mahindi Wilayani Mbinga na Mkoani Ruvuma kwa ujumla huku tukijua Mkoa wa Ruvuma ndiyo unaozalisha kwa kiasi kikubwa mahindi na chakula cha nchi hii. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naongea haya kwa uchungu sana kwa sababu wana Ruvuma wamekuwa disparate. Mwaka jana akatokea tajiri tapeli anayejulikana kwa jina la Njako akaenda pale Mbinga Kigonsera akachukua mahindi ya wakulima yenye thamani ya shilingi bilioni 5 na mpaka leo hii tunapozungumza tunaenda kwenye mzunguko mwingine wa kuuza mazao mpaka leo wakulima hawajapata fedha. Vilevile mpaka leo hawana soko ambalo wataenda kuuza mahindi yao.

Mheshimiwa Spika, wakati haya yote yanafanyika NFRA ambao wao wanasema wana jukumu la kununua mazao kwenye mikoa inayozalisha sana walikuwepo na hawajawahi kununua hata debe moja la mahindi Wilayani Mbinga. NFRA ambao wao wanasema wana jukumu la kununua mazao kwenye mikoa inayozalisha sana, wameweka vituo kwenye miji wamegeuka ma-God father, wanasubiri mkulima atembee kilomita 60, 100, 200 aende kuwapelekea gunia zake 10 za mahindi. Mkulima huyu ataweza vipi kwa sababu mpaka aende kilometa 100 gharama zote za uzalishaji zimeisha pale. NFRA watuambie kama wao wamegeuka ma-God father sisi tunataka usuluhisho wa masoko ya wakulima kwenye nchi hii ikiwemo Mkoa wa Ruvuma. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, kinachosikitisha zaidi wananchi wa Mkoa wa Ruvuma wamelima kweli kweli mahindi mwaka huu, wananchi wa Mbinga wamelima mahindi kweli kweli, kuna kizungumkuti mwaka huu wanaenda kuuza wapi? Kwa hiyo, nataka nimwambie Mheshimiwa Waziri leo hapa nitamkamatia shilingi yake. Mwaka jana tumetapeliwa, fedha zetu hazijarudishwa mwaka huu bila kutuambia tunaenda wapi kuuza mahindi yetu tunakamata shilingi yake hapa Mheshimiwa Waziri. Kwa hiyo, nakupa taarifa kabisa uje na majibu yanayoeleweka kwa wananchi wa Ruvuma na Mbinga kwamba mahindi yetu tunayapeleka wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, tunamshukuru Mheshimiwa Rais anazunguka nchi jirani kwenda kuongea na majirani zetu kuweza kujua mahindi yetu tunayauza wapi? Kinachotusikitisha wataalamu wetu wamekaa wanamshangaa Mheshimiwa Rais, yaani Mheshimiwa Rais kashatafuta masoko wanategemea mkulima atabeba gunia zake 10 aende akauze mahindi yake Malawi au Msumbiji, wataalamu wetu mnatuangusha. Haiwezekani mpaka tuje hapa tulalamike ndipo mtafute suluhu ya matatizo yetu, mlipaswa kuyaona mapema kabisa kwa sababu msimu wa mahindi sasa ndiyo umeanza. Sasa ndiyo tunataka Mheshimiwa Waziri atuambie tunaenda kuuza wapi sisi mahindi yetu wananchi wa Ruvuma kwa sababu tumechoka na kutapeliwa na kwa muda mrefu sasa tunahangaika huku na huku. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, naomba nimkumbushe Mheshimiwa Waziri Ilani yetu ya Chama cha Mapinduzi inasemaje kuhusiana suala la kilimo. Inasema: “Chama cha Mapinduzi kinatambua kwamba mageuzi ya kujenga uchumi wa viwanda ni lazima yaendane na mageuzi ya kuongeza tija kwenye kilimo”. Namkumbusha Mheshimiwa Waziri Ilani ya Chama chetu inasema nini kwenye masuala ya kilimo. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini naomba nimalizie kwa kumnukuu Mwalimu Nyerere alisema kama ifuatavyo: “Tarmac roads, too, are mostly found in towns and are of especial value to the motor-car owners. Yet if we have built those roads with loans, it is again the farmer who produces the goods which will pay for them”. Tutawalinda wakulima wa nchi hii Mheshimiwa Waziri tunaomba majibu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, ahsante, naunga mkono hoja. (Makofi)