Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Taska Restituta Mbogo

Sex

Female

Party

CCM

Constituent

Special Seats

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

1

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. TASKA R. MBOGO: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi kuchangia Wizara nyeti, Wizara ya Ulinzi. (Makofi)

Kwanza kabisa napenda nimpongeze Mheshimiwa Kwandikwa kwa hotuba yake nzuri sana aliyeitowa leo napenda niwapongeze wanajeshi wote nchini Tanzania kwa kazi nzuri sana ambayo wanaifanya kutulinda sisi wananchi, lakini pia kulinda mali zetu na kulinda nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika mchango wangu wa leo kabla sijaenda kwenye hoja ya Mheshimiwa Kwandikwa, napenda nizungumzie Mkoa wangu wa Katavi. Kwenye Mkoa wangu wa Katavi pale Mpanda Mjini mwaka 1984 kuna mnara uliwekwa pale maeneo ya Kampuni, lakini mwaka 1993 Jeshi liliondoa huo mnara, badaye mwaka 2020 ule mnara ulirudishwa pale na mwaka 2021 waliweza kufunga hiyo radar. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hoja yangu ni nini yale maeneo yanazungukwa na kata tatu, Kata ya Ilembo, Kata ya Mpanda Hotel, na Kata ya Msukumilo na hoja iliyopo Jeshi lilipokuja mwaka 1984 lilikuwa na hekari 100, liliporudi mwaka 2020 liliongeza yale maeneo na kuwa na hekari 2,200. Sasa katika maeneo yale walioongeza kuna shughuli za kijamii zinaendelea pale, kuna watu wanalima wanafuga, lakini pia kuna nyumba za watu ambazo zilikuwemo katika eneo hilo. Ombi langu kwa Wizara ya Ulinzi na kwa Mheshimiwa Waziri ni kwenda kutatua ule mgogoro ili wananchi pamoja na wanajeshi waweze kukaa kwa amani, kwa sababu kwa sasa hivi kinachoendelea wale wananchi wanapokatiza lile eneo la Jeshi kwenda kuangalia shughuli zao wanajeshi wanawapiga, lakini pia wanachoma nyumba zao na kuwanyang’anyia mali zao kama mabati. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hivyo basi, ili kuwe na amani na ili Jeshi kwa sababu ni Jeshi la wananchi, nilikuwa namuomba Mheshimiwa Waziri atafute muda ili aende Mkoani Katavi pale kwenye Wilaya ya Mpanda Mjini akaangalie hilo tatizo na aweze kulimaliza. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, niende kwenye hotuba ya Mheshimiwa Waziri; Mheshimiwa Waziri katika hotuba yake ameeleza changamoto ambazo anazikabili kwenye ukurasa wake wa 19; aya ya 78, 79 mpaka aya 80.

Mheshimiwa Naibu Spika, Mheshimiwa Waziri ameeleza kwamba tatizo analokabiliana nalo ni ukomo wa bajeti, ili nchi iweze kufanya mambo mengine, ili nchi iweze kutatua tatizo la maji, tatizo la umeme, tatizo la barabara, lakini pia ili wananchi waweze kufanya kazi kwa amani lakini pia wanajeshi wale wanatakiwa waongezewe marupurupu yao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ukiona bajeti hii ya Wizara ya Ulinzi inaukomo sasa bajeti ikiwa na ukomo na Mheshimiwa Waziri katika hizi aya nilizozitaja ameeleza kwamba ameshindwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi, ameshindwa kuwapeleka kusoma, kununua vifaa, lakini pia ameshindwa hata kutoa yale mahitaji muhimu yanayohitajika pale Jeshini kwa sababu ya ukomo wa bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ombi langu kwa Serikali bajeti ya Ulinzi, isiwekewe ukomo wa bajeti na hii itatusaidia sana sisi wananchi wa Tanzania ili tuweze kuishi kwa amani, lakini pia ili tuendeleze amani yetu iliyopo sasa hivi. Suala hili ni muhimu, nimeliona nilizungumze hapa la ukomo wa bajeti ili tuweze kuangalia tunalifanyia vipi kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ningependa kulizungumza leo ni mipaka ya nchi yetu. Mipaka ya nchi yetu mingi hakuna barabara na ndiyo maana tuna wahamiaji haramu wengi wanaingia nchini kwetu, utaweza ukajiuliza uko pale Mbeya au uko Dodoma mhamiaji haramu ameingiaingia vipi mpaka akafika hapa Dodoma na ameingilia wapi? Jibu unaweza ukajijibu mwenyewe kwamba ameingilia kwenye uchochoro wa mpakani kwa sababu hakuna barabara. (Makofi)

