Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

Hon. Festo Richard Sanga

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Makete

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Mifugo na Uvuvi

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuchangia Wizara hii ya Mifugo na Uvuvi; cha kwanza nipende kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba nzuri ambayo ameiwasilisha, lakini kubwa ambalo nataka nizungumzie sehemu mbili; nataka kuzungumzia kuhua NARCO, lakini pia nizungumzie kuhusu Bodi ya Maziwa ambayo hiko chini ya Wizara yao.

Mheshimiwa Spika, ukizungumzia kwanza kuhusu Bodi ya Maziwa na mimi kule Makete nina shamba la Kitulo ambalo ni shamba bora na ni shamba zuri ambalo Wizara yenyewe inalisimamia kwa sababu liko chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi. Shamba lile juzi wakati nauliza swali hapa walinijibu kwamba Wizara inatenga kununua mitambo mitano ili kuliwezesha lile shamba kuendelea na uzalishaji wa maziwa. Mimi nisema jambo moja Wizara ninawaomba na ninawashauri ukiangalia hapa kwenye matumizi ya fedha ambapo tunazitumia kuagiza maziwa nchini ni zaidi ya shilingi bilioni 30 tunaagizwa kutoka nje kuleta kutoka nje kuleta ndani ya Tanzania, lakini Makete tuna shamba la Kitulo ambalo ng’ombe mmoja tu ana uwezo wa kutoa lita 50 kwa siku; je, Serikali haioni haja ya kuwekeza kwenye shamba lile ambalo kwa muda mrefu limekuwa likizorota, sasa hivi liko katika hatua ambayo kwa kweli haipendezi lakini eneo ni kubwa lipo.

Mheshimiwa Spika, niwaombe Wizara ili kukimbizana na hili jambo la maziwa njooni Makete kwenye shamba la Kitulo muwekeze. Wana Makete wako tayari wawekezaji wako tayari mfanye partnership na watu ili uweze kuwekeza tuwape maziwa ya kutosha, kwa sababu ukisoma kwenye hotuba ya waziri anazungumzia kwamba wanahitaji kuongeza vituo karibu 50 vya ukusanyaji wa maziwa nchini. Mnakusanya maziwa kutoka wapi wakati hamna mpango wa mkakati mzuri wa kuhakikisha mashamba haya ya Serikali ya uzalishaji wa maziwa yanatoa maziwa vizuri na naomba kwamba idadi ya ng’ombe waongezeke pale Kitulo.

Mheshimiwa Spika, lakini miundombinu ya shamba lile iongezeke, lakini pia maslahi ya wafanyakazi pale Kitulo yaboreshwa ili lile shamba liweze kufaidisha Watanzania wetu, lakini Wanamakete wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, lakini jambo lingine ambalo nataka nizungumzie ambalo jana Mheshimiwa Spika jana alizungumzia, suala la NARCO lisiwe tena mjadala Wizara ni lazima iende ijitathmini jinsi ya kuipa majukumu mapya NARCO.

Mheshimiwa Spika, na uzuri ni kwamba mnasehemu ya kuanzia kwenye kikao cha Baraza la Mawaziri nilizungumza Waraka wa Baraza la Mawaziri wa mwaka 2002 Waraka Namba 2 walionyesha kabisa kwamba NARCO kuna mambo ambayo wameshindwa, kuyafanya ni vema Serikali ikaingia sasa mkakati wa kuwapa private sector maeneo yale muweze kuyasimimamia na kuyaendesha.

Lakini pili nikazungumzia kwamba kwenye kikao cha Waziri Mkuu cha tarehe 26 Februari, 2016 pale Kagera na bahati nzuri na mimi nilikuwepo kwenye kikao hicho, Waziri Mkuu aliagiza akasema kubainisha mpango bora wa matumizi ya ardhi ya NARCO ili kama Serikali haina uwezo wa kuendesha tujue ni nani aweze kupewa mashamba hayo. Waziri Mkuu alitoa hapa mna sehemu ya kuanzia na Waziri Mkuu alikuwa ni huyu Kassim Majaliwa. (Makofi)

Mheshimiwa Spika, niwaombe watu wa Wizara ya Mifugo NARCO ibadilishieni majukumu ya kazi ili maeneo yale ambayo Spika mwenyewe ameyazungumzia kwamba yamebaki wazi muda mrefu, Watanzania na vijana wa Kitanzania waweze kupewa na Wizara iweze kuwasimamia mashamba yale yaweze kuendeshwa, kwa sababu ukiangalia Kagera tu ina ranchi karibu nne, NARCO kazi wanayoifanya kule Kagera ni kutatua migogoro, hawajikiti kwenye kutatua suluhisho la hizi ranchi ziwezekufanya kazi.

Mheshimiwa Spika, leo hii NARCO wanakuja na mpango wa mkakati wa kwamba Mtanzania awekeze kwa mkataba wa mwaka mmoja, hata mimba yenyewe ya huyo ng’ombe ndani ya mwaka mmoja haiwezi ikawa amepata mimba jamani, tusema jambo jema muwe na vitu vyenye tija kama Wizara kusaidia wananchi wetu utawekaje mkataba mwaka mmoja mtu akaweke uwekezaji pale, ongezeni kwenye majukumu kwenye NARCO iweze kufanya kazi ambayo sisi watanzania tutaona ina tija.

Mheshimiwa Spika, niendelee kusisitiza pia kwamba NARCO wenyewe watambue kwamba ule Mradi wa Ruvu na mtupe majibu leo hii hapa, Serikali mradi wa Ruvu wa shilingi bilioni 5.7 kwa nini hadi leo umelala huko kwenye coma, uko ICU, haujawahi endelea zaidi ya miaka kumi.

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa Mzungumzaji)

SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Festo Sanga.

MHE. FESTO R. SANGA: Mheshimiwa Spika, naomba muendelee kutupa majibu hayo ahsante. (Makofi)