Jamhuri ya Muungano ya Tanzania

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Hon. Ramadhan Suleiman Ramadhan

Sex

Male

Party

CCM

Constituent

Chake Chake

Contributions

nil

Answers

nil

Commettees

2

Ministries

nil

Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2021/2022 – Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi nipate kuchangia mawazo yangu na mawazo ya wananchi wa Jimbo la Chakechake kwenye Wizara hii ya Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, na mimi nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mama yetu, Mama Samia Suluhu Hassan kwa kuwa Amiri Jeshi Mkuu wa kwanza mwanamke wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, pia nichukue fursa hii kumpongeza Waziri kwa hotuba nzuri ambayo ametuelezea dira na mwelekeo wa Wizara yake katika mwaka wa fedha 2021/2022 nimpongeze sana kwa kazi iliyotukuka. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, leo sipo vizuri sana kiafya, kifua kidogo na homa homa kwa hiyo utanivumilia, nilipanga kusema mengi lakini inawezekana katokana na hiyo hali nikapunguza kidogo yale ya kusema. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sisi tunaotoka kwenye majimbo ya visiwani Zanzibar tukisema ile dhana ya local content kwa mfano kwenye maeneo ambayo Mungu amewabariki kuwa na migodi inaweza isiwe inafahamika vizuri kwenye akili za wengi wanaotoka kwenye visiwa. Kwa sababu sisi hatujabarikiwa kupata maeneo ambayo yana uchimbaji wa dhahabu.

Mheshimiwa Naibu Spika, lakini sisi tumebarikiwa kupata maeneo mengi ambayo yamezungukwa na Kambi za Jeshi, kwa hiyo, ile dhana ya local content inaweza ikatumika mutatis mutandis kutoka kwenye dhana ya wenzetu ambao Mungu amewabariki kupata migodi na sisi ambao tumezungukwa na kambi za Jeshi. Dhana ya local content kwenye kambi za Jeshi ni vile tunavyoweza kutumia uwepo wa kambi za Jeshi kwenye maeneo yetu kama fursa. Kambi za Jeshi zikiwepo kwenye maeneo yetu kwenye majimbo yetu maana yake hiyo ni fursa ya wewe kupata Kituo cha Afya ambacho kitajengwe ndani Kambi ya Jeshi, kupata shule ambazo zinajengwa ndani ya kambi za jeshi na huduma za kijamii nyingine, kwa mfano, mimi kwenye Jimbo langu sina Kambi ya Jeshi lakini jirani yangu Jimbo la Wawi wao wanazo kambi za jeshi zaidi ya moja, ipo hospitali katika Kambi ya Jeshi ya Ali Khamis Camp ambayo imekuwa ina msaada mkubwa kwa wananchi wa Wawi na wananchi wa Chakechake, maana yake nje na zaidi ya Jimbo ambapo kambi ipo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, hospitali imekuwa ikihudumia watu, raia wengi wamekuwa wakienda kwenye hospitali hizo kupata huduma, kwa hiyo rai yangu kwa Mheshimiwa Waziri ni kwamba hizi hospitali zinatakiwa zipewe uwezo kwasababu sasa zimekuwa ni sawa sawa na hospitali za kiraia kwa jinsi zinavyohudumia hata wasiokuwa wanajeshi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika Wilaya nzima ya Chakechake sisi tumebahatika kuwa na hospitali moja ya Wilaya ambayo ndio ina sehemu za kuhifadhia maiti/ majokofu ya kuhifadhia maiti. Ushauri wangu ni kwamba tunaomba kuongezewa uwezo kwa hospitali ya Jeshi iliyoko kwenye kambi ya Ali Khamis Camp ili iwe na uwezo wa hifadhi maiti, kwa sababu Hospitali ya Chakechake haitoshi inakuwa inamezwa na mzigo, inabebeshwa mzigo mkubwa wa kuhifadhi maiti jambo ambalo halina uwezo huo. Kwa hiyo mbadala ni kuiwezesha kambi ili hospitali iliyopo kwenye Ali Khamis Camp ili liwe na Mortuary ambayo itasaidia hii Hospitali ya Chakechake kubwa ya Wilaya pale inapotokea mahitaji maalum. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la pili ambalo nilitaka kuchangia ni suala la uwekezaji wa jeshi kwenye tafiti za kisayansi, hili limesemwa sana jirani yangu Engineer kalisema, Mzee wangu Mheshimiwa Maige kalisema na Wabunge wengi waliochangia mwanzo wamelisema kwa msisitizo. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, katika maeneo ambayo sasa yameshakwenda mbele zaidi kwenye maendeleo ya kisayansi na teknolojia huko duniani ni uwekezaji na utumiaji wa sayansi kwenye majeshi; in terms ya silaha, in terms ya mbinu za kupigana, hizo drones tunazoziona (ndege zisizo na rubani) zimegundulika kutokana na vyuo vya kitafiti vya kijeshi. Kwa hiyo na mimi nataka niweke msisitizo hapa, dunia haipo tena tulipo sisi, watu walishakwenda mbele zaidi, leo watu wanateknolojia za kuzuia makombora kabla ya kufika maeneo yao yakiwa yamelengwa kuelekea kwao. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, watu wana launch rocket za kijeshi, kwa hiyo hatuwezi kufika huko kama hatujawekeza fedha nyingi kwenye maabara za kijeshi za kuweza kufanya tafiti za kisasa ili na wao jeshi letu tulipe uwezo wa kufanya ugunduzi wa silaha mpya na teknolojia mpya za kjeshi ambazo zitalipa uwezo jeshi letu kwenye kulinda mipaka na kufanya ile kazi waliyopewa kikatiba. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, miaka 2000-2005 wakati tunamaliza form four kulikuja ile dhana ya mapinduzi ya wasomi ndani ya jeshi, tulikuwa tunashawishiwa kwa sababu mimi wakati ninamaliza muda huo nilikuwa ninasoma shule ya jeshi, kwa hiyo, tulikuwa tunashawishiwa tuingie jeshi tulikuwa tukiambiwa kuna mapinduzi ya kwamba jeshi sasa linataka wasomi kwa hiyo ili hao wasomi wawe na faida ambazo sasa hivi wapo wengi ndani ya jeshi ni wengi wengi wengi wapo, ili wawe na faida ni lazima tuwekeze kwenye maabara za kisasa za kisayansi zitakazowasaidia wasomi wetu kutumia elimu zao ili kulisaidia jeshi letu la ulinzi na usalama kutulinda kisayansi zaidi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, la tatu pia ambalo nilitaka kulisema ni kuhusiana na suala la ajira; juzi kulikuwa kuna kikao cha kiutendaji baina ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar pamoja na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mheshimiwa Mchengerwa kilifanyika Zanzibar tarehe 12 Mei, 2021; moja katika vitu walivyovijadili ilikuwa ni nafasi sawa za ajira katika vyombo vya Muungano. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, Jeshi ni chombo cha Muungano, kwa hiyo, zinapotoka nafasi za ajira utaratibu tunatakiwa Zanzibar wapewe asilimia 21 ya nafasi hizo za ajira. Kwa hiyo ninasisitiza na hili Mheshimiwa Waziri alichukue na alifanyie kazi zinapotoka nafasi za ajira tunao vijana wengi mimi ndani ya Jimbo langu Chakechake wapo vijana wengi wasomi wamemaliza degree, wamemaliza form six, wamemaliza form four, wapo mtaani na wao wanahitaji hizo ajira zikiwa zinatoka itazamwe Zanzibar kwenye hiyo asilimia 21 ili na sisi tupate nafasi ya kuwa sehemu ya Jeshi la Ulinzi. (Makofi)