Kwa hiyo niiombe Serikali na nimuombe Waziri awasiliane na Waziri wa Ujenzi waangalie ni jinsi gani wataweza kuitengeneza barabara zinazozunguka nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni muhimu kwa sababu nchi yetu inapakana nan chi nyingi, inapakana na nchi za Rwanda, Burundi, Uganda, Msumbiji, lakini na nyingine nyingi. Sasa ili tuwe na uimara wa mipaka yetu na hili wale walinzi wa mipakani ambao ni wanajeshi wetu waweze kuwagundua kwa mapema wale wahamiaji haramu ni muhimu barabara zikawepo. Kwa sababu ukosefu wa barabara, mlinzi atakuwa amesimama hapa kwenye lindo, lakini yule mhamiaji haramu anapata upenyo wa kupita eneo lingine kwa sababu hakuna barabara inayonyooka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo nilikuwa naomba suala la barabara za mipakani lizingatiwe, lakini pia mipaka yetu ioneshwe, sisi tupo lakini kuna siku tutaondoka katika dunia hii, tunatakiwa kizazi kitakachokuja kikute mipaka ya nchi yetu ikiwa inafahamika vizuri. (Makofi)

Suala la mipaka nchi nyingi zimeweza kugombana kwa ajili ya mpaka wa hatua moja au mbili. Mheshimiwa manyanya alizungumza leo asubuhi kuhusu mpaka ulioko Ziwa Nyasa ndiyo utaangalia jinsi gani umuhimu wa kuweka mipaka yetu sasa hivi ili kizazi kinachokuja kikute mipaka yetu iko wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo ningependa kulizungumzia ni suala ambalo wengine wamelizungumza hapa kuhusu nyumba za wanajeshi wetu na kukaa uraiani. Ili kuweka ile dhana ya kusema huyu sasa ni mwanajeshi turudi kama jeshi lilivyokuwa zamani wale wanajeshi wakae katika kambi zao, wasikae uraiani, kwa sababu hii kwanza kikanuni inaweza ikapunguza ile sijui nitumie neno gani? Hali ambayo mwananchi anamuona kwamba huyu mwanajeshi ni mlinzi wa amani ya kwangu na ni mlinzi wa nchi, sasa inakuwa kwamba yule mwanajeshi anakaa nyumba moja na mwananchi wanatumia geti moja, labda wanatumia bafu moja, naona kama inapunguza kitu cha namna fulani, nimeshindwa kuweka maneno gani mazuri hapa, lakini maana yangu ilikuwa ni hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilikuwa naomba tulilirudishie jeshi letu heshima yake ya toka mwanzo kama jinsi lilivyoanzishwa. Nafahamu yapo mapungufu lakini kama tunaweza kutatua hili tatizo la makazi ya wanajeshi litatusaidia sana, majeshi yakae mahali pao, polisi wakae mahali pao japokuwa siyo bajeti yao hii, lakini nilitaka tu kusema hivi wale watu ambao kwa sababu wanajeshi wenyewe uwezi kumkuta mwanajeshi ameingia baa au polisi ujuwe huyo siyo mwanajeshi halali. Sasa kama huko kuna miiko basi na ukaaji vilevile wasichanganyike na rai ndiyo suala ambazo nilipenda kulizungumzia. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, suala lingine ambalo nilitaka kusema ni suala la la vile viwanda ambavyo vimeanzishwa na Jeshi letu la wananchi, kulikuwa wanajeshi waliwahi kutengeneza gari inaitwa Nyumbu, lakini sijui gari hiyo iliishia wapi.

Kwa hiyo wangekuwa wamewezeshwa na wale wataalamu waliokuwa waliotengeneza hiyo gari nafikiri sasa hivi wangeshatengeneza magari mengi, lakini pia Jeshi lina kiwanda cha kutengeneza uniform, kwa hiyo sioni hoja ile ya kusema mwanajeshi anakosa uniform wakati kuna kiwanda cha kutengeneza uniform na nilivyosoma kwenye hii taarifa ya Mheshimiwa Waziri kile kiwanda kina uwezo wa kutengeneza uniform 400 kwa siku. Sasa kama kina uwezo wa kutengeneza 400 kwa nini mwanajeshi akose uniform, ni kwamba sisi tumekosa kuwapa zile fedha/mitaji ya kununua zile material ili waweze kutengeneza hizo uniform. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo ombi langu kwa Serikali ni kuangalia hivi vitu ambavyo viko viwanda na tunafahamu wanaviwanda wanamambo ya kilimo ambayo yameanzishwa na wanajeshi na ambayo kwa kweli yanawasaidia sana kujitegemea wao wenyewe kwa wenyewe. Kwa hiyo, nilikuwa naomba sisi tuweke input tuporeshe kama ni hivyo viwanda Serikali iweke pesa hizo uniform zitengenezwe hakuna haja ya kusimama hapa na kusema kwamba wanajeshi hawana uniform wakati wanakiwanda cha kutengeneza uniform zao wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi na naunga mkono hoja. (Makofi)