Mheshimiwa Naibu Spika, nilitaka kusema chochote kuhusiana na yale maelezo ambayo uliyasema pale maana yake yale maelezo yalijitosheleza kuhusiana na dada yangu Mheshimiwa Jenista alipotoa utaratibu wa Kanuni ya 71 wa Kanuni za Kudumu za Bunge pamoja na Ibara ya 34 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, lakini cha kushangaza mtu anashangaa kwa nini mwanajeshi anakwenda kwa Mkuu wa Mkoa, lakini mtu hashangai kwa nini mwanajeshi ni daktari anatibu raia wake wenye jamii. Unaogopa mwanajeshi akiwa Mkuu wa Mkoa tu na magwanda…

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, taarrifa.

NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramandan kuna taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Esther Matiko.

T A A R I F A

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kumpa taarifa Mheshimiwa Ramadhan kwamba kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 63(2) na (3) imetoa mamlaka kwa Bunge kuishauri na kuisimamia Serikali na vyombo vyake. Kwa hiyo, pale nillikuwa ninatimiza wajibu wangu wa kuishauri Serikali kwa mujibu wa Katiba kama Mbunge. (Makofi)

NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, humu ndani humu, Kanuni zetu ziwe zinatuongoza vizuri. Nilitoa mwongozo kuhusu utaratibu ulioombwa na Mheshimiwa Jenista na sasa amesimama Mheshimiwa Esther Matiko akieleza kwamba yeye alifanya jukumu lake, nadhani nilieleza kwa kirefu kabisa kwamba Rais hafungwi na ushauri unaotolewa, kwa hiyo wewe umefanya kazi yako na yeye anachangia vile aonavyo bora kama wewe ulivyofanya ya kwako. (Makofi)

Mheshimiwa Ramadhan Suleiman Ramadhan malizia mchango wako.

MHE. RAMADHAN SULEIMAN RAMADHAN: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana na naendelea, ni kwamba wanajeshi hawa hawa ndio madaktari wetu kwenye hizo jamii zetu na magwanda yao wanatutibu na wala hatuwaogopi, ni walimu mimi kwenye Jimbo langu wapo wanajeshi ni walimu mpaka wa madrasa. Kwa hiyo wamefanya urafiki na jamii kiasi kwamba wao kwa sababu ni ndugu zetu, hao hao wanajeshi baadaye wanarudi kwa sababu ni baba au ni mjomba unamuogopaje mjomba! Hiyo ndio ambayo nilitaka nichangie.

Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo mimi nilitaka kuishia hapo, ahsante sana kwa kupata hii fursa na ninaunga mkono hoja. (Makofi)